Wahariri juu ya Putin | Magazetini | DW | 08.05.2012
  1. Inhalt
  2. Navigation
  3. Weitere Inhalte
  4. Metanavigation
  5. Suche
  6. Choose from 30 Languages
Matangazo

Magazetini

Wahariri juu ya Putin

Wahariri wa magazeti wanazungumzia juu ya Wladimir Putin kurudi tena katika kiti cha Urais nchini Urusi. Na pia juu ya mgogoro wa kisiasa nchini Ugiriki.

Wladimir Putin ni Rais wa Urusi kwa mara nyingine

Wladimir Putin ni Rais wa Urusi kwa mara nyingine.

Juu ya Rais Putin gazeti la "Delmenhorster Kreisblatt" linasema kwamba kwa wadau wa kimataifa, mkanganyiko juu ya Putin na Medvedev umepata jawabu. Mwenye kushika hatamu nchini Urusi sasa anajulikana. Kaizari Wladimir amerejea madarakani.

Mhariri wa gazeti la "Rhein Zeitung" anasema dunia sasa isitarajie kuona mageuzi nchini Urusi, kutokana na kurejea Putin katika Urais wa nchi hiyo. Mhariri wa gazeti hilo anaeleza kwamba hali ya mtamauko itaongezeka nchini Urusi katika miaka inayokuja. Sababu ni kwamba tofauti na Urusi ya zamani, Urusi ya leo ni jamii iliyo wazi.

Tabaka la kati linayajua mazingira ya jamii za maghaibi vizuri sana. Na watu wa tabaka hilo ndiyo hasa wanaozidi kutamauka, kwa sababu tathmini yao juu ya hali halisi ya maisha inatofautiana na jinsi wanavyoongozwa na serikali. Tofauti hiyo itazidi kuwa kubwa, kwa sababu hakuna matumaini ya kufanyika mageuzi chini ya utawala wa Rais Putin.

Gazeti la "Straubinger Tageblatt" linasema pamoja na kuapishwa kuwa Rais wa Urusi kwa mara nyingine, Putin anatambua kwamba mambo yamebadilika nchini. Gazeti hilo linahoji kuwa Putin anajua kwamba yeye siyo tena mtawala wa warusi wote. Maandamano yaliyofanyika kupinga ushindi wake katika uchaguzi yamempa ujumbe huo. Nguvu ya vyombo vya serikali siyo kubwa kiasi cha kuweza kuibadili mihemko ya watu. Sasa panahitajika muda wa nukta tu kuibyofa kompyuta, kwa uwongo na hadaa kujulikana nchi nzima. Putin sasa amesimama mbele ya Urusi ambayo ni taofuti na jinsi ilivyokuwa miaka minne iliyopita, alipoikabidhi kwa kibaraka wake ,Medvedev.

Ugiriki imegeuka kuwa jino bovu, usiku wa manane, katika kinywa cha Ulaya.Ulaya haipati usingizi. Ugiriki sasa inakabiliwa na migogoro ya kisiasa na kiuchumi. Mhariri wa gazeti la "Darmstädter Echo" anasema matokeo ya uchaguzi uliofanyika jumapili iliyopita yameonyesha ghadhabu za wagiriki. Lakini mhariri huyo anawanasihi wagiriki kwa kusema hasira ni hasara.

Matamanio ya wagiriki sasa ni kuondokana na jinamizi lililowainamia- yaani mgogoro wa madeni. Lakini njia waliyoitumia katika uchaguzi haitalipunga jinamizi hilo! Ni kinyume chake. Mustakabal wa Ugiriki sasa umezidi kuwa wa mashaka. Sasa chochote kinaweza kutokea, kwanza kufilisika, na baadae kuondoka katika Umoja wa sarafu ya Euro. Lakini hatua hiyo itakuwa na madhara kwa wote barani Ulaya.

Mwandishi:Mtullya Abdu/Deutsche Zeitungen

Mhariri:Othman, Miraji