1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Wahamiaji 137,000 wafanikiwa kuingia Ulaya 2015

1 Julai 2015

Umoja wa Mataifa umesema kiasi ya watu 137,000 walisafiri kupitia bahari ya Mediterrania na kuweza kuingia barani Ulaya katika kipindi cha miezi sita iliyopita wengi wao wakitoroka vita, mizozo na mateso.

https://p.dw.com/p/1Fr0d
Picha: picture alliance/epa/Italian Navy

Ripoti iliyotolewa leo na shirika la umoja wa Mataifa linaloshughulikia maslahi ya wakimbizi UNHCR imesema bara Ulaya linashuhudia mzozo wa ongezeko la wahamiaji katika viwango ambavyo ni vya kihistoria baada ya idadi ya watu wanaojaribu kuingia barani humo kupitia baharini kuongezeka kwa asilimia 86 katika kipindi cha miezi sita iliyopita ikilinganishwa na mwaka jana.

Idadi hiyo inatarajiwa kuongezeka hata zaidi msimu huu wa joto barani Ulaya kwani wafanyabiashara wa kuwasafirisha wahamiaji kwa njia haramu huchukua fursa hiyo ya kuwepo hali nzuri ya hewa kuwasafirisha watu zaidi kupitia bahari hatari ya Meditarrania.

Uhamiaji waiumisha kichwa Ulaya

Mzozo huo wa ongezeko la wahamiaji limekuwa suala la msumari moto kwa nchi za Umoja wa Ulaya ambazo zimekuwa zikivutana kuhusu namna bora ya kukabiliana na wafanyabiashara wanaowasafirisha wahamiaji kwa njia haramu na kuhusu jinsi ya kugawana mzigo wa wahamiaji wanaofanikiwa kuingia Ulaya.

Mkuu wa UNHCR Antonio Guterres
Mkuu wa UNHCR Antonio GuterresPicha: picture-alliance/dpa/S. Di Nolfi

Wengi wa wahamiaji hao huwasili kwanza Italia na Ugiriki kabla ya kusonga mbele na kuingia katika nchi nyingine za kaskazini mwa Ulaya wakiwa na matumaini ya kupata ajira suala ambalo halijapokelewa vyema katika baadhi ya nchi hizo ambazo zenyewe zinakabiliwa na tatizo la ukosefu wa ajira kwa raia wao.

Umoja wa Mataifa umesifu hatua ya Umoja wa Ulaya ya kuwakubali wahamiaji 40,000 kutoka Syria na Eritrea na kuwasmabaza katika nchi wanachama lakini umetaka kuwepo ushirikiano zaidi miongoni mwa nchi za umoja huo kuwasaidia wahamiaji hao na nchi zilizo na mzigo wa kukidhi mahitaji yao.

Mkuu wa UNHCR Antonio Guterres amesisitiza wengi wanaojaribu kuingia barani Ulaya hawaji kutafuta ajira bali ni wakimbizi wanaotafuta usalama kwa kukimbia vita na mateso nchini mwao.

Thuluthi moja ya waliowasili Italia na Ugiriki mwaka huu wanatokea Syria huku asilimia 12 ya wahamiaji hao wakitokea Afghanistan na Eritrea. Nchi nyingine ambazo wahamiaji wengi wanatokea ni Somalia, Nigeria, Iraq na Sudan.

Wahamiaji zaidi wafa mwaka huu

UNHCR imesema mwaka huu pia umeshuhudia ongezeko la idadi ya watu wanaokufa majini wakijaribu kuvuka bahari ya Mediterrania. Kiasi ya watu 1,867 wamefariki dunia 1,308 kati yao wakiripotiwa kufariki katika mwezi wa Aprili pekee.

Wahamiaji wakijaribu kuvuka bahari ya Meditarrania
Wahamiaji wakijaribu kuvuka bahari ya MeditarraniaPicha: picture alliance/dpa/Italian Navy

Guterres amesema kuwepo kwa sera bora kuhusu suala la wahamiaji na mfumo muafaka wa operesheni za uokozi itawezakana kuokoa maisha ya wengi baharini.

Wahamiaji pia wamebadilisha mkondo wanaofuata baharini kuingia Ulaya. Hivi sasa wanapitia Uturuki kuingia Ugiriki badala ya kupitia kaskazini mwa Afrika na kuingia Italia.

Umoja wa Mataifa umegundua kuwa wengi wao licha ya kufikia Ugiriki na Italia wanalenga hatimaye kutafuta hifadhi katika nchi kama Sweden na Ujerumani zinazosemekana kutoa msaada bora kwa wahamiaji.

Mwandishi:Caro Robi/afp

Mhariri: Hamidou Oummilkheir