1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Waasi wasonga mbele Tchad

Hamidou, Oumilkher17 Juni 2008

Rais Idriss Déby awatuhumu wanajeshi wa EUFOR kuwasaidia waasi

https://p.dw.com/p/EL3N
Wakimbizi wa TchadPicha: picture-alliance/ dpa



Rais Idriss Déby wa Tchad amewatuhumu wanajeshi wa Umoja wa Ulaya wanaotumikia  kikosi cha EUFOR "kufumbia macho mauwaji ya raia na wakimbizi" yanayofanywa na waasi mashariki ya nchi hiyo.


Akilihutubia taifa kwa njia ya televisheni jana usiku,rais Idriss Deby ameshuku kwa mara nyengine tena umuhimu wa kuwepo wanajeshi wa Umoja wa Ulaya nchini Tchad.Shutuma zake dhidi ya wanajeshi wa EUFOR zimejiri katika wakati ambapo hali ya kutatanisha imetanda mashariki ya Tchad kufuatia siku tano za mashambulio ya waasi.


"Tuna haki ya kujiuliza kama kweli kuna haja  ya kuwepo wanajeshi kama hao katika ardhi ya Tchad" amesema rais Idriss Déby na kuongeza tunanukuu:"kuna njama ya kimataifa iliyodhamiriwa kuitumbukiza Tchad katika janga la vita vya wenyewe kwa wenyewe" mwisho wa kumnukuu.


Wanajeshi wa EUFOR wamepelekwa Tchad kutokana na maombi ya Umoja wa mataifa ili kuwalinda wakimbizi laki tano waliokimbilia mashariki ya Tchad wakiyapa kisogo mapigano ya Darfour nchini Sudan.


Rais Idriss Déby anawatuhumu wanajeshi wa EUFOR kwa kile anachokiita tunanukuu;" kusaidiana na waasi,kuwaachia wachukue magari ya mashirika ya misaada ya kiutu,kutia moto ghala za vyakula na mafuta na kufumbia macho mauwaji ya raia na wakimbizi wasiokua na hatia."Mwisho wakumnukuu rais Idris Déby wa Tchad.


Kiongozi huyo ameonya wanaogharimia njama ya "kuiteketeza" nchi yake watakiona cha mtema kuni.


Waziri wake wa mawasiliano ,ambae pia ni msemaji wa serikali,Mahamat Hissene anasema:


"Ni shambulio jengine lililoandaliwa na serikali ya Sudan dhidi ya Tchad.Tchad imehujumuiwa na milolongo ya waasi waliopanda magari ya mashirika ya misaada ya kiutu katika mikoa ya Wadaa na Darsillah.Ni maeneo yasiyokua na ulinzi wa kijeshi na hali hii inatokea katika wakati ambapo kampeni inaendeshwa ili kutoa picha ya kusonga mbele waasi."


Wakati huo huo waasi wamesema hivi punde wamefanikiwa kuuteka mji wa Am Zoer,kilomita 80 kaskazini mashariki ya Abeche na kumkamata afisa wa ngazi ya juu wa kijeshi wa eneo hilo.


Abeche ,mji muhimu mashariki ya Tchad karibi na mpaka na Sudan,ndiko kunakokutikana kituo kikuu cha jeshi la Tchad na huko ndiko helikopta za kijeshi zilikowekwa.


Msemaji wa  Alliance Nationale -Muungano wa taifa unaoyaleta pamoja makundi kadhaa ya waasi,Ali Guedei amesema wameshaondoka Biltine mji waliouteka jana na kunyakua pia kifaru cha kijeshi .


Kwa upande wa kidiplomasia,umoja wa Afrika , baraza la usalama la umoja wa mataifa na katibu mkuu wa umoja wa mataifa Ban Ki-Moon wamelaani mashambulio ya waasi.Umoja wa mataifa unafikiria hatua "zinazofaa" dhidi ya makundi yanayotishia utulivu katika eneo la mashariki la Tchad."





►◄