1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Wafanyakazi kote duniani waadhimisha Siku ya Mei Mosi

Grace Kabogo
1 Mei 2023

Idadi kubwa ya wafanyakazi na wanaharakati ulimwenguni kote wanaadhimisha Siku ya Wafanyakazi Duniani kwa maandamano na kutoa wito wa nyongeza za mishahara, kupunguzwa kwa saa za kufanya kazi na mazingira bora ya kazi.

https://p.dw.com/p/4QkRe
Türkei | 1. Mai-Demo in Istanbul
Picha: AP/Khalil Hamra

Siku ya Wafanyakazi huadhimishwa kila Mei Mosi na nchi nyingi duniani kuangazia mafanikio na haki za wafanyakazi kwa kufanya maandamano, mikutano na matukio mengine, huku kaulimbiu ya mwaka huu wa 2023 ikiwa ni ''Haki za Wafanyakazi na Haki ya Kijamii na Kiuchumi.''

Watu wengi wamejitokeza katika maadhimisho ya mwaka huu, kuliko ilivyokuwa katika miaka iliyopita kutokana na kulegezwa au kuondolewa kabisa vizuizi vya kukabiliana na janga la UVIKO-19, huku upinzani ukiangazia jinsi mipango ya kiuchumi ya serikali itaweza kuwaathiri wafanyakazi.

Wafanyakazi Ufaransa wapinga hatua za Rais Macron

Nchini Ufaransa, vyama vya wafanyakazi vinapanga kufanya maandamano makubwa kupinga hatua ya hivi karibuni ya Rais Emmanuel Macron kuongeza umri wa kustaafu kutoka miaka 62 hadi 64.

Huko Korea Kusini, maelfu ya watu wamehudhuria matukio mbalimbali ikiwa ni mikusanyiko yake mikubwa kabisa ya Mei Mosi tangu kuzuka kwa janga la virusi vya corona mwanzoni mwa mwaka 2020. Kwa mujibu wa waandaaji, mikutano miwili mikuu katika mji mkuu, Seoul, watu takriban 30,000 walitarajiwa kujitokeza katika kila mkutano.

Mjini Tokyo, Japan, maelfu ya wanachama wa vyama vya wafanyakazi, wabunge wa upinzani na wasomi walikusanyika katika uwanja wa Yoyogi, wakidai nyogeza ya mishahara ili kukabiliana na gharama zinazoongezeka, kwani maisha yao bado hayajakaa sawa kutokana na athari za UVIKO-19.

Asien | 1. Mai in Südkorea
Wafanyakazi wa Korea Kusini wakiandamana mjini SeoulPicha: Lee Jin-man/AP

Nchini Indonesia waandamanaji wanaitaka serikali kuibatilisha sheria ya uundaji wa ajira, ambayo wamesema itawanufaisha wafanyabiashara, na kutozingatia haki na mazingira bora ya wafanyakazi.

Matukio ya kuadhimisha Siku ya Wafanyakazi nchini Ujerumani yalianza kwa maandamano yaliyopewa jina ''Take Back the Night,'' yaliyoandaliwa na watetezi wa haki za wanawake na makundi ya utambulisho wa kijinsia katika mkesha wa Mei Mosi kupinga ghasia na unyanyasaji unaoelekezwa kwa wanawake na watu wanaoshiriki mapenzi ya jinsia moja.

Maelfu ya watu walishiriki katika maandamano hayo, ambayo yalikuwa ya amani, licha ya kuwepo makabiliano kati ya washiriki na polisi. Maandamano mengine kadhaa yaliyoandaliwa na vyama vya wafanyakazi na makundi ya itikadi za mrengo wa kushoto yamepangwa kufanyika leo Ujerumani.

Sera za kazi zaangaziwa

Nchini Taiwan maelfu ya wafanyakazi wameingia mitaani kupinga kile walichokiita kukosekana kwa sera za kutosha za kazi, na hivyo kuweka shinikizo kwa chama tawala kabla ya uchaguzi wa urais uliopangwa kufanyika 2024.

Nako Korea Kaskazini, gazeti kuu la nchi hiyo la Rodong Sinmun limechapisha tahariri ndefu ikiwataka wafanyakazi kumuunga mkono kiongozi wake Kim Jong Un, kutekeleza viwango vya majukumu yao ya uzalishaji ambavyo vimewekwa na kuimarisha maisha ya umma.

Aidha, wafanyakazi katika nchi mbalimbali za barani Afrika wameandamana pia kuadhimisha Siku ya Wafanyakazi Duniani.

(AP)