Wahariri wamshambulia Günther Grass | Magazetini | DW | 05.04.2012
  1. Inhalt
  2. Navigation
  3. Weitere Inhalte
  4. Metanavigation
  5. Suche
  6. Choose from 30 Languages
Matangazo

Magazetini

Wahariri wamshambulia Günther Grass

Wahariri wa magazeti karibu yote ya Ujerumani wanalizungumzia shairi la Mwandishi mashuhuri wa Ujerumani Günther Grass mshindi wa nishani ya Nobel katika fasihi

Mwandishi mashuhuri wa Ujerumani Günther Grass

Mwandishi mashuhuri wa Ujerumani Günther Grass.

Grass amesema katika shairi lake kwamba Israel yenye silaha za nyuklia inahatarisha amani ya dunia. Pia ameonya dhidi ya kuazisha vita dhidi ya Iran.Kauli za Mwandishi huyo juu ya Israel zimetifua tufani nchini Ujerumani.

Mhariri wa gazeti la "Sächsiche" anasema ni haki ya kila mwandishi kutoa maoni yake,hata kufikia kiwango cha kuivunja miiko.Lakini aliyoyasema Günther Grass ni kauli kombo. Mhariri wa gazeti hilo anaeleza kuwa Günther Grass ameteleza. Anaiwasilisha Israel kama mvamizi,ingawa ni Iran ambayo wakati wote imekuwa inatishia kuiangamiza Israel. Grass anazipuuza kauli za Rais wa Iran Mahmoud Ahmadinejad juu ya kukana kutokea maangamizi ya wayahudi.Gazeti hilo linasema Grass pia anadai kwamba ni Israel inayopanga kuwaangamiza watu wa Iran. Ama kuhusu hoja za ukweli Mwandishi huyo anatembea kichwa chini miguu juu!

Günther Grass ameliita shairi lake ,kinacholazimu kusema". Mhariri wa gazeti la"Hannoversche Allgemeine"anakubaliana na Mwandishi huyo lakini anasema ukweli uliopo ni kwamba sera za Israel zinakosolewa nchini Ujerumani mara kwa mara, magazetini na katika medani nyingine. Vyombo vya habari vya Ujerumani pia vinazungumzia ukweli kwamba Israel inajishamirisha kijeshi dhidi ya Iran. Lakini jambo la kushangaza ni kwamba Günther Grass hakusema lolote juu ya masuala ya msingi kuhusiana na mgogoro baina ya Israel na Wapalestina.

Gazeti la"Hannoversche Allgemeine" linasema anachokitaka Mwandishi huyo ni kusimama katika mimbari ya wanaovunja miiko. Lakini huenda akasimama katika mimbari yenye nguzo zinazosambaratika Gazeti la "Braunschweiger"linasema sera za Israel,bila shaka zinakosolewa nchini Ujerumani. Lakini fedheha iliyomo katika aliyoyasema Günther Grass ni kwamba anajifanya kuwa shahidi wa harakati za amani duniani. Lakini anafanya hivyo,kana kwamba anavunja mwiko,kutokana na yeye mwenyewe kuwa sehemu ya taifa lililofanya maangamizi ya Wayahudi. Mtu hawezi kuwa mtawa lakini wakati huo huo akahitaji kuungamana.

Gazeti la "SüdKurier" linasema hakuna kitu kibaya kama kushangiliwa na watu waliosimama katika upande potovu. Günther Grass analijua hilo vizuri. Mhariri wa gazeti hilo anaeleza, kuwa lawama za Günther Grass hazitapokewa vizuri nchini Israel ikiwa hakusema lolote juu ya vitisho vinavyotolewa na viongozi wa Iran juu ya kuiangamiza Israel.

Lakini gazeti la"Leipziger Volkszeitung" linasema mtu anaweza kutoa madai mengi juu ya Günther Grass,kwa mfano alinyamaa kimya kwa muda mrefu juu ya historia yake ya miaka ya nyuma, kwamba alibeba silaha kwa niaba ya mafashisti. Lakini jee kweli mtu anaweza kusema kwamba Günther Grass anawachukia wayahudi? Jibu ni hapana!. Na hata hao wanaohusika wanashindwa kuthibitisha.

Mwandishi:Mtullya abdu/Deutsche Zeitungen

Mhariri: Yusuf Saumu