Waingereza wanapiga kura leo. | Matukio ya Kisiasa | DW | 06.05.2010
  1. Inhalt
  2. Navigation
  3. Weitere Inhalte
  4. Metanavigation
  5. Suche
  6. Choose from 30 Languages

Matukio ya Kisiasa

Waingereza wanapiga kura leo.

Matokeo ya kura za maoni yaonyesha David Cameron wa chama cha Kihafidhina, anaongoza.

Msururu wa matokeo ya kura ya maoni yaliyochapishwa na magazeti sita ya Uingereza yanakiweka chama cha upinzani cha kihafidhina, Conservative cha David Cameron kwenye uongozi.

Wahariri wa magazeti hayo hata hivyo walikubaliana na pendekezo kwamba Cameron hatafaulu kupata ushindi unaohitajika kuwa waziri mkuu na itambidi ashirikiane na chama cha Liberal Democrats cha Nick Clegg.

Takwimu za kura ya maoni zinaonyesha kwamba chama cha kihafidhina kitashinda kati ya asilimia 35 na 37 ya kura na chama cha Leba kimekadiriwa kupata kati ya asilimia 27 na 29 na kile cha Liberal Democrats kimepigiwa upatu kupata kati ya asilimia 26 na 28 ya jumla ya kura.

Karte Großbritannien Englisch

United Kingdom, London --- DW-Grafik: Peter Steinmetz

Matokeo hayo yanaashiria kwamba bunge halitakuwa na chama ambacho kitaweza kuunda serikali na hivyo uwepo wa uwezekano wa kuunda seriklali ya muungano. Hali kama hiyo ilijitokeza katika uchaguzi wa 1974 chini ya waziri mkuu mconservative Edward Heath. Chama cha Kiliberali kinachoongozwa na Nick Clegg kinapaniwa kuwa na uzito mkubwa wa kuzingatiwa katika kuundwa kwa serikali na hivyo kukipa umuhimu bungeni.

Hata hivyo katika mchakato huo wa uchaguzi matokeo ya kura ya maoni hayatoi sura kamili ya jinsi hali itakavyokuwa hasa kuhusiana na jinsi viti 649 vitakavyoaniwa nchini Uingereza.

Mapema wiki hii, chama cha Leba cha waziri mkuu wa sasa Gordon Brown kilikuwa katika nafasi ya tatu na hivyo kuzua hofu ya kudidimia kwa chama hicho ambacho kimetawala nchini Uingereza tangu mwaka wa 1997.

Maoni kabla ya uchauzi kuanza yalionyesha kwamba kati ya wapiga kura milioni 45 nchini Uingereza, takriban theluthi moja hawakuwa wameamua watakichagua chama kipi. Ilitangazwa leo kwamba viti vitakavyoaniwa vimepungua hadi 649 baada ya mgombea ubunge wa jimbo moja kufariki.

Baada ya kampeni kali ya mwezi mmoja, ikiwemo mijadala kwenye Televisheni, inatarajiwa kwamba wapiga kura wengi watajitokeza na hata kufikia asilimia 70 ya wapiga kura waliojiandikisha, utabiri ambao haukushuhudiwa hata katika uchaguzi wa mwaka 1997 ambapo waziri mkuu wa zamani Tony Blair aliibuka mshindi.

Wachunguzi wa kisiasa wanadai kwamba uchaguzi huu ni kinyang’anyiro ambacho kitabadilisha mazingira ya kisiasa katika historia ya Uingereza. Ikiwa chama cha Leba cha Gordon Brown kitashinda, basi kitakuwa kimejipa sifa isiyo ya kawaida ya kurejea madarakani katika mazingira ya upinzani mkubwa..

Ushindi wa chama cha kihafidhina; Conservative cha David Cameron utakua ni afuweni baada ya miaka 13.

Mtazamo unaosisitizwa ni kwamba kutaundwa serikali ya muungano na angalau kutakipa chama cha Liberal Democrats nafasi ya kusikika . Kuna msisimko mkubwa wa kisiasa nchini Uingereza na gazeti la Daily Mirror leo lina picha ya mgombeaji David Cameron na maandishi ’waziri mkuu’ na lile la The Sun limeweka picha yake katika mfano wa mabango yaliyotumiwa katika uchaguzi wa rais Obama wa Marekani yakiwa na kauli mbiu ya matumaini.

Mwandishi, Peter Moss /DPA/AP

Mhariri, Abdul-Rahman Mohammed

Unaweza kusikiliza matangazo yetu hapa

Kusikiliza matangazo ya Idhaa ya Kiswahili ya DW, tafadhali bonyeza alama ya spika ya masikioni hapo chini, na kuwasiliana nasi, tafadhali tuandikie moja kwa moja kupitia: kiswahili@dw.com