Wafadhili wakutana Kuwait kuichangia Syria | Matukio ya Kisiasa | DW | 15.01.2014
  1. Inhalt
  2. Navigation
  3. Weitere Inhalte
  4. Metanavigation
  5. Suche
  6. Choose from 30 Languages
Matangazo

Matukio ya Kisiasa

Wafadhili wakutana Kuwait kuichangia Syria

Wafadhili wanakutana leo nchini Kuwait kuchangisha fedha zitakazowasaidia raia milioni 13 wa Syria walioathirika na vita. Umoja wa Mataifa umeiomba jumuiya ya kimataifa kuchangisha dola bilioni 6.5 kuisaidia nchi hiyo.

Huku wasyria wakikabiliwa na msimu wa baridi kali mwaka wa tatu sasa wa vita, wajumbe kutoka nchi 69 na mashirika 24 ya kimataifa wanahudhuria mkutano wa siku moja wa kuchangisha fedha unaosimamiwa na katibu mkuu wa Umoja wa Mataifa, Ban Ki Moon.

Mapigano yamezidi kupamba moto nchini humo na uwezekano wa kufanyika kwa mkutano wa kimataifa wa kutafuta amani Syria nchini Uswisi Jumatano ijayo bado unatiliwa shaka.

Shirika la kimataifa la kutetea haki za binaadamu, Amnesty International, limesema katika taarifa iliyotoa hapo jana kuwa vita vinavyoendelea Syria vimechochea mzozo mbaya zaidi wa kibinaadamu kuwahi kushuhudiwa katika historia ya hivi karibuni duniani.

Mamilioni ya wakimbizi wa Syria wahitaji msaada

Umoja wa Mataifa unatarajia kuchangisha dola bilioni 2.3 kuwasaidia watu milioni 9.3 walioko Syria na dola nyingine bilioni 4.2 kuwasaidia wasyria wanaoishi katika mataifa mengine kama wakimbizi, idadi ambayo inatarajiwa kufikia wakimbizi milioni 4.1 ifikapo mwishoni mwa mwaka huu.

Nembo ya mkutano wa mwaka uliopita wa kuichangia Syria

Nembo ya mkutano wa mwaka uliopita wa kuichangia Syria

Amnesty International inasema wakati ni sasa kwa ulimwengu kukomesha mateso wanayopitia wasyria ambao wengi wao wanakumbwa na uhaba mkubwa wa chakula, dawa na makaazi.

Shirika hilo pia linaitaka serikali ya Syria kuondoa vizuizi vinavyotatiza kufikiwa kwa maeneo ya raia yaliyo katika ngome za waasi.

Mashirika yasiyo ya kiserikali yanayokutana Kuwait hapo jana yaliahidi kutoa dola milioni 400 kuwasaidia raia wa Syria huku Kuwait ambayo ni mwenyeji wa mkutano huo ikiahidi kutoa dola milioni 142 nao Umoja wa Ulaya uliahidi kutoa dola milioni 225.

Kamishna anayeshughulikia misaada wa Umoja wa Ulaya, Kristalina Georgieva, amesema hali ya kibinaadamu nchini humo imezidi kuzorota bila ya kuboreka huku ikikiswa kuwa zaidi ya watu 130,000 wameuawa katika vita vya Syria.

Mzozo wa Syria ndiyo mbaya zaidi katika historia

Umoja wa Mataifa umesema mchango huo kwa ajili ya Syria unaotarajia kuchangisha dola bilioni 6. 5 ndiyo mkubwa zaidi kuwahi kuhitajika kukidhi mahitaji ya mzozo unaolenga nchi moja katika historia yake.

Wakimbizi wa Syria walioko nchini Lebanon

Wakimbizi wa Syria walioko nchini Lebanon

Katika mkutano wa kwanza wa kuichangia Syria mwaka jana ulioandaliwa huko huko Kuwait, nchi zilizoshiriki ziliahidi dola bilioni 1.5 lakini ni asilimia 75 tu iliyotimizwa.

Shirika la chakula duniani, WFP, limesema limeongeza msaada wa kutoa chakula. Kulingana na mashirika ya misaada, wasyria milioni 10.5 wanakabiliwa na uhaba wa chakula, watoto zaidi ya milioni moja wana utapiamlo na karibu nusu ya idadi ya raia wa nchi hiyo hawana maji ya kutosha.

Lebanon kwa hivi sasa ndiyo iliyo na idadi kubwa zaidi ya wakimbizi kutoka Syria ikiwa na wakimbizi 905,000 Jordan ikiwahifadhi wakimbizi 575,000, Uturuki 562,000, Iraq 216,000 na Misri 145,000. Idadi hiyo inatarajiwa kuongezeka maradufu ifikapo mwishoni mwa mwaka huu.

Mwandishi: Caro Robi/afp/Reuters
Mhariri: Josephat Charo

DW inapendekeza

Matangazo

Unaweza kusikiliza matangazo yetu hapa

Kusikiliza matangazo ya Idhaa ya Kiswahili ya DW, tafadhali bonyeza alama ya spika ya masikioni hapo chini, na kuwasiliana nasi, tafadhali tuandikie moja kwa moja kupitia: kiswahili@dw.com