Wakimbizi wa Sudan Kusini watiririka Ethiopia | Matukio ya Afrika | DW | 16.04.2014
  1. Inhalt
  2. Navigation
  3. Weitere Inhalte
  4. Metanavigation
  5. Suche
  6. Choose from 30 Languages
Matangazo

Matukio ya Afrika

Wakimbizi wa Sudan Kusini watiririka Ethiopia

Takribani wakimbizi 1000 kutoka Sudan Kusini huingia nchini Ethiopia kila siku, wengi wao wakiwa katika hali mahtuti. Haya yameelezwa na Umoja wa Mataifa, ambao pia umesema 95% ya wakimbizi hao ni wanawake na watoto.

Wakimbizi kutoka Sudan Kusini ndani ya kambi nchini Ethiopia

Wakimbizi kutoka Sudan Kusini ndani ya kambi nchini Ethiopia

Shirika la Umoja wa Mataifa linalowashughulikia wakimbizi UNHCR limesema tangu kuzuka kwa mapigano nchini Sudan Kusini, wakimbizi wanaovuka mpaka kuingia Ethiopia ni kati ya 800 na 1000 kila siku. Msemaji wa shirika Ariane Rummery ameiambia DW kwamba idadi yao inazidi kuongezeka sio nchini Ethiopia tu, bali pia katika mataifa mengine jirani.

''Nchini Ethiopia pekee tumekwishapokea wakimbizi wanaozidi 95,000, na katika nchi nyingine jirani, Uganda Sudan na Kenya wapo wakimbizi wapatao 290,000 kutoka Sudan Kusini. Bila kusahau kuwa hata ndani ya Saudan Kusini kwenyewe wapo watu 800,000 walioyahama makazi yao ambao wanahitaji msaada.'' Amesema Rummery.

Masaibu makubwa njiani

Kwa mujibu wa UNHCR, wale wanaowasili katika mkoa wa Gambella nchini Ethiopia wanakuwa wametembea kwa muda wa majuma matatu, na wengi wanakuwa katika hali mahtuti. Msemaji wa shirika la kuwahudumia wakimbizi Ariane Rummery anasema wanawasili wakiwa na simulizi za kutisha kuhusu masaibu yaloyowakuta njiani.

Wakimbizi hao wanasema njia wanayopita ni matatizo matupu

Wakimbizi hao wanasema njia wanayopita ni matatizo matupu

''Wanaelezea walivyotembea muda mrefu bila kupata chakula hata kidogo. Utapiamlo miongoni mwao huwa ni wa kiwango kikubwa, na watoto wapatao 4000 wamewekwa kwenye mpango maalumu wa lishe. Hali kadhalika akina mama 3,500 wanaonyonyesha wanapewa vyakula maalumu kuboresha afya yao. Hayo yanakupa sura halisi ya matatizo wanayowasili nayo kambini.'' Rummery amesema.

Vita vinavyoendelea nchini Sudan Kusini ambavyo vimechukua mrengo wa kikabila, vimekwishaangamiza maisha ya maelfu ya watu. Makabila yanayohusika zaidi katika vita hivyo ni Dinka analotoka rais Salva Kiir, na Nuer la aliyekuwa makamu wake na ambaye sasa ni kiongozi wa waasi, Riak Machar.

Msimu wa mvua wabisha hodi

Wakati huu msimu wa mvua kubwa unapokaribia, UNHCR na mashirika mengine ya msaada wanafanya kila juhudi kujenga kambi mpya katika maeneo yaliyoinuka ndani ya Ethiopia.

Mapigano nchini Sudan Kusini yamedumu kwa zaidi ya miezi mitano

Mapigano nchini Sudan Kusini yamedumu kwa zaidi ya miezi mitano

Tayari UNHCR imekwishahamisha watu kutoka kambi ya Kule ambayo ilikuwa bondeni, na kuanzia jana shughuli zilianza kuwahamisha wale walioko Leitchour.

Mbali na wale ambao tayari wanaishi kambini nchini Ethiopia, wapo wengine takribani 10,000 ambao wamesalia katika eneo la mpaka baina ya nchi mbili.

Kwa ushirikiano na serikali ya Ethiopia, shirika la UNHCR linajenga kambi nyingine ambayo itakuwa tayari kuwapokea wakimbizi 30,000 mwishoni mwa mwezi hu wa Aprili.

Kambi nyingine yenye uwezo wa kuwapa hifadhi watu 50 inajengwa kwenye eneo la Pagak lililo mpakani baina ya Ethiopia na Sudan Kusini.

Huku hayo yakijiri, kiongozi wa waasi, Riak Machar ameliambia shirika la habari la AFP kwamba amepania kupigana hadi kuukamata mji mkuu Juba, na kuonya kuwa vita hivi haviwezi kumalizika hadi pale rais Salva Kiiir atakapofukuzwa madarakani. Tayari vita hivyo vimedumu kwa miezi mitano.

Mwandishi: Daniel Gakuba/AFPE/Interview

Mhariri:Josephat Charo

DW inapendekeza