Wahariri wana maoni yao | Magazetini | DW | 02.06.2008
 1. Inhalt
 2. Navigation
 3. Weitere Inhalte
 4. Metanavigation
 5. Suche
 6. Choose from 30 Languages
Matangazo

Magazetini

Wahariri wana maoni yao

Obama ndie atakaekua mgombea wa Democrats wanaashiria wahariri

Rais wa sasa G.W. Bush na Barack Obama ambae huenda akawa mgombea wa kwanza chotara katika historia ya Marekani

Rais wa sasa G.W. Bush na Barack Obama ambae huenda akawa mgombea wa kwanza chotara katika historia ya MarekaniMkutano mkuu wa chama cha kiliberali cha FDP mjini München,kongamano kuhusu mustakbal wa chama cha Social Democratic mjini Nürnberg na kinyang'anyiro cha chama cha Democratic cha kuania tikiti ya kugombea kiti cha rais wa Marekani,uchaguzi utakapoitishwa mwezi November ujao ni miongoni mwa mada zilizotangulizwa mbele na wahariri wa magazeti ya Ujerumani hii leo.


Tuanzie na mkutano mkuu wa chama cha FDP mjini München.Gazeti la DIE WELT linamulika zaidi mjadala kuhusu sera za kodi za chama hicho na kuandika:


"Suala la kimsingi limegeuka kua chanzo cha kuania madaraka.Hadi dakika hii mapendekezo yote ya maana kuhusu kodi za mapato yalikua yakitolewa na chama cha FDP.Hali hiyo lakini imebadilika tangu CSU walipojitia kati katika mashindano ya nani atashauri mfumo mkali zaidi wa kodi,mfumo unaostahiki na ambao si wakutatanisha.Hatimae FDP kimeamua kufuata mkondo wa mshikamano katika suala hilo la kodi.Pendekezo la mtaalam mashuhuri wa masuala ya fedha Hermann Otto Solms limewavutia wengi zaidi kuliko lile la mshindani wake,mkuu wa chama cha FDP -katika jimbo la North Rhine Westfalia Andreas Pinkwart.Kiroja ni kwamba Pinkwart hajaondolewa patupu.Lengo lake ni kuchaguliwa kua kiongozi wa chama kwa daraja ya taifa.Kiti hicho kinakaliwa na Guido Westerwelle.Akishindwa Westerwelle kukiongoza chama cha kiliberali hadi katika serikali ya muungano,basi Pinkwart atakua na nafasi nzuri ya kuridhi kiti cha mkuu wa chama hicho cha kiliberali nchini."


Hayo ni maoni ya gazeti la DIE WELT.Kuhusu kongamano lililojadili hali ya siku za mbele ya chama cha Social Democrat mjini Nürnberg,gazeti la NEUE OSNABRÜCKER ZEITUNG linaandika:


"Mapambazuko hayawi hivi.Ingawa mwenyekiti wa chama cha Social Democratic SPD Kurt Beck amefanikiwa kuzuwia pasitokee uasi chamani,hata hivyo ameshindwa kuchora njia itakayokikwamua chama chao.Wafuasi wa chama cha SPD hawapendezewi na jinsi uongozi wa chama chao unavyoendeshwa.Hata kama malumbano yanasifiwa kua ni ya maana chamani, hata hivyo yanaweza kuleta hasara yakiangaliwa na walio nje kua na matokeo yasiyokadirika."


Kinyang'anyiro cha kuania tikiti ya chama cha Democratic kwa uchaguzi ujao wa rais nchini Marekani ni mada iliyohanikiza pia magazetini hii leo.Gazeti la SÜDDEUTSCHE ZEITUNG linaandika:


"Barack Obama atachaguliwa hivi karibuni kua mgombea wa chama cha Democratic.Hata wafuasi wakakamavu wa HiIlary na vichwa mchungu wengineo wanautambua ukweli huo tangu halmashauri ya suluhu ilipokutana.Matokeo yanayobishwa ya uchaguzi wa Florida na Michigan yatazingatiwa lakini nusu bin nusu.Hillary Clinton atajipatia vikura lakini havitamsaidia pakubwa.Ndo kusema Hilary clinton atakua makamo mgombea?Haiwezekani na Obama asingependelea pia.Suala muhimu zaidi watu wanalojiuliza ni kwa jinsi gani Hillary Clinton anafikiria kuchangia mnamo wiki na miezi ijayo kuhakikisha umoja ndani ya chama cha Democratic?"


Hayo ni maoni ya SÜDDEUTSCHE ZEITUNG ambayo kimsingi yanalingana na yale ya PFORZHEIMER ZEITUNG,linaloandika:


"Barack Obama ameshashinda.Kila mmoja anatambua kwamba yeye ndie atakaeshindana na mgombea wa chama cha Republican John McCAIN kampeni ya uchaguzi itakapoanza.Clinton anaonyesha kua na shida ya kuutambua ukweli wa hali ya mambo.Hali hiyo inaweza kukigharimu ushindi chama cha Democrat.Kwasababu Obama, naang'are vipi,anahitaji hata hivyo uungaji mkono timamu wa chama chake.►◄
 • Tarehe 02.06.2008
 • Mwandishi Hamidou, Oumilkher
 • Chapisha Chapisha ukurasa huu
 • Kiungo https://p.dw.com/p/EBCj
 • Tarehe 02.06.2008
 • Mwandishi Hamidou, Oumilkher
 • Chapisha Chapisha ukurasa huu
 • Kiungo https://p.dw.com/p/EBCj