Wageni na uchaguzi wa Ujerumani | IDHAA YA KISWAHILI | DW | 10.09.2013
  1. Inhalt
  2. Navigation
  3. Weitere Inhalte
  4. Metanavigation
  5. Suche
  6. Choose from 30 Languages
Matangazo

IDHAA YA KISWAHILI

Wageni na uchaguzi wa Ujerumani

Raia milioni tano wa Kijerumani wenye asili ya kigeni wamejisajili kupiga kura kwenye uchaguzi mkuu, lakini suala la ikiwa watapiga kura na watampigia nani kura zao lina uhusiano mkubwa wa wasifu wa wapiga kura hao.

Juan Diaz amehamia Berlin na moja kwa moja kuupenda mji huo kutokana na kuwa na raia wa nchi mbali mbali ambao wamekusanyika na kuwa mfano wa zulia lililofumwa kwa rangi tafauti.

Diaz ni Mmarekani, wazazi make ni Wacuba walioukimbia utawala wa Fidel Castro na kwenda kuishi uhamishoni Miami. Kwa ujumla anauelezea utambulisho wake kuwa ni mgumu. Ziada ya hayo Diaz amekuwa raia wa Ujerumani kwa mwaka wa saba sasa.

"Niliomba uraia ili kuweza kuwa na haki ya kusema pia nilitaka kuwa na haki ya kuchangia maoni na kuwa na usemi katika kuchaguwa nani awe kansela na nani aingie bungeni." Anasema Diaz.

Wageni milioni 16

Ingrid Tucci, mtafiti wa masuala ya kijamii.

Ingrid Tucci, mtafiti wa masuala ya kijamii.

Kwa mujibu wa Idara ya Takwimu ya Serikali ya Shirikisho la Jamhuri ya Ujerumani, mwaka 2011 kulikuwa na takriban wananchi milioni 16 kama Juan Diaz wanaoishi Ujerumani, wakiwa ni watu wenye asili ya wahamiaji walioziacha nchi ambazo walizaliwa wao au wazazi wao au mababu zao, lakini wengi wao aidha ni wadogo sana kuweza kuwa na haki ya kupiga kura au hawana uraia wa Ujerumani.

Ni mtu mwenye uraia wa Ujerumani tu ndiye anayeweza kuwa na haki ya kupiga kura. Na katika kesi maalum, raia wa Umoja wa Ulaya huruhusiwa kupiga kura katika uchaguzi wa serikali za mitaa na uchaguzi wa bunge la Ulaya lakini sio uchaguzi mkuu wa Ujerumani.

Taarifa za Idara ya Takwimu za serikali zinasema theluthi moja ya watu weye asili ya wahamiaji wataruhusiwa kupiga kura katika uchaguzi mkuu wa Ujerumani wa mwaka huu. Idadi yao imekuwa ikiongezeka, kwani mwaka 2011 pekee zaidi ya watu 100,000 walipewa uraia.

Upendeleo wa vyama hutegemea nchi wanakotoka

Mjumbe wa CDU, Cemile Giousouf.

Mjumbe wa CDU, Cemile Giousouf.

Hata hivyo, sio wananchi wote wenye asili ya wahamiaji huteremka vituoni wakati wa uchaguzi. Kutokana na Idara ya Utafiti ya Serikali ya Ujerumani ya mwaka 2012 kuhusu wahamiaji na wakimbizi watu wenye asili ya kigeni mara chache wanashiriki katika uchaguzi ambapo asilimia 72.3 miongoni mwao walishiriki katika uchaguzi wa Ujerumani mwaka 2009 wakati wananchi wa Ujerumani walioshiriki uchaguzi huo walikuwa asilimia 81.5.

Katika makundi hayo yote mawili asilimia 80 ya waliotumia haki yao ya kupiga kura walikuwa ni watu walioajiriwa. Wananchi waliotumia haki yao ya kupiga kura ambao hawana historia ya wahamiaji idadi yao ilikuwa asilima 81.5 .

Juan Diaz hakubaliani na wazo la kutopiga kura. Kwa Mjerumani huyo mwenye asili ya Marekani na Cuba jambo hilo haliwazii kabisa. "Mimi siku zote naona kuwa ni jambo zuri sana wakati ninapopokea kadi yangu ya haki ya kupiga kura ".

Haki ya kupiga kura ni haki ya msingi isiothaminika ambayo yeye hawezi kuachana nayo.Akiwa kama msuluhishi baina ya vyama hasimu mara nyingi huwa safarini katika nchi za Balkan na hupiga kura yake na mapema kwa njia ya posta.

Uchunguzi wa maoni kuhusu uchaguzi unasema kwamba kama vile anavyopiga kura yake Diaz,watu huvipigia kura chama cha CDU au SPD.

Wahamiaji mara nyingi hupendelea kuvipigia kura vyama hivyo viwili vikuu anasema Ingrid Tucci wa Taasisi ya Utafiti wa Kiuchumi ya Ujerumani.

Mtaalamu huyo wa uchumi jamii amefanya utafiti juu ya uaminifu kwa vyama kwa watu wenye asili ya wahamiaji. Kwa hiyo watu waliokuja nchini katika miaka ya 1950 na 1960 kama wafanyakazi wa kigeni kutoka Ulaya ya Kusini, Yugoslavia na Uturuki hupendelea chama cha SPD kwa sababu wanaweza kuwekwa katika kundi la "tabaka la jadi la wafanyakazi".

Walowezi wenye asili ya Kijerumani ambao wamerudi nchini kutoka iliokuwa Muungano wa Kisovieti baada ya kumalizika kwa Vita Baridi hupendelea zaidi vyama vya CDU na CSU.

Tajiriba ya wahamijaji ni muhimu

Mmoja wa Wajerumani wenye asili ya kigeni akipiga kura katika uchaguzi mkuu wa 2009.

Mmoja wa Wajerumani wenye asili ya kigeni akipiga kura katika uchaguzi mkuu wa 2009.

Tucci anaamini kwamba suala la uaminifu kwa vyama linahusiana sana na tajiriba ya wahamiaji. Chama cha CDU kimewapigania sana wahamiaji waliokuwa na asili ya Kijerumani ili waweze kuhamia nchini Ujerumani na kusaidia sana hatua za kuwaingiza upya katika jamii.

Tucci anasema kwa upande mwengine dini haina dhima kubwa katika suala la uchaguzi.Utafiti wake umeonyesha kuwa dini,kiwango cha elimu na hadhi ya kikazi vina ushawishi mdogo katika suala la upendeleo wa vyama.

Anafikiria kuna uhusiano wa moja kwa moja kati ya mienendo ya kupiga kura na tajiriba ya wahamiaji ambapo kwa vyovyote vile unaweza kuboreshwa zaidi. Kwa sababu upendeleo wa wazi kwa vyama vya CDU na SPD unatafautiana kwa kutegemea vizazi:

Kwa mujibu wa data za mwaka 2011 asilimia 18 ya kizazi kipya yaani watoto wa wahamiaji waliozaliwa nchini wanapendelea chama cha Kijani na kila mara kama asilimia 40 hupendelea CDU au SPD. Kwa hiyo hawatafautiani sana na watu ambao hawana asili ya wahamiaji anafafanuwa Tucci.

Diaz atampigia kura nani hapo mwezi wa Septemba ni kitu kilicho wazi.Huko nyuma aliwahi kumfanyia kazi mwanasiasa wa CDU,alishiriki mikutano mingi ya chama cha Kijani na alishiriki mara nyingi midahalo ya kisiasa ya vyama vyote mjini Berlin.

Huko nyuma anasema kwamba Wajerumani katika duru za mikutano mara nyingi wamekuwa wakimwambia kuwa "wewe ni mgeni huna haki hiyo ya kuchangia "Jambo hilo limekuwa likimkasirisha lakini hivi sasa ana haki kamili ya kutowa mchango wake wa maoni.

Mwandishi: Naomi Conrad/ Mohamed Dahman
Mhariri: Mohammed Khelef

Matangazo

Sikiliza Matangazo Yetu

Unaweza kusikiliza matangazo yetu hapa

Kusikiliza matangazo ya Idhaa ya Kiswahili ya DW, tafadhali bonyeza alama ya spika ya masikioni hapo chini, na kuwasiliana nasi, tafadhali tuandikie moja kwa moja kupitia: kiswahili@dw.com