1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Wakimbizi Afrika kukabiliwa na upungufu mkubwa wa chakula-UN

Daniel Gakuba
19 Juni 2022

Wakimbizi walioko Afrika Mashariki na Afrika Magharibi wanakabiliwa na hatari ya kupunguziwa chakula cha msaada kutokana na kuongezeka kwa mahitaji huku fedha zinazotolewa kugharamia mahitaji hayo zikiendelea kupungua.

https://p.dw.com/p/4CubM
Symbolbild Äthiopien Ankunft des Konvois mit Hilfslieferungen in Tigray
(Picha ya maktaba) Wakimbizi nchini Ethiopia wakipokea msaada wa chakulaPicha: Amanuel Sileshi/AFP

Taarifa ya Shirika la Chakula Ulimwenguni, WFP iliyochapishwa Jumapili mjini Roma, Italia, imesema kuwa robo tatu (75%) ya wakimbizi wanaohudumiwa na Umoja wa Mataifa katika ukanda wa mashariki mwa Afrika, wamepunguziwa mgao wa chakula kwa hadi asilimia 50. Kwa mujibu wa shirika hilo, walioathirika zaidi ni wale wanaotafuta hifadhi katika kambi za nchini Ethiopia, Kenya, Sudan Kusini na Uganda.

Soma zaidi: UN: Vita vya Ukraine kusababisha mgogoro wa chakula duniani

''Tumelazimika kuchukua hatua za kuvunja moyo za kupunguza kiwango cha chakula tunacowapatia wakimbizi, ambao msaada wetu ndilo tegemeo lao pekee la kuishi,'' amesema Mkurugenzi Mkuu wa WFP David Beasley.

Mkurugenzi huyo mkuu ameongeza kuwa raslimali zilizopo hazikidhi mahitaji ya msaada wa chakula yanayoongezeka kwa kasi kote duniani.

Ukraine-Krieg | David Beasley, Exekutivdirektor des UN-Welternährungsprogramms
Mkurugenzi Mkuu wa WFP, David BeasleyPicha: Jung Yeon-je/AFP

Afrika Magharibi nako hali si shwari

Upande wa Afrika Magharibi, hususan nchini Burkina Faso, Kameruni, Chad, Mali, Mauritania na Niger, WFP nako imepunguza mgao wa chakula kwa wakimbizi.

Shirika hilo la chakula la Umoja wa Mataifa limeonya juu ya kuvurugika haraka kwa utaratibu wao wa msaada katika mataifa mengine ya Afrika, yakiwemo Angola, Malawi, Msumbiji, Jamhuri ya Kongo, Tanzania na Zimbabwe.

Soma zaidi: Asilimia 40 ya watu wa Tigray wanakabiliwa na ukosefu mkubwa wa chakula 

Jumanne iliyopita, WFP ilitoa rai ya kupatiwa dola milioni 426 ili iweze kuepusha janga la njaa nchini Sudan Kusini, ambako miaka mingi ya ghasia na mafuriko imewafanya watu wengi kuyapa kisogo makaazi yao.

Ilisema katika taifa hilo changa linaloandamwa na mizozo, theluthi mbili (takribani 66%) ya wakaazi wote wanahitaji msaada wa kibinadamu, huku wapata milioni 8.3, wakimbizi miongoni mwao, wakitarajiwa kukabiliwa na uhaba mkubwa wa chakula mwaka huu.

Südsudan l Krise l Hunger - Kinder in Juba
Sudan Kusini ni mojawapo ya nchi ambako wakimbizi wanakabiliwa na hali ngumu ya chakulaPicha: Tony Karumba/AFP via Getty Images

Vita vya Ukraine vyaifanya hali kuwa mbaya zaidi

Mzozo wa vita nchini Ukraine umezidisha makali ya tatizo la wakimbizi duniani pamoja na kitisho cha njaa. Sio tu kwamba vita hivyo vimesababisha wakimbizi wapya zaidi ya milioni sita walioyahama maeneo ya mapigano, bali pia vimechochea ongezeko kubwa la bei ya bidhaa muhimu kama nafaka.

Soma zaidi: WFP yaomba dola milioni 121 kuwasaidia watu wa Cabo Delgado

Jana Jumamosi, Mkuu wa diplomasia katika Umoja wa Ulaya Josep Borrell aliiuhumu Urusi kufanya chaguo la kutumia mauzo ya nafaka kama silaha ya vita, kwa kuzuia usafirishaji wa ngano na mazao mengine kutoka Ukraine kwenda katika nchi maskini.

Kabla ya uvamizi wa Urusi, Ukraine ilikuwa mojawapo ya nchi zinazoongoza kwa kuuza nje mazao ya chakula, ikichangia asilimia 12 ya mauzo ya ngano, asilimia 15 ya biashara ya mahindi, na karibu asilimia 50 ya mafuta ya alizeti yanayouzwa kwenye soko la dunia.

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres amesema vita hivi vya Ukraine vinaweza kuwasukuma makumi ya mamilioni ya watu kwenye ukingo wa njaa.

-AFP