1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
ImaniIndia

Mamilioni ya Wahindu waanza tamasha kubwa zaidi India

Angela Mdungu
13 Januari 2025

Umati mkubwa wa mahujaji wa Kihindu umekusanyika nchini India na kuoga katika maji wanayoamini kuwa matakatifu Jumatatu katika wa ufunguzi wa tamasha la ibada linalofahamika kama Kumbh Mela.

https://p.dw.com/p/4p68r
India- Kumbh Mela
Tamasha la Kihindu la Maha Kumbh Mela Januari 13, 2025Picha: NIHARIKA KULKARNI/AFP

Waandaaji wa  tamasha hilo wanatarajia watu milioni 400 watashiriki kwenye kusanyiko hilo kubwa zaidi kuwahi kutokea. Tamasha la kidini la Wahindu linalohusisha ibada ya kuoga linafanyika katika eneo inapokutana mito mitatu, Ganges, Yamuna na Saraswati. Waziri Mkuu wa India Narendra Modi ameliita kusanyiko hilo kuwa  "tukio takatifu" linalounganisha pamoja watu wengi katika imani, ibada na utamaduni. Naye Waziri kiongozi wa jimbo la Uttar Pradesh Yogi Adityanath, amewakaribisha mahujaji kwenye tamasha alililota kuwa kubwa zaidi la kiroho na kiutamaduni.

Mmoja wa mahujaji wanaoshiriki kwenye tamasha hilo Bharti Jha amelizungumzia akisema kuwa, "Tamasha la Maha Kumbh linafanyika kila baada ya miaka 12 na huibua maadili ya imani na kuabudu ndani yetu. Watu wanasema kuwa kuoga katika mto Ganges kunasafisha dhambi zetu zote."

Wakati wa kuanza kwa tamasha hilo, watawa wa Kihindu wameonekana wakiwa wamebeba bendera kubwa za madhehebu yao wakati matrekta yakikokota sanamu za miungu ya kihindu na kusindikizwa na tembo. Mahujaji waliojitokeza kwa wingi wamesikika wakipiga ngoma pamoja na honi kama sehemu ya ibada yao.

Waratibu wa tamasha hilo wanasema  wingi wa watu wanaoshiriki ni sawa na idadi jumla ya raia wote wa Canada na Marekani.

Ulinzi umeimarishwa kwenye eneo la tamasha

Polisi nchini humo wamesema wanaendelea kulinda doria usiku na mchana ili kuhakikisha usalama wa hali ya juu katika tukio hilo.

Eneo la Prayagraj kando ya mito wanakoshiriki Wahindu katika tamasha hilo la kiibada limeonekana likiwa limefurika mahema yakiwemo ya hadhi ya juu. Licha ya hali ya hewa kuwa nyuzi joto 15 mahujaji wamesema hawakuhisi baridi wakati wakifanya ibada ya kuoga.

India, tamasha la Maha Kumbh 2025
Mmoja wa waumini wa Kihindu katika tamasha la Maha Kumbh MelaPicha: NIHARIKA KULKARNI/AFP

Takriban vyoo 150,0000 vimeandaliwa ili kuhudumia umati huo mkubwa wa  watu wakati kukiwa na mtandao wa majiko ya ya kijamii yanayoweza kuwahudumia takriban watu 50,00 kwa wakati mmoja. Kulingana na serikali ya India, tamasha lililopita la Kumbh Mela lililofanyika mwaka 2019 lilihudhuriwa na watu milioni 240.

Chimbuko la tamasha hilo ni utamaduni wa Kihindu kuhusu mapambano kati ya miungu na mashetani ili kupata udhibiti wa sanamu ambayo wahindu wanaamini inawapa watu uwezo wa kuishi milele. Tamasha la Kumbh Mela pia ni fursa muhimu kwa serikali ya Kihindu ya India kujisafisha.