Wakimbizi wa Burundi Tanzania waahidiwa amani nyumbani | Makala | DW | 04.10.2019
  1. Inhalt
  2. Navigation
  3. Weitere Inhalte
  4. Metanavigation
  5. Suche
  6. Choose from 30 Languages
Matangazo

Makala

Wakimbizi wa Burundi Tanzania waahidiwa amani nyumbani

Ahadi kwa wakimbizi wa Burundi wanaotaka kurejea nyumbani kutoka Tanzania, juhudi za kupambana na maradhi ya Ebola na ushawishi wa nchi za Ulaya barani Afrika ni miongoni mwa mada za Afrika magazetini wiki hii

Tunaanzia Tanzania ambako wakimbizi wa Burundi waliokuwa wakiishi nchini humo wameombwa warejee nyumbani kwa ahadi kwamba nchi yao ni salama. Gazeti la Frankfurter Allgemeine linazungumzia  kuhusu ahadi zenye mashaka na kuandika: "Pale waziri wa mambo ya ndani wa Burundi Pascal Barandagiye alipoitembelea kwa muda mfupi nchi jirani ya Tanzania, aliipigia upatu nchi yake akisema "Usalama na Utulivu" unanawiri upya nchini Burundi na kwamba serikali inaidhibiti kikamilifu hali ya mambo.

Frankfurter Allgemeine linasema matamshi hayo ya waziri Barandagiye ameyakusudia  serikali ya Tanzania sawa na Waburundi ambao malaki wanaishi katika kambi za wakimbizi nchini Tanzania. Ikiwa matamshi hayo yanawafurahisha maafisa wa serikali ya rais John Magufuli, lakini kwa wakimbizi wa Burundi yanazuwa mashaka. Mashaka kuelekea ahadi za waziri wa ndani wa Burundi zimesikika pia kutoka jumuia ya ushirikiano kusini mwa Afrika SADC, linaandika gazeti la Frankfurter Allgemeine.

Juhudi za kupambana na Ebola

Mada nyengine iliyogonga vichwa vya habari vya magazeti ya Ujerumani kuhusu bara la Afrika wiki hii inahusiana na maradhi ya kuambukiza ya Ebola yanayotishia maisha sio tu katika Jamhuri ya Kidemokrasi ya Kongo bali pia katika nchi jirani ambazo baadhi zimeshaanza kuchukua hatua za tahadhari. Gazeti la mjini Berlin, die tageszeitung au taz kama linavyojulikana kwa ufupi, linaandika kuhusu juhudi za Josua Kakule ambae binafsi awali  kabla ya kuambukizwa alikuwa akiyataja maradhi ya Ebola kuwa ni ya kubuni .

Hivi sasa  padri huyo wa zamani Josua Kakule ameamua kupanda piki piki na kuingia vijijini kuwatanabahisha wananchi kuhusu hatari ya maradhi ya Ebola . Anajaribu kuwafumbua macho watu watambue kwamba virusi vya Ebola havijaletwa na mashetani. Gazeti la die tageszeitung linakumbusha watu zaidi ya 2,100 wamefariki dunia tangu Agosti mwaka 2018 katika maeneo ya mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasi ya Kongo kutokana na Ebola. Na kwa mujibu wa ripoti zilizochapishwa hivi karibuni, hadi septemba 29 iliyopita, watu 2133 wamekufa kutoka watu 3191 walioambukizwa virusi vya Ebola.

Ujerumani yasaidia kupambana na Ebola

Maradhi hatari ya Ebola yameripotiwa pia na gazeti la Süddeutsche Zeitung linalozungumzia juhudi za Ujerumani kusaidia kupambana na maradhi hayo. Gazeti linasema Ujerumani imechangia Euro milioni moja katika mkutano wa wafadhili wa Umoja wa Afrika kwa lengo la kupambana na Ebola. Süddeutsche Zeitung limemnukuu msemaji wa wizara ya afya akisema fedha hizo zitatumika kupanua shughuli za kituo cha udhibiti na kinga ya maradhi ya Ebola. "Tutakapotambua mapema hatari ya kuripuka maradhi ya Ebola ndipo tutakapoweza kupambana na maradhi hayo ipasavyo" amesema waziri wa afya Jens Spahn wa chama cha CDU alipokuwa katika ziara ya siku nne mjini Addis Abeba."Watasaidiwa wakaazi wa maeneo husika na kuepusha pia kuenea maradhi hayo "amenukuliwa na gazeti la Süddeutsche Zeitung akisema.

Kipaumbele cha sera za ushirikiano kati ya Ulaya na Afrika

Mada yetu ya mwisho katika ukurasa wa Afrika katika magazeti ya Ujerumani wiki hii inatufikisha njia panda inayoliunganisha bara la Ulaya na lile la Afrika. Lilikuwa gazeti la Zürcher Zeitung lililozungumzia sera za Umoja wa Ulaya kuelekea bara la Afrika. Gazeti linasema kuanzia viongozi wawili wenye usemi mkubwa katika Umoja wa Ulaya Kansela Angela Merkel wa Ujerumani na rais Emmanuel Macron wa Ufaransa kufikia mwenyekiti mpya wa halmashauri kuu ya Umoja wa Ulaya Ursula von der Leyen, wote wameweka wazi kabisa uhusiano wa siku za mbele kuelekea bara la Afrika hautatuwama tena katika ile misingi ya kawaida ya misaada ya maendeleo. Ushirikiano pamoja na serikali za Afrika utajikita zaidi katika masuala ya usalama kama ilivyoshadidiwa na Ujerumani na Ufaransa katika mkutano wa G-7 katika mkakati uliopewa jina "Mkakati wa Sahel.

 

Mwandishi:Hamidou Oummilkheir/ARD Presse Archiv

Mhariri: Jacob Safari