1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Walimu wakatazwa kuvaa hijabu shuleni

P.Philipp - (P.Martin)27 Februari 2009

Shirika la Haki za Binadamu-Human Rights Watch- katika ripoti yake mpya limekosoa sheria zilizopitishwa na baadhi ya majimbo ya Ujerumani,kuzuia vazi la hijabu katika ofisi za kiserikali.

https://p.dw.com/p/H2a4

Mdahalo wa vazi la kujifunika kichwa na mtandio-hijabu- umezuka upya nchini Ujerumani.Wanasiasa na majaji wanajirahisishia wanapomtumia mwalimu kuzuia vazi la hijabu.Sheria hiyo haiwaathiri walimu wengi kwani si Waislamu.Na miongoni mwa walimu wa kiume huku Ujerumani ni shida kumuona Myahudi alievaa kofia au Kippah akisomesha darasani.Kwa hivyo sheria hiyo inawaathiri Waislamu wachache waliojijumuisha Ujerumani hadi kuwa walimu na wapo tayari kuwa sehemu ya jamii bila ya kuacha dini na ishara zingine za dini yao.

Sasa ni kipi wanachohofia hao wanasiasa na wanasheria?Je,wana wasiwasi kuwa walimu wa Kiislamu wanaovaa hijabu shuleni watawaslimisha watoto wa Kijerumani?Hiyo wala haiwezi kuwa sababu. Ikiwa watafanya hivyo basi wanapaswa kukatazwa sawa na mwalimu wa Kikristo asieruhusiwa kufanya kazi ya umishionari shuleni.

La kuamua iwapo mwalimu afukuzwe kazi ni elimu yake.Kwa maneno mengine kilicho ndani ya kichwa ni muhimu na sio kile kilicho juu ya kichwa.Mwalimu kukatazwa kuvaa hijabu vile vile hutoa ishara nyingine ya mashaka: Watoto watahisi kuwa ni kosa na ni marufuku kuvaa hijabu.Kwa hivyo baadae watakuwa na fikra hiyo watakapokabiliana na Waislamu waliovaa hijabu-na siku hizi hao wanakutikana kote Ujerumani.

Utengano na ubaguzi unaidhinishwa rasmi kwa sheria kama hiyo.Kwa kisingizio cha kutaka kuzuia mwelekeo wa sera kali,mtu mzima mwenye akili zake anakatazwa kuvaa kile anachohisi kuwa ni muhimu sana kwa dini yake. Ikiwa ni kutetea wanawake ili wasilazimishwe kuvaa hijabu basi ifanywe kama ilivyokuwa huko Ufaransa.Wasichana wapigwe marufuku kuvaa hijabu shuleni.Lakini ikubaliwe kuwa mwalimu alie mtu mzima ana uhuru wa kujiamulia kile atakachovaa.

Au inaweza kuelezwa kama ilivyokuwa kuhusika na uamuzi wa msalaba shuleni: Mwanzoni Mahakama ya Katiba ya Ujerumani iliamua kuwa msalaba usiruhusiwe kwenye kuta za darasani ikiwa unakera wengine. Lakini ukweli wa mambo ni tofauti kabisa siku hizi: Anaekereka basi ana chaguo jingine. Ikiwa ni hivy, basi anaeudhika kuona hijabu vile vile aende darasa jingine.Ukweli uliopo ni kuwa katika kesi hizo maarufu kuhusu hijabu hakuna mzazi alielalamika bali daima walikuwa watumishi wa serikalini au wanasiasa. Na bila shaka hapo kuna maslahi mengine na wala hayahusiki na elimu katika shule za Ujerumani.