1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Tanzania yaondoa marufuku ya kusafirisha nje wanyama pori

Saumu Mwasimba
4 Juni 2022

Marufuku hiyo imeondolewa kwa muda wa miezi sita ambapo wafanyabiashara watakuwa huru kusafirisha nje wanyama pori kuanzia Juni 6 hadi Desemba 5

https://p.dw.com/p/4CHiZ
Giraffen
Picha: WANG Yu and GUO Xiaocong

Tanzania imeondowa kwa muda marufuku ya usafirishaji wanyama pori iliyokuwa imewekwa miaka sita iliyopita kwa lengo la kuwalinda wanyama pamoja na ndege katika nchi hiyo ya Afrika Mashariki.

Uamuazi wa kuondolewa marufuku hiyo kwa kipindi cha miezi sita kumewaibua watetezi wa mazingira na wanyama pori kutowa mwito kuwepo michakato ya ufuatiliaji kuwalinda wanyama dhidi ya ujangili ambao umepunguwa kwa kiasi.

Mamlaka ya wanyama pori nchini Tanzania ijumaa ilitowa taarifa ikisema serikali imekuwa ikitathmini biashara ya usafirishaji wanyama pori hai tangu ilipowekwa marufuku hiyo na hivi sasa imeamua kuondowa marufuku hiyo.

BG Ukraine Haustiere und Krieg
Picha: Jamie Wiseman/ dmg media Licensing/picture alliance

Taarifa hiyo imebaini  kwamba wafanyabiashara watakuwa na kipindi cha miezi sita kuanzia Juni 6 hadi Desemba 5 kumaliza kuuza wanyama waliokuwa wamebakisha walioshindwa kuwauza wakati marufuku hiyo ilipokuwa ikitekelezwa.

Tanzania iliweka marufuku ya kusafirisha wanyama pori mnamo mwaka 2016 chini ya utawala uliopita uliokuwa ukiongozwa na hayati rais John Pombe Magufuli ambaye namna yake ya uongozi ilimfanya apachikwe jina la ''Bulldozer''.

Wakati huo serikali ilihalalisha marufuku hiyo kwasababu ya dosari zilizokuweko kwenye biashara,ikiwemo usafirishaji nje wa wanyama wanaolindwa.

     

Rais wa sasa wa Tanzania,Samia Suluhu Hassan  ameamua kujitenga na baadhi ya sera zilizokuwa zikifuatwa na mtangulizi wake,tangu alipoingia madarakani mwaka jana kufuatia kifo cha ghafla cha Magufuli. 

WWF: Uamuzi huo usifute mafanikio yaliofikiwa

Shirika la kutetea mazingira na wanyama pori la WWF limetahadharisha kwamba kuondolewa kwa marufuku hiyo hakupaswi kuyaondowa mafanikio yaliyopatikana katika kuwalinda wanyama pori,na kuchochea kurudi  hatua kama ujangili  ambao umeonekana kupungua.

Amani Ngasuru ambaye ni mkurugenzi wa WWF nchini Tanzania ameliambia shirika la habari la AFP kwamba mifumo ya uhakika ya ufuatiliaji inahitajika pamoja na data kuenda sambamba na maamuzi kama yaliyofanyika.

Eco Africa I Namibia Giraffes
Picha: DW

Tanzania inafahamika kwa fukwe zake za kuvutia katika visiwa vya Zanzibar,lakini pia matembezi ya safari ya kutazama wanyama pori pamoja na mlima mrefu barani Afrika,Kilimanjaro,yote hayo yakiwa vivutio vikubwa kwa watalii.

Mnamo mwaka 2010 kiasi wanyama 116 pamoja na ndege  16 baadhi wakiwa ni wanyama wanaotakiwa kulindwa walisafirishwa  kutoka uwanja wa ndege wa Kilimanjaro,huko kaskazini mwa nchi hiyo kwa ndege ya shirika la ndege la Qatar.

Kwa mujibu wa vyombo vya habari vya ndani ya Tanzania, miongoni mwa wanyama hao walikuwemo twiga wanne, aina chungunzima ya paa,na ndege aina ya Tai.

Mwandishi:Saumu Mwasimba

Mhariri:Hawa Bihoga