Wakimbizi wa Iraq nchini Syria | Masuala ya Jamii | DW | 15.03.2007
 1. Inhalt
 2. Navigation
 3. Weitere Inhalte
 4. Metanavigation
 5. Suche
 6. Choose from 30 Languages

Masuala ya Jamii

Wakimbizi wa Iraq nchini Syria

Wakati hali inaendelea kuwa ngumu nchini Iraq, Wairaqi millioni mbili walikuwa wamekimbia kutoka nchi yao, wangi wao kwenye nchi jirani, hasa Jordan na Syria. Wairaqi wengi wanaingia nchi hizo kama watalii baada ya kuuza makazi yao nchini Iraq. Hii ndiyo sababu mashirika yasiyo ya kiserikali yanaamini kuwa idadi ya wakimbizi inaweza kuwa mara mbili kubwa kuliko inavyojulikana. Mwandishi wetu Karin Leukefeld aliwatembelea Wairaqi wanaoishi Syria.

Wairaqi wanaotemebela kaburi ya Sayedah Zaynab mjini Damaskus

Wairaqi wanaotemebela kaburi ya Sayedah Zaynab mjini Damaskus

Ni wakati wa chakula cha mchana. Tumo katika mkahawa wa nyama ya Kebab uitwao “Beit Iraki”, maana yake ni “nyumba ya Iraq”. Lakini nchi hii si Iraq bali tuko nchini Syria, katika mtaa nje ya mji wa Damaskus.

Mwenye mkahawa ni Abu Maan ambaye alikuja Syria mwaka mmoja uliopita. Kabla ya hapo aliishi Baghdad ambapo maisha yake kama mfanyabiashara yalikuwa mazuri – mpaka biashara yake iliporwa. Halafu hali ilikuwa mbaya zaidi, anaeleza mzee Abu: “Nilitekwa nyara mara tatu. Hatuna serikali nchini Iraq. Kwa kawaida wahalifu wanashikwa na kuadhibiwa, hata ikiwa wanapiga risasi hewani tu. Lakini serikali hii hata haijali watu wanaotumia makombora. Hakuna usalama.”

Na ndiyo sababu, Abu Maan alikimbilia Syria. Idara ya Umoja wa Mataifa inayoshughulikia masuala ya wakimbizi, UNHCR, ilisema kukimbia kwa Wairaqi kutoka nchi yao ni tukio kubwa zaidi la uhamiaji tangu kufukuzwa Wapalestina mnamo mwaka 1948. Nchini Syria sasa kuna Wairaqi Millioni moja, wengi wao wakiwa mjini Damaskus.

Tayari kabla ya jua kuchomoza, uwanja mbele ya jengo la UNHCR mjini Damaskus umejaa wakimbizi. Kila siku mamia ya wakimbizi kutoka Iraq huandikishwa. Wakimbizi hupewa vitambulisho ambavyo vinawasaidia kupata elimu na huduma za afya za bure. Wanasubiri hapa wanaonekana wamechoka sana.

Mmoja wao ni Jeanne Jamil Mansour. Baba yake aliuawa, kaka yake alitekwa nyara na mama yake alijeruhiwa vibaya na kupelekwa hospitali, Bibi huyu ametuambia: “Niko hapa kwa miaka mitatu sasa. Hakuna mtu yeyote anayetusaidia. Tuende wapi basi, nani atatusaidia sisi Wairaqi, Waislamu na Wakristo? Unaona vile ninavyotetemeka, nisemaje?”

Syria ni nchi ya pekee ambayo mpaka wake na Iraq bado uko wazi. Lakini idadi kubwa ya wakimbizi wanaoingia kutoka Iraq imebadilisha maisha ya mjini Damakus, yaani bei zimepanda sana, hasa kodi za nyumba. Pia inazidi kuwa ni vigumu kupata kazi.

Umoja wa Mataifa umeomba Dola Millioni 60 kwa ajili ya kuwasaida wakimbizi nchini Syria. Laurens Jolles, mwakilishi wa UNHCR mjini Damaskus juu ya mahitaji nchini Syria: “Tunahitaji fedha hizo kuhakikisha huduma za afya na kusaidia katika mfumo wa elimu. Shule za hapa Syria zimejaa kabisa. Hakuna walimu wa kutosha, lazima shule mpya zijengwe na nyingine zirekebishwe. Halafu wakimbizi wengi hawana uwezo wa kujipatia chakula. Lazima tuwasaidie. Na pia kusaidia katika mfumo wa taifa wa afya.”

Bw. Jolles lakini pia anahisi kuwa kuwepo wakimbizi wengi hivi kunazusha wasiwasi katika jamii ya Syria, na ndiyo sababu, anasema, inabidi kuwasaidia wakimbizi ili kuhakikisha usalama.

 • Tarehe 15.03.2007
 • Mwandishi Karin Leukefeld / Maja Dreyer
 • Chapisha Chapisha ukurasa huu
 • Kiungo https://p.dw.com/p/CHlS
 • Tarehe 15.03.2007
 • Mwandishi Karin Leukefeld / Maja Dreyer
 • Chapisha Chapisha ukurasa huu
 • Kiungo https://p.dw.com/p/CHlS

Unaweza kusikiliza matangazo yetu hapa

Kusikiliza matangazo ya Idhaa ya Kiswahili ya DW, tafadhali bonyeza alama ya spika ya masikioni hapo chini, na kuwasiliana nasi, tafadhali tuandikie moja kwa moja kupitia: kiswahili@dw.com