1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Waasi wakamata kijiji muhimu kutoka jeshi la serikali Aleppo

6 Mei 2016

Makundi ya wapiganaji nchini Syria yamekamata kijiji muhimu kutoka majeshi ya serikali leo(06.05.2016)katika mapigano makali kusini mwa Aleppo na watu 73 waliuwawa,licha ya usitishaji mapigano kwa masaa 48 mjini Aleppo.

https://p.dw.com/p/1Ij0h
Syrien Zerstörung in Aleppo
Magofu yanaonekana kila sehemu katika mji wa AleppoPicha: Getty Images/AFP/K. Al-Masri

Makundi ya wapiganaji ikiwa ni pamoja na Al - Nusra Front lenye mafungamano na al-Qaeda , jana yalianzisha mashambulizi dhidi ya majeshi ya serikali katika kijiji cha Khan Touman , ambacho ni muhimu kwa sababu ya eneo kilichopo karibu na njia kuu kutoka Damascus kwenda Aleppo.

Syrien Zerstörung in Aleppo
Watu wa familia moja wakipita katika majengo yaliyoharibiwaPicha: Getty Images/AFP/K. Al-Masri

Wakati huo huo mashambulizi ya anga yamesababisha kuuwawa watu 28 katika kambi iliyotengwa kwa ajili ya watu wanaokimbia makaazi yao Kaskazini mwa Syria karibu na mpaka na Uturuki wakati usitishaji mapigano kwa muda wa masaa 48 ukiendelea mjini Aleppo.

Usitishaji wa mapigano umekuja baada ya mapigano makali ndani na kuzunguka mji wa Aleppo na kuwezekana wakati utawala wa rais Bashar al-Assad na waasi wamekubali kufanya hivyo kutokana na mbinyo wa kidiplomasia kusitisha mapigano.

Syrien Krieg Kämpfe in Aleppo
Watu wakipita katika vifusi vya nyumba zilizoharibiwa mjini AleppoPicha: Reuters/A. Ismail

Lakini wakati raia wakiingia mitaani baada ya wiki mbili za mapigano makali katika mji huo uliogawika, eneo muhimu la mapigano katika vita vya miaka mitano sasa nchini Syria, wengine wameshambuliwa upande wa magharibi ya mji huo.

Mashambulizi ya anga

Shirika linaloangalia haki za binadamu nchini Syria limesema mashambulizi ya anga yameilenga kambi karibu na Sarmada, katika jimbo la Idlib , ambalo linadhibitiwa na kundi lenye mafungamano na al-Qaeda la Al-Nusra Front.

Al-Nusra Front na washirika wao walikamata kijiji cha Khan Touman na vijiji vya karibu baada ya mapigano yaliyochukua chini ya masaa 24, kwa mujibu wa shirika linaloangalia haki za binadamu nchini Syria.

Syrien Bombardiertes Krankenhaus in Aleppo Tariq al-Bab
Majengo yaliyoporomoka mjini AleppoPicha: Reuters/A. Ismail

"Kiasi ya wapiganaji 43 wa Al-Nusra, ikiwa ni pamoja na kamanda wao wa eneo hilo, na 30 katika upande wa jeshi la serikali na wanamgambo wanaowaunga mkono wameuwawa katika mapigano hayo, limesema shirika hilo lenye makao yake makuu nchini Uingereza, ambalo linategemea mtandao wake wa vyanzo vinavyowapatia habari nchini Syria.

Majeshi yanayoiunga mkono serikali yaliwafurusha wapiganaji hao wa jihadi kutoka Khan Touman, kijiji kilichoko kilometa 10 kusini magharibi mwa Aleppo , mwezi Desemba.

"Kukamatwa kwa eneo hilo na vijiji vya karibu kuna maana maeneo ya kujihami ya majeshi ya serikali kusini mwa mji wa pili nchini Syria wa Aleppo yamerudishwa nyuma," mkuu wa shirika hilo Rami Abdel Rahman amesema.

Muziki mjini Palmyra

Makubaliano ya kusitisha mapigano kwa masaa 48 kati ya majeshi ya serikali na waasi ambao si wapiganaji wa jihadi yanaonekana kwa kiasi kikubwa kuendelea wakati yakiingia katika siku ya pili leo Ijumaa.

Syrien Krieg Kämpfe in Region Aleppo 2012
Wapiganaji waasi wakipambana na majeshi ya serikaliPicha: picture-alliance/dpa/Maysun

Wakati huo huo wanamuziki mashuhuri wa Urusi jana walipiga muziki wa klasiki katika ukumbi wa kale katika mji uliokumbwa na mapigano wa Palmyra katika hatua ya serikali ya Urusi kuonesha mafanikio yake katika mji huo wa kale. Mkuu wa kitengo cha kutegua mabomu ya ardhini wa Urusi Yuri Mikhailovich amesema.

"Tumesafisha hekta 234 za ardhi, majengo 10 ya kihistoria na kuripua vifaa vya kuripuka 2,991 katika mji wa kale wa Palmyra."

Muongozaji mashuhuri wa muziki huo Valery Gergiev aliongoza okestra maarufu ya kutoka mji wa Saint Petersburg ya Mariinsky kwa kupiga muziki wa Sebastian Bach, Sergei Prokofiev na Rodion Shchedrin mbele ya kundi la wanajeshi wa Urusi, mawaziri wa serikali na waandishi habari.

Mwandishi: Sekione Kitojo / afpe / rtre

Mhariri: Daniel Gakuba