Wajumbe wakwama kwenye mazungumzo ya Brexit | Matukio ya Kisiasa | DW | 16.10.2019
  1. Inhalt
  2. Navigation
  3. Weitere Inhalte
  4. Metanavigation
  5. Suche
  6. Choose from 30 Languages
Matangazo

Mazungumzo ya Brexit hayajafikia mwafaka

Wajumbe wakwama kwenye mazungumzo ya Brexit

Bado hakuna suluhisho lililofikiwa katika kutafutia ufumbuzi vipengee muhimu vinavyosababisha mkwamo katika mazungumzo ya Brexit kati ya Umoja wa Ulaya na Uingereza wakati viongozi wakuu wakijiandaa kukutana,

Mazungumzo kuhusu Uingereza kujiondoa kwenye Umoja wa Ulaya yanaendelea mpaka wakati huu lakini tayari inazungumzwa kwamba hakuna makubaliano yaliyofikiwa kuhusu masuala yanayosababisha kizingiti.

Mazungumzo yanayofanyika tangu Jumanne  na kwenda mpaka usiku wa manane na kuendelea mpaka leo Jumatano  yana nia ya kutafuta makubaliano ya kisheria kuhusu mpango mpya wa Uingereza juu ya hiyo Talaka wanayoiomba,kabla ya mkutano wa kilele uliopangiwa kufanyika kesho alhamisi na ijumaa.

Mkutano wa alhamisi na ijumaa utawakutanisha viongozi wakuu wa Umoja wa Ulaya mjini Brussels.Waziri mkuu wa Ireland Leo Varadkar akizungumzia kinachoendelea Brussels baada ya kuulizwa swali bungeni amesema  njia ya kuelekea kupatikana makubaliano ipo lakini kuna mambo mengi ambayo bado yanahitaji kupatiwa ufumbuzi.

''Mazungumzo hayatomalizika wiki hii au hata hata mwezi huu kwa kufikiwa makubaliano.Kitakachofanyika ni kufikishwa mwisho tu kwa awamu ya kwanza ya Brexit. Na kitakachotokea pindi makubaliano yakifikiwa wiki hii au mwezi huu,ni kwamba tutaanza kujadili juu ya mustakabali wa uhusiano wetu wa kiuchumi ,kiusalama,na makubaliano ya biashara huru.Makubaliano ambayo tutayajenga baina ya  Uingereza na Umoja wa Ulaya.''

Waziri mkuu huyo wa Ireland anasema,mazungumzo ya dakika za mwisho kati ya Umoja wa Ulaya na Uingereza mpaka sasa yameshindwa kuyatatua masuala yanayoleta mvutano na kuuzuia mchakato wa Brexit. Kizingiti kikubwa kiko kwenye suala zima la biashara na mpaka wa Ireland ingawa mkuu wa mazungumzo ya Brexit wa Umoja wa Ulaya   Michel Barnier amenukuliwa akisema anaimani makubaliano yatafikiwa. ''Mazungumzo yamekuwa na tija lakini bado kuna masuala kadhaa muhimu ya kutatuliwa amesema Barnier''

Rais wa baraza la Ulaya Donald Tusk amewaambia waandishi habari leo kwamba ndani ya masaa saba au nane kila kitu kinabidi kiwe kimeshajulikana juu ya mwelekeo uliofikiwa. Kiongozi wa mazungumzo ya Brexit upande wa Uingereza David Frost alionekana akiondoka makao makuu ya Tume halmashauri ya Umoja wa Ulaya leo baada ya mazungumzo: Kimsingi ikiwa leo yatapatikana makubaliano kesho na keshokutwa makubaliano hayo yataangaliwa na viongozi wa Umoja wa Ulaya na huenda Umoja huo ukaitisha mkutano wa dharura wa kilele mwishoni mwa Oktoba wa ama kuyaidhinisha makubaliano hayo,kuirefushia muda zaidi Uingereza au kufanya maandalizi ya mwisho ya kutengana kwa njia ya mparaganyiko. 

Mwandishi:Saumu Mwasimba

Mhariri: Sekione Kitojo

 

Matangazo

Unaweza kusikiliza matangazo yetu hapa

Kusikiliza matangazo ya Idhaa ya Kiswahili ya DW, tafadhali bonyeza alama ya spika ya masikioni hapo chini, na kuwasiliana nasi, tafadhali tuandikie moja kwa moja kupitia: kiswahili@dw.com