Wafadhili waahidi dola milioni 250 kwa Somalia | Matukio ya Kisiasa | DW | 23.04.2009
  1. Inhalt
  2. Navigation
  3. Weitere Inhalte
  4. Metanavigation
  5. Suche
  6. Choose from 30 Languages
Matangazo

Matukio ya Kisiasa

Wafadhili waahidi dola milioni 250 kwa Somalia

Fedha zitatumika katika vita dhidi ya ugaidi na kuimarisha usalama ndani ya Somalia

Katibu mkuu wa Umoja wa mataifa Ban Ki Moon

Katibu mkuu wa Umoja wa mataifa Ban Ki Moon

Mkutano huo wa kimataifa uliodhaminiwa na Umoja wa mataifa umetoa ahadi ya kuisadia Somalia katika kukabiliana na harakati za maharamia katika pwani yake ambao katika miezi ya hivi karibuni wamekuwa kiendelea kuimarisha harakati zao kwa kuziteka nyara meli kadhaa pamoja na mabaharia.

Kamishna wa Umoja wa Ulaya anayehusika na masuala ya maendeleo Louis Michel amesema fedha zilizoahidiwa kutolewa katika mkutano huo zitatumiwa na serikali ya Somalia kukabiliana na ongezeko hilo la maharamia pamoja na kuimarisha hali ya usalama katika taifa hilo linalokabiliwa na vita vya wenyewe kwa wenyewe.Akizungumza katika mkutano huo katibu mkuu wa Umoja wa mataifa Ban Ki Moon amesema panahitakija pia msaada utakaosaidia kuimarisha jeshi la kuweka amani la Umoja wa Africa lililoko mjini Mogadishu pamoja na maafisa wa polisi na vikosi vingine vya usalama.

''Msaada pia unatakiwa kwa haraka kugharimia mishahara ya wanajeshi na maafisa wa polisi pamoja na kununua vifaa muhimu kama vile mahema na magari ya kijeshi''

Katibu mkuu Ban Ki Moon pamoja na rais wa Somalia Sheikh Sharrif Ahmed wameitolea mwito jumuiya ya wafadhili wa kimataifa kutoa fedha zaidi kwa nchi hiyo ya Africa mashariki fedha zaidi kukabiliana na uharamia pamoja na kurejesha utawala wa kisheria baada ya miongo miwili ya kutokuweko serikali madhubuti.

Aiidha katibu mkuu Ban Ki Moon ameuambia mkutano huo kwamba hali ya utulivu na usalama ni muhimu katika taiafa hilo ikiwa jumuiya ya kimataifa inataka kuona mafanikio ya juhudi za maridhiano pamoja na kuinusuru serikali ya umoja wa kitaifaKatibu huyo mkuu wa Umoja wa mataifa kwa upande mwingine amesisitiza wazi kwamba hana nia ya kupeleka kikosi cha Umoja huo nchini Somalia katika kipindi chochote ingawa amesema hali hiyo inaweza kutokea ikiwa tu hali inaruhusu kuchukuliwa hatua hiyo.

Waandalizi wa mkutano huo unaaongozwa na Ban Ki Moon pamoja na Umoja wa Africa wamesema zaidi ya dolla millioni 250 zinatakiwa kwa ajili ya kuimarisha usalama mwaka ujao nchini humo.

US-Kriegsschiff USS Bainbridge

Meli kadhaa ziko mikononi mwa maharamia wakisomalia

Kwa upande mwingine mkuu wa tume ya Umoja wa Ulaya Jose Manuel Barosso ameitaka jumuiya ya kimataifa na wafadhili kutambua kwamba uharamia nchini Somalia hauwezi kumalizika ikiwa matatizo ya Somalia hayatatafutiwa ufumbuzi,Anasema-

''Vitendo vya uharamia hivi karibuni navishutumu kwa hali zote kwa niaba ya tume ya Umoja wa Ulaya,ndio kiini kilichoishtua jumuiya ya kimataifa,lakini itakuwa ni kosa kwetu sisi kushughulikia tu suala la uharamia,lazima tufahamu kwamba hiyo ndio dalili iliyojitokeza kufuatia matatizo makubwa nchini Somalia.''

Somalia Polizisten in Mogadishu

Maafisa wa usalama wa Somalia mjini Mogadishu

Marekani ambayo kwa upande wake inaingalia upya sera yake kuelekea Somalia inapanga kuisadia katika kujenga upya vikosi vya usalama pamoja na kuipa nguvu serikali ya nchi hiyo lakini imesema kwamba haina nia ya kubakia nchini humo.Harakati za maharamia nchini Somalia zimepamba moto katika nchi hiyo licha ya kuweko kwa vikosi vya kimataifa ikiwemo vikosi maalum kutoka jumuiya ya NATO,Umoja wa Ulaya na Marekani.Meli za kijeshi za kikosi cha Jumuiya Nato zinatazamiwa hii leo kukamilisha shughuli zake katika eneo hilo huku wajumbe wakijadiliana ikiwa muda wa kikosi hicho unabidi kuongezwa.

Wakati huohuo inaarifiwa kwamba kiongozi wa upinzani mwenye msiammao mkali anayetuhumiwa kuhusiana na kundi la al qaeda Sheikh Hassan Dahir Aweys amewasili Mogadishu kwa mara ya kwanza katika kipindi cha miaka miwili akitokea Eretrea alikokuwa amekimbilia kufuatia opresheni za wanajeshi wa Ethiopia nchini Somalia.

Mwandishi Saumu Mwasimba APE

Mhariri Mohammed Abdul-Rahman.

Matangazo

Unaweza kusikiliza matangazo yetu hapa

Kusikiliza matangazo ya Idhaa ya Kiswahili ya DW, tafadhali bonyeza alama ya spika ya masikioni hapo chini, na kuwasiliana nasi, tafadhali tuandikie moja kwa moja kupitia: kiswahili@dw.com