1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Wakulima Kenya kunufaika kutokana na nishati ya mvuke

Wakio Mbogho1 Novemba 2018

Sekta ya kilimo nchini Kenya inatarajiwa kufaidika pakubwa kutokana na mbinu za ubunifu za matumizi ya nishati ya mvuke mashambani. 

https://p.dw.com/p/37Woz
Picha: Getty Images/AFP/T. Karumba

Wakulima nchini Kenya watanufaika kutokana na ushirikiano na kampuni ya kuzalisha nishati ya mvuke GDC kupitia matumizi ya nishati hiyo kwenye kilimo.

Wakati Kenya inajizatiti kuchimba nishati hii kwa wingi ili kupunguza gharama ya bidhaa hiyo muhimu kwa wananchi, sekta ya kilimo inatarajiwa kufaidika pakubwa kutokana na mbinu za ubunifu za matumizi ya nishati hiyo mashambani. 

Kampuni ya kuzalisha umeme nchini Kenya, GDC imeanza mipango ya kuchimba kawi zaidi katika maeneo yaliyo na idadi kubwa ya watu na ambao wanashiriki kilimo kwa kiwango kikubwa katika maeneo ya bonde la ufa.

Meneja wa maswala ya mazingara katika kampuni hiyo Gabriel Wetang'ula ameeleza kuwa hatua hiyo ya upanuzi itawawezesha pamoja wa washirika wao kubuni njia zaidi za matumizi ya mvuke unaochimbwa hasa katika kuimarisha sekta ya kilimo.

Ushirikiano huo unatarajiwa utawafaa wakulima kwa kuwa unawapa hursa ya kushiriki miradi ya kuboresha kilimo na hatimaye kuongeza mazao yao.
Ushirikiano huo unatarajiwa utawafaa wakulima kwa kuwa unawapa hursa ya kushiriki miradi ya kuboresha kilimo na hatimaye kuongeza mazao yao.Picha: Getty Images/AFP/Y. Chiba

Kando na mvuke huo kutumiwa kutengeza umeme, utatumika pia kupasha joto mashamba, kusindika maziwa, kukausha nafaka, katika kilimo cha samaki, kati mengine. Tayari baadhi ya wakulima wanaofuga samaki na wanaokuza tomato na pilipili hoho kupitia vyumba vya joto karibu na mradi wa Menengai wa kampuni hiyo wameshaanza kunufaika na huduma hiyo.

Mvuke huo hutumika kupasha joto na kutengeza mazingara yanayofaa kwa kilimo cha samaki na ukuzaji wa mboga. Joto kutoka kwenye kawi ya mvuke vilevile huimarisha uzalishaji wa chakula kwa kupunguza mavamizi ya magonjwa na wadudu wa mimea.

Dr Immaculate Maina, waziri wa kilimo katika serikali ya kaunti ya Nakuru ana imani kuwa ushirikiano huo utawafaa wakulima kwa kuwa unawapa hursa ya kushiriki miradi ya kuboresha kilimo na hatimaye kuongeza mazao yao.

Sekta ya kilimo inatarajiwa kufaidika pakubwa kutokana na mbinu za ubunifu za matumizi ya nishati hiyo mashambani. 
Sekta ya kilimo inatarajiwa kufaidika pakubwa kutokana na mbinu za ubunifu za matumizi ya nishati hiyo mashambani. Picha: picture alliance/Photoshot

Halikadhalika, ametaja kuwa mashirika ya kilimo katika eneo hilo yaliyokuwa yameporomoka kutokana na ukokesekanaji wa kawi yenye gharama nafuu, sasa yana nafasi ya kuchipuka tena.

Kampuni ya GDC ilianza kuchimba kawi katika eneo la Menengai, kaunti ya Nakuru Februari mwaka 2011 na tayari imechimba visima 35 vinavyotoa mvuke wa 167MW. Kenya imekuwa ikiimarisha jitihada za kuchimba kawi zaidi ya mvuke ili kuongeza kiwango cha bidhaa hiyo muhimu kuweza kukimu mahitaji ya watu wake.

Aidha, itazingatiwa kuwa matumizi ya kawi ya mvuke yanaendana na kiwango stahiki cha utoaji wa hewa chafu ya kaboni kulingana na sheria za kimataifa.

 

Mhariri: Iddi Ssessanga