1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Waasi watishia kulipiza kisasi Myanmar

30 Machi 2021

Idadi ya waliokufa katika ukandamizaji wa jeshi la Myanmar dhidi ya waandamanaji imepita watu 500, wakati makundi ya waasi wenye silaha leo Jumanne wakitishia kulipiza kisasi iwapo umwagaji damu hautasitishwa.

https://p.dw.com/p/3rNJL
Myanmar Militärputsch Protest Ermordete Demonstranten
Picha: AP Photo/picture alliance

Viongozi wa dunia wanaendelea kukosoa kampeni ya jeshi dhidi ya wanaharakati wanaopinga mapinduzi na kutaka kurejeshwa kwa serikali iliyochaguliwa pamoja na kutaka kuachiliwa kwa kiongozi wa raia Aung San Suu Kyi.

Marekani imesitisha makubaliano ya kibiashara na Myanmar na Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, Antonio Guteres, ametoa wito kwa umoja wa ulimwengu kushinikiza jeshi, baada ya waandamanaji zaidi kuuawa.

Soma zaidi:  Hali yazidi kutisha Myanmar

Wakati huo huo makundi matatu ya waasi wa kikabila yamelaani ukandamizaji huo na kutishia kujiunga pamoja na waandamanaji iwapo wanajeshi wataanzisha tena vurugu.

Makundi hayo ya Taang National Liberation Army, Myanmar Nationalities Democratic Alliance Army na Arakan Army yameungana na kutoa tamko la pamoja dhidi ya utawala wa jeshi.

Debbie Stothard mwanaharakati wa Shirikisho la Kimataifa la Haki za Binadamu (FIDH) ameoonya kuwa kuungana kwa makundi haya kunaweza kuibua vita vya wenyewe kwa wenyewe.

Soma zaidi: Amnesty yaorodhesha ukatili dhidi ya waandamanaji Myanmar

Wakimbizi walioitoroka Myanmar wadaiwa kufukuzwa Thailand

Weltspiegel 30.03.2021 | Myanmar Thailand | Ankunft Flüchtlinge aus Karen in Mae Hong Son
Picha: Karen Women's Organization/Reuters

Takriban watu 3,000 wamekimbia Myanmar kupitia msituni kutafuta usalama katika mpaka wa Thailand. Lakini wanaharakati wameiambia AFP kuwa mamlaka ya Thai imewafukuza wakimbizi hao kwa madai ya kuwazuia viongozi wa Umoja wa Mataifa katika kambi hio.

Hata hivyo Msemaji wa wizara ya mambo ya nje wa Thailand Tanee Sangrat amesisitiza kuwa ripoti za kuwafukuza wakimbizi sio sahihi.

Rais Joe Biden hapo jana alitangaza kuwa Mkataba wa Mfumo wa Biashara na Uwekezaji wa 2013, ambao haakuwa umekamilika ambao ni msingi wa kukuza biashara utasimamishwa hadi demokrasia itakaporejeshwa Myanamar.

soma zaidi:  Umoja wa Mataifa kuijadili Myanmar Jumatano

Vyanzo vya kidiplomasia vimedokeza kuwa Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa litakutana kesho Jumatano kujadili hali hiyo, baada ya Uingereza kutaka mazungumzo ya dharura.

Myanmar Monywa | Proteste gegen Militärregierung
Picha: AFP

Ufaransa imelaani vurugu hizo na China imejumuika katika kupaza sauti na kutoa wito kwa pande zinazozozana kusitisha vurugu.

Urusi imesema ina wasiwasi sana juu ya kuongezeka kwa majeruhi miongoni mwa raia, licha ya kukiri kwamba ilikuwa ikiunda uhusiano na mamlaka ya jeshi. 

Marekani, Uingereza na Umoja wa Ulaya wameweka vikwazo kwa kujibu mapinduzi na ukandamizaji, lakini hadi sasa shinikizo la kidiplomasia halijawashawishi majenerali kusitisha vurugu hizo.

 

Chanzo AFP