1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Wakenya waanza kupiga kura kumchagua rais mpya

Sylvia Mwehozi | Jacob Safari
9 Agosti 2022

Mamilioni ya Wakenya wameanza kumiminika katika vituo vya kupigia kura mapema leo kumchagua rais mpya, bunge na viongozi wengine.

https://p.dw.com/p/4FIGF
Kenia Wahlen 2022
Picha: Luis Tato/AFP

Kiti cha urais kinawaniwa na wagombea wanne ambao ni mwanasiasa mkongwe Raila Odinga, Makamu Rais William Ruto, George Wajackoyah na David Mwaure. Kura za maoni zimetabiri ushindani mkali kati ya Odinga na Ruto. Jumla ya wapiga kura milioni 22 wamejiandikisha kushiriki uchaguzi wa leo utakaohitimisha utawala wa rais Uhuru Kenyatta.

Kuelekea kura ya leo, tume huru ya uchaguzi na mipaka IEBC ilitangaza kuahirisha uchaguzi wa magavana wa Mombasa na Kakamega, kwa madai ya hitilafu katika karatasi za kupigia kura. Uchaguzi mwingine uliofutwa ni ule wa viti vya ubunge vya Kacheliba na Pokot Kusini. Suala la kupanda kwa gharama za maisha, ufisadi uliokithiri ni miongoni mwa masuala yatakawasukuma wapiga kura. Matokeo rasmi ya uchaguzi huo yatatangazwa ndani ya wiki moja baada ya uchaguzi.

Kenia Der Präsidentschaftskandidat und stellvertretende Präsident William Ruto
Mgombea urais William RutoPicha: John Irungu/Mariel Müller/DW

Rais aliyeko madarakani Uhuru Kenyatta, ambaye kikatiba amezuiwa kuwania muhula wa tatu, amemkosoa hadharani makamu wake na kuonyesha kumuunga mkono Odinga.

Kabila la Kenyatta la Wakikuyu ambalo ndilo lenye idadi kubwa ya watu nchini Kenya, limetoa marais watatu tangu nchi hiyo ilipopata uhuru kutoka kwa Uingereza mwaka 1963. Ila katika uchaguzi wa mwaka huu, kabila hilo halina mgombea. Kutokana na kutambua jinsi kura nchini Kenya zinavyopigwa kwa misingi ya kikabila, wagombea wawili walio mstari wa mbele katika kuwania kiti hicho cha urais, Odinga na Ruto, wote wamechagua makamu wao kutoka kabila la Wakikuyu.

Ruto

Na sasa moja kwa moja katika kuwaangazia wagombea hao, tuanze na William Ruto. Ruto anauongoza muungano wa Kenya Kwanza na alihudumu kama mbunge na waziri wa kilimo kabla kuwa makamu wa rais.

Katika uchaguzi wa mwaka 2007, Ruto alikuwa katika upande mmoja na Odinga na wakapoteza uchaguzi huo na machafuko yaliyofuatia uchaguzi huo, yalisababisha vifo vya zaidi ya watu 1,200.

Kenia Der Präsidentschaftskandidat Raila Odinga
Mgombea urais Raila OdingaPicha: John Irungu/Mariel Müller/DW

Baadae, Ruto alifunguliwa mashtaka katika Mahakama ya Kimataifa ya Uhalifu ICC kwa dhima yake katika machafuko hayo, ila kesi hiyo haikufika mbali huku Ruto akikanusha kuhusika kwa njia yoyote ile.

Mwaka 2013 na 2017, Ruto aliungana na Kenyatta na wakamshinda Odinga mara mbili.

Ruto ambaye ni mzungumzaji mzuri, ameahidi kuongeza matumizi kwa wakulima wadogo wadogo na biashara za kibinafsi, na kufanyia mabadiliko bima ya kitaifa ya afya na fedha za wastaafu.

Mbele ya Wakenya, Ruto anasema yeye ni muuzaji kuku wa zamani ambaye anawawakilisha watu wa kawaida na anapambana na wanasiasa wanaotoka katika koo za kitajiri.

Odinga

Raila Odinga naye anagombea urais kupitia Muungano wa Azimio la Umoja ambao unajumuisha chama cha Jubilee chake Uhuru Kenyatta. Odinga ni mwana wa makamu wa kwanza wa rais wa Kenya, Jaramogi Oginga Odinga naye Kenyatta ni mwana wa rais wa kwanza wa taifa hilo Jommo Kenyatta.

Kenia Wahlen 2022
George Wajackoyah wa kulia anayewania uraisPicha: Yasuyoshi Chiba/AFP

Odinga ambaye ni mfungwa wa zamani wa kisiasa anasema, alishinda chaguzi tatu zilizopita nchini humo ila matokeo yalichakachuliwa. Machafuko yalishuhudiwa baada ya kura za mwaka 2007 na 2017.

Odinga ameahidi kupambana na ufisadi uliokithiri, kutoa malipo ya kila mwezi kwa Wakenya wasio na ajira, bima ya afya kwa wote na elimu ya bila malipo kwa kila mmoja kutoka shule ya msingi hadi chuo kikuu. Alimpa jina  mwanawe wa kwanza jina Fidel kama kiongozi wa zamani wa Cuba Fidel Castro, kutokana na siasa zake za kuegemea mrengo wa kushoto

Ngome yake iko magharibi na eneo la Nyanza nchini Kenya, maeneo ambayo wakaazi katika miaka iliyopita wamelalamikia kutengwa na serikali kutokana na kuunga mkono upinzani.

Wajackoyah

Kenia Wahlen 2022
David Mwaure katikati anayewania uraisPicha: John Ochieng/SOPA Images/ZUMAPRESS.com/picture alliance

George Wajackoyah mwenye umri wa miaka 63 ambaye anajitambulisha kama wakili, msomi na jasusi wa zamani, anagombea urais wa Kenya kwa tiketi ya chama cha Roots.

Ameahidi kuhalalisha kilimo cha bangi kwa ajili ya matumizi ya kimatibabu na katika viwanda. Ameahidi pia kuziuza korodani za fisi na sumu ya nyoka kwa mataifa ya nje ili kuyalipa madeni ya Kenya.

Wajackoyah vile vile iwapo atachaguliwa, anapanga kusimamisha utekelezwaji wa katiba ya Kenya kwa kipindi cha miezi sita na kumnyonga yeyote atakayekuwa amepatikana na hatia ya ufisadi.

Wajackoyah amewavutia wapiga kura wengi vijana na kuwaghadhabisha viongozi wengi wa dini.

Waihiga

David Mwaure  Waihiga ambaye ni wakili pia anagombea urais kupitia chama cha Agano. Yeye ameahidi kukabiliana na ufisadi serikalini na pia kuchapisha kandarasi za serikali kwa miradi mikuu ya miundo msingi kama reli, bandari na barabara kuu.