1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
JamiiMali

Mali: Wafanyakazi wa Msalaba Mwekundu waachiwa huru

Grace Kabogo
20 Machi 2023

Kamati ya Kimataifa ya Msalaba Mwekundu, ICRC imesema wafanyakazi wake wawili waliotekwa nyara mapema mwezi huu kaskazini mwa Mali, wameachiwa huru.

https://p.dw.com/p/4Ow3p
Symbolbild Roter Halbmond
Picha: Fischer/Bildagentur-online/picture alliance

Taarifa ya ICRC iliyochapishwa jana jioni katika ukurasa wake wa Twitter, imeeleza kuwa wafanyakazi hao wako salama na wameachiwa bila masharti. Wafanyakazi wawili wa ICRC walitekwa nyara Machi 4, katika miji ya Gao na Kidal, kaskazini mwa Mali.

Nchi hiyo inakabiliwa na ukosefu wa usalama na mzozo wa kisiasa tangu mwaka 2012, wakati wapiganaji wa jihadi na makundi yanayotaka kujitenga yalipozuka kaskazini mwa nchi.

Soma pia: Makundi ya kigaidi nchini Mali yashambulia kambi ya jeshi

Daktari wa Shirika la Afya Duniani, WHO, alitekwa nyara nchini Mali mwishoni mwa mwezi Januari, na aliachiwa huru mwezi Februari.

Mwezi Mei, Waitaliano watatu na raia mmoja wa Togo walitekwa nyara kusini mwa Mali. Maelfu ya raia, polisi na wanajeshi wameuawa Mali na zaidi ya watu milioni mbili wameyakimbia makaazi yao.