Wahouthi washambulia viwanja vya ndege vya Saudi Arabia | Matukio ya Kisiasa | DW | 15.02.2021
  1. Inhalt
  2. Navigation
  3. Weitere Inhalte
  4. Metanavigation
  5. Suche
  6. Choose from 30 Languages
Matangazo

YEMEN

Wahouthi washambulia viwanja vya ndege vya Saudi Arabia

Wapiganaji wa Kihouthi nchini Yemen wamevishambulia viwanja viwili vya ndege vya Saudi Arabia kwa kutumia ndege zisizo rubani, huku Saudi Arabia ikisema imezitungua ndege hizo kabla ya kusababisha madhara.

Kwa mujibu wa Wahouthi kupitia mtandao wa Twitter, mashambulizi hayo ya leo (Jumatatu, Februari 15) yalifanikiwa kusimamisha operesheni za kijeshi zilizokuwa zifanyike kutokea viwanja hivyo vya ndege kwa zaidi ya masaa mawili.

Viwanja vya ndege vya Jeddah na Abha ndivyo vinavyotajwa kwenye mashambulizi hayo ya ndege zisizo rubani.

Hata hivyo, muungano wa kijeshi unaoongozwa na Saudi Arabia umesema ulizidunguwa ndege hizo za Wahouthi licha ya tukio hilo kutothibitishwa na mamlaka nchini Saudia. 

Kwa mujibu wa msemaji wa Wahouthi, Yahya Sarea, wapiganaji wao wamekuwa wakifanya mashambulizi takribani kila siku kwa siku tisa mfululizo dhidi ya uwanja wa ndege za kijeshi kusini mwa Saudia.

Jumatano ya wiki iliyopita, mamlaka za Saudia zilisema mashambulizi yalisababisha moto kwenye ndege moja ya abiria katika uwanja wa ndege wa Abha. 

Mapigano makali katikati ya Yemen

Arabischer Frühling in Jemen - 10 Jahre seit der Revolution

Wapiganaji wa Kihouthi nchini Yemen.

Mapigano makali kati ya pande hizo mbili yanaendelea kwenye jimbo la Marib, yakiripotiwa kupoteza maisha ya watu 12 hivi leo na yakiwa yameshauwa zaidi ya wengine 40 tangu yaanze wiki iliyopita. Wahouthi wanawania kuchukuwa udhibiti wa jimbo hilo lenye rasilimali nyingi ya mafuta na gesi, na pia ambalo limekuwa likionesha upinzani mkali dhidi yao kwa kipindi kirefu.

Ofisi ya habari ya Wahouthi imesema kuwa muungano wa kijeshi unaoongozwa na Saudi Arabia umeshambulia zaidi ya mara kumi kwenye jimbo hilo, na mashambulizi mengine mawili kwenye jimbo jirani la Jaw, ambalo lilitumiwa na waasi hao kuanzisha mashambulizi dhidi ya Marib. 

Jimbo hilo ambalo ndilo pia lenye bwawa la kale lenye jina hilo, limekuwa kimbilio kubwa kwa raia wa Yemen waliokimbia mashambulizi ya Wahouthi tangu vita kuanza, na mapigano haya ya sasa yanahatarisha usalama wa wakimbizi hao wa ndani.

Infografik Streitkräfte Jemen EN

Rangi buluu isiyokoza ndiyo maeneo yanayodhibitiwa na Wahouthi, maeneo ya kijivujivu yanadhibitiwa na serikali na buluu iliyokoza yanadhibitiwa na al-Qaida.

Umoja wa Mataifa wataka kuyanusuru mazungumzo ya amani

Umoja wa Mataifa unajaribu kuyafufuwa mazungumzo ya amani na kukomesha vita hivyo, ambavyo unasema vimesababisha janga kubwa kabisa la kibinaadamu duniani. Lakini mapigano haya sasa yanaelekea kuwa kikwazo kikubwa cha kurejewa kwa mazungumzo hayo. 

Wiki mbili zilizopita, utawala wa Rais Joe Biden wa Marekani ulitangaza dhamira yake ya kuliondowa kundi la Wahouthi kwenye orodha ya makundi ya kigaidi, kama sehemu ya kampeni yake ya kukomesha vita hivyo, ambavyo viliungwa mkono na utawala wa Rais Barack Obama, wakati huo Biden akiwa makamu wake.

Muungano huo wa kijeshi ulijiingiza nchini Yemen mwaka 2015 kuinga mkono serikali ya Abdu Mansoor Hadi, kuyadhibiti maeneo ya mjii mkuu na mengine yenye watu wengi yaliyokuwa yakishikiliwa na Wahouthi.