1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Waendesha mashtaka wapekuwa ofisi za VW

8 Oktoba 2015

Waendesha mashtaka nchini Ujerumani wamelipekuwa jengo la kampuni ya magari ya Volkswagen katika makao yake makuu ya Wolfsburg na maeneo mengine

https://p.dw.com/p/1GlFo
Deutschland Wolfsburg Autostadt VW Logo
Picha: picture-alliance/dpa/R. Jensen

Ofisi ya waendesha mashtaka mjini Braunschweig karibu na Wolfsburg walisema nia ya kufanya upekuzi huo ni kupata stakabadhi na kifaa cha kuhifadhi data kufuatia kampuni hiyo kutumia programu ya udanganyifu kukwepwa mitambo inayopima viwango vya uchafuzi wa mazingira.

Upekuzi huo ulifanywa kwa msaada wa waendesha mashtaka watatu wakisaidiana na ofisi ya uchunguzi wa kesi za uhalifu katika jimbo la ujerumani Lower Saxony.

Afisa Mtendaji Mkuu wa Volkswagen Matthias Mueller.
Afisa Mtendaji Mkuu wa Volkswagen Matthias Mueller.Picha: Reuters/F. Bimmer

Nani alihusika na udanganyifu?

Kampuni hiyo ya magari ya Ujerumani ilisema imetoa stakabadhi kadhaa kwa waendesha mashtaka hao. Awali kampuni hiyo ilikwenda mahakamani mnamo tarehe 23 mwezi Septemba kwamba inaunga mkono uchunguzi unaofanywa na waendesha mashtaka katika udanganyifu huo pamoja na watu wanaodaiwa kuhusika katika sakata hilo.

Waendesha mashtaka wanatafuta ushahidi utakaothibitisha ni nani hasaa aliyehusika na sakata hilo na kuelezea ni kwa namna gani udanganyifu huo ulifanyika.

Mkurugenzi wa muda mrefu wa kampuni hiyo Martin Winterkorn alijiuzulu baada ya sakata hilo kuibuka nchini Marekani tarehe 18 mwezi Septemba akisema hakujua kilichokuwa kikiendelea. Nafasi yake ilichukuliwa na Mkuu wa zamani wa kampuni ya Porshe Matthias Mueller.

Volkswagen hadi sasa imewasimamisha kazi watu wanne wakiwemo wakuregenzi watatu waliokuwa wanashughulikia ujenzi wa injini ya magari hayo na kuridhia kampuni ya Marekani kufanyiwa uchunguzi.

Mapema siku ya Alhamisi naibu Kansela wa Ujerumani na waziri wa uchumi Sigmar Gabriel aliutembelea mji wa Wolfsburg yanakotengenezwa magari ya Volkswagen, kuonesha mshikamano na wafanyakazi wa kampuni hiyo na kuwaka wajitahidi zaidi, kujisafisha kutokana na kashfa hiyo.

Watu wakiwasili katika makao makuu ya Volkswagen mjini Wolfsburg, Ujerumani.
Watu wakiwasili katika makao makuu ya Volkswagen mjini Wolfsburg, Ujerumani.Picha: Getty/AFP/R. Hartmann

Naibu Kansela awapa moyo wafanyakazi

Sigmar Gabriel, alishiriki mkutano wa wawakilishi wa kampuni hiyo kutoka Ujerumani wakati wakijaribu kupata jibu la nani aliweka chombo cha udanganyifu katika magari milioni 11 inayotumia mafuta ya dieseli ili kuzuwiya kusoma utoaji wa gesi unaochafua mazingira. Gabriel amesema ni muhimu kutuma ujumbe kwamba wafanyakazi wa kampuni hawatalipia makosa yaliofanywa na wakurugenzi au meneja wa kampuni hizo.

Kwengineko kampuni hiyo ya Volkswagen iliwasilisha mipango yake kwa serikali kuhusu kuyarekebisha magari yaliyoathirika, ikisema itachukuwa hadi mwaka ujao kwa suala hilo kutatuliwa. Mkurugenzi mkuu mpya wa kampuni hiyo Matthias Mueller amesema iwapo mambo yatakwenda kama yalivyopangwa kazi hiyo itaanza mwezi Januari, na kwamba kufikia mwishoni mwaka 2016, magari yote yatakuwa yamerekebishwa.

Mwandishi: Amina Abubakar

Mhariri: Iddi Ssessanga