Walioenguliwa Tanzania hawajui hatima yao kuhusu uchaguzi | Matukio ya Afrika | DW | 08.09.2020
  1. Inhalt
  2. Navigation
  3. Weitere Inhalte
  4. Metanavigation
  5. Suche
  6. Choose from 30 Languages
Matangazo

Matukio ya Afrika

Walioenguliwa Tanzania hawajui hatima yao kuhusu uchaguzi

Kuna idadi kubwa ya wagombea wa upinzani nchini Tanzania ambao hawajui hatma yao katika uchaguzi mkuu baada ya majina yao kuenguliwa katika hatua za mwanzo za urejeshaji wa fomu.

Wagombea hao sasa wanaendelea kutegea sikio maamuzi yatakayotolewa na Tume ya Taifa ya Uchaguzi inayoshughulikia rufaa zao wakati kampeni za uchaguzi huo zikizidi kupamba moto. 

Idadi yao inatajwa kuwa kubwa na wengi wao ni wale waliojitokeza kuwania nafasi za ubunge na udiwani kwenye uchaguzi wa Oktoba, ambao joto lake limeendelea kupanda kwa kasi kutokana na mvutano mkali wa hoja unaoendelea kuhushudiwa kwenye majukwaa ya kampeni.

Vyama vilivyokumbwa na kadhia hiyo ya wagombea wake kupigwa kalamu nyekundu na wasimamizi wa uchaguzi, ni kutoka chama kikuu cha upinzani, Chadema chama cha ACT Wazalendo, Chama cha NCCR Mageuzi na chama cha wananchi Cuf ambacho kimezindua kampeni zake jana katika mikoa ya kusini.

Karibu wagombea wote wamefikisha malalamiko yao katika tume ya taifa ya uchaguzi NEC ambayo hadi sasa bado haijabainisha ni lini itayatolea maamuzi malalamiko hayo.

Kuchelewa kutolewa kwa maamuzi hayo kumevifanya baadhi ya vyama hivyo na wagombea wenyewe kuingiwa na wasiwasi hasa wakati huu ambapo wagombea wa chama tawala CCM wakiendelea kuchanja mbuga kwenye majukwaa ya kampeni.

Walioenguliwa bado wanasubiri uamuzi wa tume ya uchaguzi

Walioenguliwa bado wanasubiri uamuzi wa tume ya uchaguzi

Akizungumzia suala hilo la rufaa, mkurugenzi wa habari, mawasiliano ya umma na uenezi wa chama cha wananchi Cuf, Mohammed Ngulangwa licha ya kuonyesha matumaini yake kwa tume hiyo, hata hivyo anaona kuchelewa kutoa maamuzi kwa wakati kunawaweka kihoro juu wanasiasa wengi.

Kumekuwa na ripoti zinazosema kwamba baadhi ya wagombea walioenguliwa wamekuwa wakipiga hodi mara kwa mara katika ofisi za tume hiyo kwa lengo la kutaka kujua majaliwa yao.

Mgombea mmoja wa ubunge huko Singida Magharibi kupitia chama cha ACT Wazalendo, aliyeenguliwa amelazimika kurejea jijini Dar es salaam kujitafakari upya baada ya kushindwa kuanza kampeni zake.

Hali kama hiyo imejitokeza pia kwa wagombea wengine, ambao wanakesha wakitafakari kuhusiana na hatma zao kisiasa kutokana na kizingiti hicho walichokumbana nacho katika hatua za awali.

Tume hiyo ilikuwa imepanga kuanza kuzisikiliza rufaa hizo zinazofikia 557 kuanzia Septemba Mosi.