1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Wahamiaji 31 wagunduliwa kwenye lori Ufaransa

Lilian Mtono
3 Novemba 2019

Polisi nchini Ufaransa imegundua uwepo wa wahamiaji 31 waliokuwa nyuma ya lori ikiwa ni pamoja na watoto ambao hawakuwa na mzazi ama mlezi.

https://p.dw.com/p/3SOED
Symbolbild Frankreich Zollkontrolle
Picha: picture-alliance/dpa/D. Crasnault

Kulingana na mwendesha mashtaka wa umma mjini Nice nchini Ufaransa, kwenye tukio la jana Jumamosi maafisa hao wa polisi waligundua uwepo wa wahamiaji hao wakati wakifanya ukaguzi wa kawaida wa barabarani.

Miongoni mwa wahamiaji hao ni watoto wasio na wazazi wala walezi, na waligunduliwa wakati wa ukaguzi huo kwenye mji wa La Tubier ulioko karibu na mpaka wa Italia.

Mwendesha mashitaka huyo amesema wahamiaji wote 31 waliokuwa kwenye lori ni raia wa Pakistan. Dereva wa lori ambaye pia ni raia wa Pakistan alikamatwa na mamlaka za Ufaransa.

Wahamiaji hao pia hatimaye walikabidhiwa kwa mamlaka za Italia, hii ikiwa ni kulingana na gazeti la Ufaransa la Nice-Martin.

Waendesha mashitaka, pamoja na mambo mengine watafanya uchunguzi kuangazia iwapo matukio kama haya yanahusiana na biashara haramu ya binadamu. Na iwapo watagundua kwamba hakuna mahusiano, dereva wa lori hilo atashitakiwa kwa kuwasaidia watu hao kuingia kinyume cha sheria za uhamiaji, hii ikiwa ni kulingana na shirika la habari la AFP.

UK 39 Leichen in LKW Container in Essex
Maafisa udhibiti wa mipakani wanahofia kutokea tukio jingine kama la Uingereza ambao walikuta miili ya wahamiaji kwenye lori.Picha: Reuters/H. McKay

Wasiwasi baada ya vifo vya wahamiaji waliokuwa kwenye lori, Uingereza.

Kugunduliwa kwa wahamiaji hao kunakuja siku kadhaa baada ya mamlaka za Ufaransa, kwenye mji wa bandari wa Calais kulisimamisha lori lililokuwa na jokofu ambalo lilikuwa limebeba wahamiaji wanane.

Wahamiaji hao wote, ambao walikuwa ni pamoja na watoto walikimbizwa hospitalini baada ya kuonyesha dalili za tatizo la joto la mwili kushuka isivyo kawaida ama kitaalamu hypothermia.

Mashirika ya udhibiti wa mipakani yamekuwa katika tahadhari kubwa kufuatia vifo vya wahamiaji 39 nchini Uingereza Oktoba 23 ambapo wahamiaji waliohisiwa kuwa raia wa Vietnam walikuwa wakisafirishwa kwenye lori lililokuwa na jokofu. Lori hilo liligunduliwa mashariki mwa London.

Mtu aliyedaiwa kuwa dereva wa lori hilo, kijana mwenye umri wa miaka 25 kutoka Ireland Kaskazini tayari ameshitakiwa kwa makosa ya mauaji. Anakabiliwa na mashitaka 39 ya kuua kwa kukusudia, usafirishaji haramu wa binadamu pamoja na makosa ya uhamiaji.