1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Waasi wameanza mapambano mapya dhidi ya vikosi vya Gadhafi

1 Aprili 2011

Waasi nchini Libya wameanza mapambano mapya dhidi ya vikosi vinavyomtii Kiongozi wa Libya Mummar Gadhafi katika eneo lenye hazina ya mafuta la Brega

https://p.dw.com/p/10lqy
Waasi nchini LibyaPicha: AP/dapd

Waasi hao wamesema, nguvu hiyo mpya inashabaha ya kuresheja maeneo kadhaa ambayo walikuwa wameyateka kwa takribani wiki mbili zilizopita.

Mapambano yanafanyika umbali wa kilometa 800 mashariki mwa mji wa Tripoli na kwamba waasi wamewazuia raia pamoja na waandishi wa habari kufika katika uwanja wa mapambano.

Krieg in Libyen
Waasi wakiwa katika mapambanoPicha: dapd

Wakiwa katika eneo la maandalizi ya kivita huko mashariki mwa mji wa Ajdabiyah, Waasi walifanya ukaguzi wa zana zao na kuzuia raia wasio na silaha kushiriki mampambano katika eneo la mpakani mwa eneo hilo na Brega ambapo vikosi vya Gadhafi vimeweka kambi.

Waasi wamedai mpaka sasa hakuna atakayejigamba kuwa analishikilia eneo hilo lenye mafuta kwa kuwa wamekuwa wakilichukua na kunyang'anywa kwa takriban wiki kadhaa sasa.

Vikosi vya Gadhafi, vimejiandaa vizuri kijeshi lakini waasi ambao wamekuwa wakisaidiwa na makombora ya ndege za kivita za vikosi vya muungano walionekana kushindwa kumudu kishindo cha wapinzani wao katika mapambano yaliyopita.

Khaled al- Farjani, aliwahi kuwa rubani wa ndege za kivita na hivi sasa amejiunga na waasi anasema, kama Mungu akijalia wataanza kuurejesha mji wa Ajdabiyah alafu Brega kisha Ras Lanuf.

Miji ya Ras Lanuf na Es Sider kwa hivi sasa ipo katika himaya ya vikosi vinavyomuunga mkono Kanali Gadhafi ambavyo vinatumia silaha kali kupambana na waasi.

Lakini Waasi wenyewe pamoja na tatizo la silaha duni walizonazo bado hawana mafunzo ya kivita.

Katika harakati nyingine za upande huo wa waasi, Shirika la Habari la Uingereza-Reuters limeripoti kwamba kiasi cha magari kumi yameonekana yakitoka eneo la Bengazi kuelekea Ajdabiyah yakiwa na zana za kivita.

Hata hivyo taarifa hiyo ya Reuters, haikuweza kubainisha tamati ya safari hiyo ya kivita.

Mpango huu mpya wa waasi unatazamwa kama unaweza kufanikiwa baada ya kufurushwa na vikosi vya Gadhafi na kuiacha miji waliyokuwa wakiishikilia katika kipindi cha siku mbili zilizopita.

Marekani, Ufaransa na Uingereza ambao wamekuwa wakiendeleza mashambulizi ya makombora ya anga, wamekuwa wakijadili uwezekano wa kuwapa silaha waasi hao.

Hata hivyo kuna habari za kichini chini kwamba rais Obama ametia saini mpango wa siri kuwasaidia waasi.

Awali Katibu Mkuu wa NATO Anders Fogh Rasmussen alisema"Nato itashiriki kikamilifu kutekeleza azimio la Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa,nalo ni tutakuwa huko kuwalinda Walibya, wala si kudhuru."

Shirika la habari la Reuters lilifanikiwa kuzungumza na mpiganaji mmoja muasi Zaitoun akiwa mstari wa mbele na kumuuliza kama kuna uwezeshwaji wowote wa zana za kivita kutoka nchi za magharibi na alionesha mshangao.

Mpiganaji huyo alisema amesikia maneno mengi lakini mpaka sasa hakuna hata moja lililotekeleza huku akisema kama wangalikuwa na vifaa vya kisasa basi mambo yangekuwa mazuri kwao.

Mwandishi: Sudi Mnette /RTRE/AFP

Mhariri: Josephat Charo