1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Wafadhili waichangishia fedha Congo

13 Aprili 2018

Wafadhili wanakutana mjini Geneva Uswisi Ijumaa katika harakati za kuchangisha dola bilioni 1.7 kwa ajili ya Jamhuri ya Kidemokrasi ya Congo ambayo inakabiliwa na mzozo.

https://p.dw.com/p/2vz7o
Uganda Flüchtlinge aus DR Kongo UNHCR Camp
Picha: Reuters/J. Akena

Wataalam wanasema huenda mzozo huo ukapindukia na kuwa janga kubwa. Mkutano huo unakuja wakati kukiwa na hofu kwamba  mizozo ya kikabila, ufisadi na hali mbaya ya usalama ni mambo yanayozusha hofu ya umwagikaji damu.

Kwa wale walioachwa bila makao, kitisho ni cha kweli. Raia mmoja wa Congo alielezea mzozo wa kikabila katika mkoa wa Ituri kwa kusema, "ni kama wakati tulipokuwa katika vita vya wenyewe kwa wenyewe." Kulingana na makadirio ya shirika la msalaba mwekundu karibu Wacongo 70,000 wamekimbilia Uganda kwa kuuvuka mto Albert tangu Januari. Ituri ni mkoa mmoja tu kati ya mingi ambayo makundi yaliyojihami na wahalifu wanawasumbua raia.

Ukosefu wa usalama umezidisha idadi ya wakimbizi wa ndani ya nchi

Zaidi ya hayo kuna mzozo wa kisiasa unaozunguka suala la urais ambapo watu wengi wanamtaka rais Joseph Kabila ambaye muhula wake ulikwisha Desemba mwaka 2016 ajiuzulu. Lakini makubaliano yanayonuiwa kutoa nafasi ya kipindi cha mpito cha serikali mpya bado hayajatekelezwa na maandamano nchini humo yanadhibitiwa.

Deutschland Treffen Steinmeier mit Filippo Grandi in Berlin
Kamishna wa UNHCR Filippo GrandiPicha: picture-alliance/dpa/R. Jensen

Kulingana na Afisi ya mratibu wa misaada ya kibinadamu ya Umoja wa Mataifa OCHA, ukosefu wa usalama nchini Congo ambao umekuwa ukiendelea umepelekea watu milioni 4.3 kuachwa bila makao nchini mwao. Kamishna wa Shirika la Umoja wa Mataifa kuhusu wakimbizi Filippo Grandi wakati wa ziara nchini Congo wiki iliyopita alisema,

"Kwa bahati mbaya shughuli za wakimbizi katika Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo zinaendelea kukumbwa na uhaba wa fedha na kwa bahati mbaya ndivyo hali hii ilivyo katika sehemu zengine Afrika. Na nataka kuikumbusha jamii ya kimataifa kwamba Afrika bado iko mbali sana kuzifikia nchi tajiri duniani," alisema Grandi. "Idadi kubwa ya wakimbizi hawa hawawezi kusafiri kuelekea Ulaya kuikumbusha dunia kuhusiana na uwepo wao. Wanaishi hapa, wanapitia magumu hapa na wana mahitaji pia," aliongeza Mkuu huyo wa UNHCR.

Waziri Mkuu wa zamani Badibanga ataka maendeleo yazingatiwe baada ya mkutano huu 

Grandi ameitaka jamii ya kimataifa kuongeza viwango vya fedha zilivyojitolea kutoa. Kwa mantiki hii ndiyo mkutano wa uchangishaji fedha wa leo huko Geneva ukaratibiwa ambapo alioupanga ni mwanasiasa na Waziri Mkuu wa zamani wa Congo Samy Badibanga. OCHA, Uholanzi pamoja na Umoja wa Ulaya wamealikwa ili kufanikisha uchangishaji wa dola bilioni 1.7.

Kinshasa Samy Badibanga Pressekonferenz
Waziri Mkuu wa zamani wa DRC Samy BadibangaPicha: Reuters/K.Katombe

Katika mahojiano ya hivi majuzi na DW Badibanga alisema kustawi kwa Congo kunahitaji mshikamano na jamii ya kimataifa.

"Baada ya mkutano huu wa uchangishaji fedha, maendeleo ya nchi lazima yaangaziwe kwasababu ni rahisi sana kwa nchi maskini na ambayo iko nyuma kimaendeleo kutumbukia kwenye machafuko tena," alisema Badibanga.

Lakini serikali ya Congo inapinga mkutano huo wa uchangishaji fedha ikisema Umoja wa Mataifa ulichapisha idadi ya isiyo ya kweli ya wakimbizi waliokimbia kutoka Congo. Msemaji wa serikali ya Congo Lambert Mende alisema kwamba iwapo hakutokuwa na mawasiliano ya kusawazisha idadi ya wakimbizi basi serikali haitohudhuria mkutano huo.

Mwandishi: Philip Sandner

Tafsiri: Jacob Safari

Mhariri: Mohammed Abdul-Rahman