1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Waasi watimuliwa na vikosi vya Chad

4 Februari 2008
https://p.dw.com/p/D1ro

NDJAMENA:

Majeshi ya Chad yametumia helikopta na vifaru kuvitimua vikosi vya waasi vilivyozingira Ikulu ya rais baada ya kuuvamia mji mkuu,Ndjamena.Kwa mujibu wa Balozi wa Chad nchini Marekani Mahamoud Adam Bechir,waasi wametimuliwa na sasa serikali imedhibiti hali ya mambo.Akaongezea kuwa Rais Deby yupo Ikulu mjini Ndjamena

Lakini kwa mujibu wa msemaji wa waasi,vikosi vyao vimerejea nyuma ili kuwapa raia nafasi ya kuondoka mji mkuu na baadae waasi wataendelea na mashambulio yao.Ripoti za mashahidi zinasema,maiti nyingi zipo barabarani kufuatia mapigano ya siku mbili.

Wakati huo huo serikali ya Chad imesema kuwa imefanikiwa kukomesha mashambulizi mengine ya waasi karibu na mpaka wa Sudan na imeituhumu Khartoum kuwa inawasaidia waasi wanaojaribu kumpindua Rais Idriss Deby.Rais Nicolas Sarkozy wa Ufaransa amelaani vikali majeribio ya kutaka kumuondosha Deby madarakani.Ufaransa imewahamisha zaidi ya raia 500 wa kigeni kutoka Chad na kuwapeleka nchi jirani ya Gabon.Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Ban Ki-Moon amesema,ameingiwa na wasiwasi kuhusu matukio ya Ndjamena.