1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Waislamu washerehekea sikukuu ya Eid al-Adha

21 Agosti 2018

Waislamu katika maeneo mbalimbali duniani wanasherehekea siku kuu ya Eid al-Adha licha ya tofauti zilizopo miongoni mwa viongozi wa dini ya Kiislamu ambapo baadhi wameamuru sikukuu ya Eid kuwa Jumatano.

https://p.dw.com/p/33U0j
Haddsch Islamische Pilgerfahrt nach Mekka | Kabaa, Große Moschee
Picha: Getty Images/AFP/K. Sahib

Sheikh mkuu wa Saudi arabia  hussein bin Abdelaziz al-Sheikh aliwataka Waislamu kuwa pamoja  na kutahadharisha kuwa hijja si mahala pa makundi na  kauli za kisiasa. Matamshi yake yalionekana kuwalenga mahujaji kutoka Iran yenye malumbano na Marekani.

Mjini Tehran Kiongozi mkuu wa kidini wa Iran Ayatollah Khamenei alitoa wito wa Umoja miongoni mwa waislamu, wakati wa salamu zake za eid hii leo, zilizosomwa kwenye televisheni ya taifa .

Gavana wa Makka Mwana wa Ufalme Khalid al-feisal alisema kiasi ya mahujaji 86,000 wa Iran wametekeleza hijja mwaka huu na 300 kutoka Qatar, ambayo imo katika mzozo wa kidiplomasia na saudia kuhusiana na kile kilichoelezwa kuwa ni uungaji mkono wa Qatar wa makundi ya kigaidi, madai ambayo Qatar imeyapinga.

Hijja  safari hii imetekelezwa kwa usalama, huku maafisa wakisema wamechukua hatua zote za tahadhari.  Mkusanyiko huu mkiubwa wa waislamu duniani, ulishuhudia  ajali za mkanyagano mnamo miaka ya nyuma na katika baadhi ya  maafisa wamekabiliwa na hali ngumu kuidhibiti hali ya mambo.

Baadhi ya waislamu kusali Eid Jumatano

Katika kile kinachoashiria kuwepo kwa tofauti kuhusu siku hasa ya Eid baadhi ya waislamu katika nchi kadhaa watasali eid hapo kesho, . Sala ya eid leo itafuatiwa na kuchinja mnyama ambapo nyama baadae hutolewa kwa jamii marafiki na wasiojiweza.

Kulingana na sheria za Kiislamu, Mwenyezi Mungu alimweka katika jaribio Nabii Ibrahim ili kutambua utiifu wake kwake kwa kumuagiza kumtoa sadaka mwanawe wa kiume na wa kipekee, Ismael. Utiifu wa Ibrahim na mwanawe ulizawadiwa na Mungu kwa kumwacha hai Ismael na badala yake kumteremshia kondoo, kisha kumjaalia mtoto mwingine kwa jina Ishaaq.

Nchini Saudi Arabia mahujaji milioni mbili waliofika eneo hilo vile vile wanasherehekea siku kuu hii, huku wengi wakionekana wakitembea katika eneo la Mina wakirusha mawe katika minara mitatu, kuashiria jinsi Nabii Ibrahim alipompiga shetani alipojaribu kumkataza kutomchinja mwanawe alivyoagizwa na Mwenyezi Mungu.

Kwa kukamilisha hajj mtu huwa ametimiza nguzo ya tano ya Uislamu ambapo kila muislamu mwenye uwezo hutakiwa kuitimiza alau mara moja maishani mwake. Mmoja wa mahujaji Ashraf Abdelrahman mwenye umri wa miaka 46  alisema atarejea nyumbani Sudan akiwa kama aliyezaliwa upya.

Mwandishi: Sophia Chinyezi

Mhariri: Mohammed Abdulrahman