1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Wahanga wa unyanyasaji kingono wawasili mjini Roma

Sylvia Mwehozi
20 Februari 2019

Wahanga wa unyanyasaji kingono katika Kanisa Katoliki duniani wanatarajia kukutana na maaskofu na kamati ya maandalizi ya mkutano wa kilele utakaonza Alhamis juu ya kashfa ya unyanyasaji kingono.

https://p.dw.com/p/3DiBv
Nonnen in der katholischen Kirche
Picha: Imago/UIG

Kwa mujibu wa mwanaharakati wa Italia, Papa Francis alikuwa akutane na wahanga hao siku ya Jumatano kabla ya kuanza mkutano wa kilele. Mwanaharakati Francesco Zanardi wa shirika la Italia la Rete I'Abuso ambalo ni sehemu ya kampeni ya kundi la kukomesha unyanyasaji kingono dhidi ya watoto, alisema wamepokea ujumbe wa kukutana na Papa Francis siku ya Jumatano, lakini Vatican haukuthibitisha uwepo wake.

Siku ya Jumanne maafisa wa Vatican walisema wahanga wa unyanyasaji watakuwa na fursa ya kukutana na kamati ya maandalizi ya mkutano wa kilele ambayo inajumuisha makadinali wawili lakini sio Papa mwenyewe. Vatican ilikuwa imesema kwamba mkutano wa Papa na wahanga si sehemu ya ajenda.

Matthias Katsch ambaye ni mwanachama wa Ujerumani wa kampeni hiyo alisema wawakilishi karibu 40 wa asasi zinazowakilisha wahanga wamekwenda mjini Roma ili kupaza sauti zao na kuikosoa Vatican kupendekeza kukutana na baadhi yao. Doris Wagner ni mtawa wa zamani ambaye ni mhanga wa unyanyasaji na anasema, "wakati nilipobakwa mwaka 2008 na padre, nilidhani nilikuwa mtawa pekee ambaye nilifanyiwa kitendo hicho, na nilikaa nikiwaza hilo kwa miaka mingi hadi pale nilipofanikiwa kusoma taarifa za tangu mwaka 2001. Na katika taarifa hizo mlikuwa na kesi mbaya za unyanyasaji kingono dhidi ya watawa ikiwemo ubakaji, kulazimishwa kutoa mimba, maambukizi ya HIV na hata kifo".

VAE Papst Franziskus in Abu Dhabi
Papa Francis katika ziara ya hivi karibuni huko rasi ya UarabuniPicha: Reuters/A. Jadallah

Makasisi wa Kikatoliki kutoka duniani kote waliomba radhi siku ya Jumanne kwa kushindwa kushughulika pale mapadri wa kanisa hilo walipowabaka watoto na kukiri kwamba jumuiya yake ilipofushwa na unyanyasaji huo na kusababisha kukosekana kwa uaminifu, kukataliwa na kufunika madhambi.

Mashirika mawili yanayowakilisha umoja wa makasisi duniani yalitoa tamko la pamoja kuelekea mkutano wa kilele wa Papa Francis na maaskofu. Katika taarifa yake, wameapa kutekeleza zaidi hatua za uwajibikaji kuhakikisha kwamba hakuna tena kuficha uozo unaofanywa na wakuu wa kidini na kwamba watoto daima wanatakiwa kuwa salama wakiwa mikononi mwa wachungaji.

Makasisi wa kidini wamejikuta chini ya kashfa ya miongo kadhaa, tangu maaskofu wa dayosisi walipoanza kumulikwa kwa kuwalinda na kuwakingia kifua mapadri wao, walifanya hivyo kwa kuwahamisha kutoka parokia moja kwenda nyingine ambako waliendeleza unyanyasaji kingono dhidi ya watoto.

Umoja wa wakuu wa kidini unawakilisha uongozi wa makasisi wa kiume ambao una karibu mapadri 133,000 duniani kote. Tawi lake la kike linawakilisha watawa wa kike ambao ni takribani 500,000 duniani kote. Katika taarifa yake makundi hayo yamesema yanaona aibu namna yalivyoshindwa ndani ya mazingira wanayohudumia. Mkutano wa kilele wa kukomesha unyanyasaji kingono utaanza siku ya Alhamis na kumalizika Jumapili.

Mwandishi: Sylvia Mwehozi

Mhariri: Sekione Kitojo