Wajerumani wazidi kuihama nchi yao | Matukio ya Kisiasa | DW | 17.12.2007
 1. Inhalt
 2. Navigation
 3. Weitere Inhalte
 4. Metanavigation
 5. Suche
 6. Choose from 30 Languages

Matukio ya Kisiasa

Wajerumani wazidi kuihama nchi yao

Ajira kiini cha kuhama

Tangu kumalizika kwa vita kuu ya pili ya dunia watu wengi duniani wamekuwa na uhuru wa kwenda kuishi na kufanya kazi katika nchi mbalimbali.

Kwa mujibu wa takwimu za Ujerumani, inaonesha kwamba raia wengi wa nchi hiyo wamekuwa wakiondoka kwenda kutafuta maslahi mazuri zaidi katika nchi zingine ambako wanafikiri kwamba watafanikiwa mara dufu kwa kupata mishahara minono au biashara nzuri.

Mfano mzuri umeonekana kwa Wajerumani wenye taaluma za kidaktari, biashara na uhandisi wakati vijana wanandoto za kupata shahada mbalimbali kutoka nchini Marekeni.

Idadi kubwa ya wajerumani wanakimbilia kufanya kazi katika nchi za Switzerland , Uhispania , Ireland , na katika nchi za Scandinavia ambazo ni Sweden , Denmark na Norway . Idadi kubwa ya wahamiaji wa Kijerumani imejitokeza baada ya vita kuu ya pili ya dunia iliyokwisha mwaka 1945.

Zaidi ya maslahi mazuri ni kitu gani kingine kinachowafanya Wajerumani wengi waachane na nchi yao na kwenda kutafuta maisha nchi za nje? Juergen Horn ni kijana mjasiriamali aliyeamua kuwekeza katika nyanja ya mawasiliano ya mtandano wa internet nchini Ireland, kwa vile halipi ushuru mkubwa na hakuna ukiritimba kama Ujerumani.

Kutokana na maelezo ya mfanyabiashara huyo wa Kijerumani, ni dhahiri kwamba nchi yake ya kuzaliwa haina mzaha na masuala ya kodi. Nchini Ujerumani unaweza kupata kiasi kikubwa cha pesa, lakini pia makato ya kodi huwa makubwa na kukufanya ubaki na pesa kidogo tu.

Mtafiti mwingine wa taasisi ya uchumi ya Ujerumani aitwaye Juergen Schupp, anasema tatizo la ajira pia limewalazimu wazawa wengi wa nchi hiyo kwenda ughaibuni kutafuta kazi kama anavyofafanua. Kutokana na hilo, Ujerumani itakosa wataalamu muhimu kwa vile hivi sasa vijana wanakimbia uhaba wa kazi.

Kristina Hermanns ni binti wa Kijerumani anayefanya kazi nchini India . Anasema maisha ya India na Ulaya siyo tofauti sana katika matumizi ya pesa, lakini kampuni yake inamlipia kodi ya nyumba, usafiri, umeme na bima ya afya. Hivyo mshahara anaoupata hauna matumizi makubwa kama ambavyo angeutumia akiwa Ujerumani.

Wachambuzi wa masuala ya kijamii na uchumi nchini Ujerumani wameshabashiri kuwa miaka ijayo nchi hiyo itakuwa na uhaba wa wataalamu kutokana na ukweli kuwa vijana wengi wanapenda kufanya kazi nje ya nchi kama anavyoeleza mtafiti Juergen Schupp wa taasisi ya uchumi ya Ujerumani.

Utafiti unaonesha kwamba asilimia mbili ya wakazi zaidi ya milioni 82 wa Ujerumani, wana mipango ya kwenda kutafuta kazi au kufanya biashara nje nchi.

 • Tarehe 17.12.2007
 • Mwandishi Tuma Dandi
 • Chapisha Chapisha ukurasa huu
 • Kiungo https://p.dw.com/p/CciO
 • Tarehe 17.12.2007
 • Mwandishi Tuma Dandi
 • Chapisha Chapisha ukurasa huu
 • Kiungo https://p.dw.com/p/CciO

Unaweza kusikiliza matangazo yetu hapa

Kusikiliza matangazo ya Idhaa ya Kiswahili ya DW, tafadhali bonyeza alama ya spika ya masikioni hapo chini, na kuwasiliana nasi, tafadhali tuandikie moja kwa moja kupitia: kiswahili@dw.com