1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Waasi wajisalimisha DRC

Benjamin Kasembe20 Septemba 2021

Zaidi ya waasi 700 kutoka katika  baadhi  ya makundi ya wanamgambo waliripotiwa kujisalimisha mbele ya jeshi la Jamhuri ya Kidemokrasi ya Congo huko Kivu ya kaskazini katika kipindi cha miezi minne tangu kutangazwa kwa serikali ya kijeshi tarehe 6 Mei. Sikiliza ripoti kamili na mwandishi wetu wa Goma Benjamin Kasembe.

https://p.dw.com/p/40YYK

Huku hayo yakiarifiwa mawakala kutoka asasi za kiraia wamedai  hakuna mafanikio yoyote wakati huu ambapo mamia ya wananchi bado waendelea kuuawa na wengine kadhaa kuvitoroka vijiji vyao katika mikoa ya Kivu kaskazini na Ituri.
 
Akiuhutubia mkutano wa wandishi habari mwishoni mwa juma lililopita  katika mji huu wa Goma,msemaji wa jeshi hapa kivu ya kaskazini amesifu kwanza juhudi za jeshi la Jamuhuri ya Kidemokrasi ya Congo katika operesheni zinazo lenga kuyatokomeza makundi ya waasi yanayo endesha mauwaji dhidi ya raia.

Tangu kutangazwa  mamlaka ya kijeshi terehe 6 mei imekadiriwa, zaidi ya silaha 400 pamoja na wapiganaji 700 walijisalimisha mbele ya jeshi la Congo na takriban aslimia 90 ya vijiji vilivyo kuwa awali chini ya uongozi wa wanamgambo vimedhibitiwa na jeshi tiifu kwa serikali.

Mbali na tangazo  hilo la maafisa wa jeshi  hapa kivu ya kaskazini, miungano ya kiraia pamoja na mawakala wanao tetea haki za binadamu wamekua wakivishutumu vyombo vya usalama kufuatia ongezeko la visa vya uhalifu vinavyofanywa na makundi ya waasi.

Hata hivyo kulingana na ripoti iliyo tolewa mapema mwanzoni mwa wiki iliopita na shirika la kutetea haki za binadamu, Human Rights Watch imekadiria kuwa watu wasio pungua 672 waliuawa katika mashambulizi yaliyoendeshwa na makundi ya wanamgambo tangu kutangazwa  kwa serikali yakijeshi hadi septemba 10 mwaka huu.

Hali hii   imewatia  sasa wasiwasi mkubwa wananchi ambao baadhi wamesema wamepoteza matumaini yao kwa juhudi za utafutaji wa amani  katika wilaya ya Beni na ndani ya maeneo kadhaa yanayo gubikwa na vurugu za vita.

 
Tangu kuwekwa kwa mamlaka yakijeshi katika mikoa ya kivu kaskazini na Ituri usalama wa wananchi bado unasalia kuwa tete nakuwafanya maelfu kutoroka miji na vijiji vyao ili kupata hifadhi ndani ya maeneo yanayo dhaniwa kuwa ni tulivu lakini bila msaada wa vyakula na maji safi.


Mhariri: Yusuf Saumu