1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Wachimba mgodi waliyonasa Chile waanza kuokolewa

13 Oktoba 2010

Hatimaye zoezi la kuwaokoa wachimbaji 32 waliyonasa katika mgodi mmoja nchini Chile kwa muda wa siku 69 limeanza.

https://p.dw.com/p/PdEh
Mchimba mgodi wa kwanza kuokolewa Florencio Avalos.Picha: AP

Ilikuwa ni shangwe na vilio vya furaha pale mchimbaji wa kwanza alipookolewa.Florencio Avalos ndiyo alikuwa wa kwanza kutoka ambapo walinasa zaidi ya mita 600 chini ya ardhi,na kupokelewa kwa shangwe na watu waliyokuwepo na kushuhudiwa na dunia nzima kutokana na wingi wa vyombo vya habari vilivyoko katika eneo la tukio, kama anavyosimulia mwandishi huyu wa televisheni ya BBC.

´´Florencio Avalo analia hapa anaonana na baba yake kwa mara ya kwanza baada ya siku 69, kila mtu anaangalia tukio hili la kusisimua na kushindwa kuamini baada ya siku nyingi kama hizi.Hiki ndicho kinachotokea hivi sasa´´

Chile Bergleute Bergarbeiter Rettung
Rais wa Chile Sebastian Pinera (mbele) akikumbatiana na Florencio AvalosPicha: AP

Rais Sebastian Pinera wa Chile alikuwepo kuwalaki wachimba mgodi hao. ambao wanachukuliwa kama mashujaa.Rais Pinera alikumbatiana na Avalos, na baadaye kuwaambia waandishi wa habari.

´´Florencio amenishukuru mimi kwa niaba ya wenzake waliyonaswa kwa muda wa siku 69.Anatoa shukurani wa serikali ya Chile na watu wa Chile na ameniambia kuwa tokea siku ya kwanza waliponasa walitambua kuwa hawako pekee yao wanaungwa mkono na taifa lote´´

Kelele za furaha zilizidi kuwa kubwa zaidi pale mchimbaji wa pili Mario Sepulveda alipotoka. Sepulvedo mwenye umri wa miaka 40 alitoka huku akiwa ameshika kipande cha mwamba na kukitoa kama zawadi kwa maafisa na waokoaji, huku akitabasamu na kumwemweseka, kabla ya kujiunga na watu waliyokuwepo kushangalia.Baadaye akiwa katika hali ya umakini, alisema

Chile Bergleute Bergarbeiter Rettung Mario Sepulveda
Mario Sepulveda akiungana na watu kushangalia kuokolewaPicha: AP

´´ Nilikuwa na mungu pamoja na shetani, nilikuwa katikati yao kupambana.Hatimaye nilifanikiwa kukamata mkono wa mungu.Ulikuwa ni mkono unaostahiki kushikwa.Siku zote nilikuwa na imani na kujua kuwa mungu atatutoa hapa´´

Viongozi mbalimbali dunia wametuma salam za pongezi, miongoni mwao akiwa Rais Barack Obama wa Marekani ambaye amesema kwa uwezo wa mwenyezi mungu ana imani wachimba mgodi hao wataungana na familia zao wakiwa na afya njema.

Serikali ya Chile imeahidi kuwa itawahudumia wachimba mgodi hao na kuhakikisha kuwa wanakuwa katika afya, ambapo kwenye eneo la zoezi kuna timu ya wauguzi.Pia wamepelekwa katika hospitali iliyo karibu na eneo hilo.Watalaam wa afya wamesema kuwa hali za afya za wachimba mgodi hao zitakuwa za kawaida.

Rais wa Bolivia Evo Morales alikuwa akitarajiwa kuwasili katika eneo la tukio.Mmoja kati ya wachimba mgodi 32 waliyonasa Carlos Mamani ni raia wa Bolivia.

Mwandishi:Aboubakary Liongo/BBC/CNN/DPA/ZPR/AFP

Mhariri:Mohamed Abdulrahman