Wabunge wa Afghanistan wamtaka rais Ghani ajiuzulu | Matukio ya Kisiasa | DW | 30.09.2015
  1. Inhalt
  2. Navigation
  3. Weitere Inhalte
  4. Metanavigation
  5. Suche
  6. Choose from 30 Languages
Matangazo

Matukio ya Kisiasa

Wabunge wa Afghanistan wamtaka rais Ghani ajiuzulu

Wabunge wa Afghanistan wamemtaka rais Ashraf Ghani kujiuzulu kutokana na namna serikali yake ilivyoshughulikia mapigano ya mji wa Kaskazini wa Kunduz ambao sasa uko mikononi mwa wanamgambo wa Taliban.

Rais wa Afghanistan Ashraf Ghani

Rais wa Afghanistan Ashraf Ghani

Wanamgambo hao wa Taliban waliuteka mji wa Kunduz baada ya kufanya shambulizi la kijasiri mjini humo siku ya Jumatatu na kuapa kuendelea kupambana na vikosi vya Afghanistan. Hata hivyo maelfu ya polisi na wanajeshi waliochoka wamekwama katika uwanja wa ndege wa mji huo wa Kunduz wakisubiri msaada kutoka maeneo mengine ya nchi.

"Ni aibu kwa namna serikali ilivyoishughulikia hali mjini Kunduz, Rais Ghani pamoja na Wazir Mkuu mtendaji Abdulla Abdulla ni lazima wajiuzulu," alisema Iqbal Safi, mbunge kutoka mkoa wa Kapisa wakati wa kikao cha bunge kilichokuwa kinapeperushwa moja kwa moja kupitia televisheni ya kitaifa.

Baadhi ya wanamgambo wa Taliban

Baadhi ya wanamgambo wa Taliban

Kutekwa kwa mji wa Kunduz ni pigo kubwa kwa utawala wa Ashraf Ghani tangu alipoingia madarakani mwaka mmoja uliopita, mji huo umekuwa mji wa kwanza mkubwa kutekwa tena na wanamgambo tangu mwaka wa 2001. Aidha wabunge wengine waliiunga mkono hoja ya mbunge Iqbal Safi, kwa kupiga kelele bungeni wakitaka wazee wakutane mara moja ili kuanza mchakato wa kumuondoa rais Ghani.

Mwaka wa kwanza wa rais huyo wa Afghanistan umekumbwa na mapigano na mgogoro wa kisiasa ambapo Umoja wa Mataifa umetoa idadi ya majeruhi 5,000 katika nusu ya kwanza ya mwaka.

Kwa upande wake naibu msemaji wa rais Ghani, Sayed Zafar Hashemi, amesema ni haki ya bunge kulalamika, lakini akasema kitu ambacho rais anakipa kipaumbele ni usalama wa watu wa Kunduz na kuwatokomeza au kuwaondoa kabisa magaidi katika eneo hilo.

Ameongeza kuwa wanajeshi wa Afghanistan wanapiga hatua na tayari rais ameagiza uchunguzi ufanywe kubaini ni kwa nini mji wa Kunduz umetekwa kiurahisi na wanamgambo.

Wanajeshi maalum wa NATO watoa msaada kwa wanajeshi wa Afghanistan

Kikosi maalum cha wanajeshi wa NATO chawasili mjini Kunduz

Kikosi maalum cha wanajeshi wa NATO chawasili mjini Kunduz

Huku hayo yakiarifiwa Jumuiya ya kuijihami ya NATO imesema kikosi maalum cha wanajeshi wake wa kigeni kimefika Kunduz kuwasaidia wanajeshi wa Afganistan, na tayari vikosi vya marekani vimefanya mashambulizi ya angani mara tatu tangu siku ya Jumanne. Vikosi maalumu vilivyofika Kunduz vinajumuisha vile vya Marekani, Uingereza na Ujerumani.

Vile vile mapigano makali yameripotiwa karibu na maeneo ya uwanja wa ndege huku wanamgambo wa Taliban wakiendelea kuusogelea hii ikionesha wazi changamoto iliyopo ya kuukomboa mji wa Kunduz.

Kulingana na Wizara ya Afya ya Afghanistan hadi sasa hospitali mjini Kunduz zimepokea miili 30 na zaidi ya watu 200 waliojeruhiwa.

Mwandishi: Amina Abubakar/Reuters/AFP

Mhariri: Josephat Charo

Matangazo

Unaweza kusikiliza matangazo yetu hapa

Kusikiliza matangazo ya Idhaa ya Kiswahili ya DW, tafadhali bonyeza alama ya spika ya masikioni hapo chini, na kuwasiliana nasi, tafadhali tuandikie moja kwa moja kupitia: kiswahili@dw.com