1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Waasi wakubali kusitisha mapigano Chad

3 Februari 2008
https://p.dw.com/p/D1aP

NDJAMENA:

Kiongozi wa waasi wa Chad,Mahamat Nouri amekubali kusitisha mapigano dhidi ya vikosi vya serikali kufuatia juhudi za upatanisho za Rais Muammar Gaddafi wa Libya.Kwa mujibu wa shirika la habari la Libya-JANA-pande hizo mbili zinatazamiwa kukutana kwa majadiliano ya kutekeleza makubaliano ya amani na upatanisho.Rais Gaddafi alichaguliwa na Umoja wa Afrika siku ya Jumamosi kama mpatanishi katika mgogoro huo wa Chad.Mapigano makali yalizuka siku ya Jumamosi katika mji mkuu Ndjamena baada ya waasi kuuvamia mji huo na kuyazingira makazi rasmi ya Rais Idriss Deby.Waasi wametishia kumpindua Deby ikiwa hatokubali kujadili makubaliano ya kugawana madaraka.

Ufaransa imeshaanza kuwahamisha raia wake na wa nchi zingine za kigeni kutoka Ndjamena.Umoja wa Mataifa pia unapanga kuwahamisha wafanyakazi wake kutoka Chad.Wakati huo huo msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Ujerumani mjini Berlin amesema,serikali ya Ujerumani inatayarisha mpango wa kuhamisha raia wake kutoka Chad iwapo kutakuwa na haja ya kufanya hivyo.