1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Wafanyakazi 10 wa shirika la kutoa misaada wauawa Afghanistan

Kabogo Grace Patricia8 Agosti 2010

Mmoja kati ya wafanyakazi hao ni raia wa Ujerumani.

https://p.dw.com/p/Oeov
Mtu mmoja akitoka nje ya jengo la ofisi za International Assistance Mission mjini Kabul, Afghanistan.Picha: AP

Serikali ya Ujerumani imethibitisha kuwa mwanamke wa Kijerumani ni miongoni mwa watu 10 wasio kuwa na silaha ambao waliuawa na kundi la Taliban nchini Afghanistan mapema jana. Msemaji wa serikali, amesema Ujerumani imelaani vikali mauaji hayo na inataka uchunguzi wa kina ufanyike ili wahusika waweze kufikishwa mahakamani.

Kundi la madaktari wanaofanya kazi katika shirika la misaada la Kikristo linalojulikana kama International Assistance Mission, lilishambuliwa kaskazini-mashariki mwa Afghanistan. Miongoni mwa wale waliouawa pia ni Wamarekani sita, Muingereza mmoja na Waafghani wawili waliokuwa wakifanya kazi na shirika hilo la misaada.

Raia wengine wawili wa Afghanistan walinusurika katika shambulio hilo. Kundi la Taliban limedai kuwaua wanaume saba na wanawake watatu, kwa sababu walikuwa wamisionari wa Kikristo, ingawa inasemekana pia kuwa wizi huenda ikawa sababu ya mauaji hayo.