1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Wahariri wa magazeti wazungumzia juu ya biashara ya vifaru vya kijeshi baina ya Ujerumani na Saudi Arabia.

Abdu Said Mtullya5 Julai 2011

Saudi Arabia yakusudia kununua vifaru kutoka Ujerumani.

https://p.dw.com/p/11p9H
Serikali ya mseto ya Ujerumani ya Kansela Merkel yadaiwa kuiuzia vifaru Saudi Arabia.(Kushoto ni waziri wake Westerwelle)Picha: dapd

Wahariri wa magazeti ya Ujerumani leo wanatoa maoni yao juu ya biashara ya vifaru vya kijeshi kati ya Ujerumani na Saudi Arabia na juu ya matokeo ya uchaguzi wa nchini Thailand.

Mhariri wa gazeti la Märkische Allgemeine anasema biashara ya vifaru baina ya Ujerumani na Saudi Arabia ni kashfa . Mhariri wa gazeti hilo anasema ikiwa vifaru hivyo kweli vitapelekwa Saudi Arabia ,serikali ya mseto ya Kansela Merkel itakiuka misingi ya biashara ya nje; kwa mfano Ujerumani haipaswi kupeleka silaha katika maeneo yenye mizozo au kwa tawala zinazowanyanyasa wananchi wao ,aidha Ujerumani haipaswi kupeleka silaha zitakazohatarisha usalama wa Israel.

Na mhariri wa gazeti la Südkurier anasema wakati sasa umefika kwa Ujerumani kufuatilia kwa matendo, kauli za kulaani hatua za tawala fulani katika nchi za kiarabu. Mhariri huyo anaeleza kuwa watawala wa Saudi Arabia wanazo sababu za kutaka kuimarisha ulinzi kwa kuagiza vifaru kutoka Ujerumani.

Harakati za mapinduzi zinaendelea katika nchi za kiarabu,tawala za kidhalimu zinayumba. Mhariri huyo pia anaeleza kwamba Saudi Arabia yenyewe inashiriki katika kuzizima harakati za wapinzani katika nchi jirani ya Bahrain. Serikali ya Ujerumani imezilaani hatua za kijeshi zilizochukuliwa na Saudi Arabia katika Bahrain. Na sasa umefika wakati kwa Ujerumani kuchukua hatua baada ya kutoa kauli.

Gazeti la Frankurter Rundschau pia linatoa maoni yake juu ya mpango wa kuiuzia Saudi Arabia vifaru. Lakini maoni hayo yanamlenga Waziri wa mambo ya nje wa Ujerumani Guido Westerwelle. Gazeti hilo liasema Waziri huyo huyo alielipinga azimio la Umoja wa Mataifa juu ya kuwalinda raia nchini Libya, ati kwa sababu nguvu za kijeshi zinatumika sasa ananyamaza kimya juu ya mpango wa Ujerumani wa kuiuzia virafu Saudi Arabia. Siasa hiyo siyo ya uadilifu.

Mhariri wa gazeti la Westfälische anazungumzia juu ya uchaguzi wa Thailand kufuatia uchaguzi mkuu wa jumapili iliyopita. Anasema anatumai jeshi la nchi hiyo, kama lilivyoahidi, litayaheshimu matokeo ya uchaguzi huo ambapo chama cha upinzani kilishinda . Anaeleza kuwa aghalabu wanajeshi wa Thailand ni wepesi wa kutafuta sababu za kjiiingiza katika siasa, kama ilivyotokea miaka mitano iliyopita, pale walipoona kwamba siasa za nchi zilienda kinyume na maslahi yao. Kwa sasa wanajeshi hao wanaweza kuutumia mzozo wa mpaka na Kambodia kama sababu ya kujiingiza katika siasa.

Mwandishi/Mtullya Abdu/Deutsche Zeitungen/

Mhariri/Abdul-Rahman