Waasi wadungua helikopta Ukraine | Matukio ya Kisiasa | DW | 30.05.2014
  1. Inhalt
  2. Navigation
  3. Weitere Inhalte
  4. Metanavigation
  5. Suche
  6. Choose from 30 Languages
Matangazo

Matukio ya Kisiasa

Waasi wadungua helikopta Ukraine

Rais Mteule wa Ukraine Petro Poroshenko ameapa kuwaadhibu waasi wanaoiunga mkono Urusi ambao wameiangusha helikopta ya kijeshi mashariki mwa nchi hiyo na kuuwa wanajeshi 12 akiwemo generali mmoja.

Mpiganaji wa waasi katika mji wa Donetsk.

Mpiganaji wa waasi katika mji wa Donetsk.

Wanamgambo walidunguwa helikopta chapa Mi-8 kutoka angani kwa kutumia kombora la kutoka ardhini hapo jana jambo lililoifanya Ikulu ya Marekani kusema kwamba tukio hilo linazusha wasi wasi kwamba waasi hao wamekuwa wakipatiwa silaha kutoka nje.

Poroshenko amesema itabidi wafanye kila inalowezekana kuhakikisha hakuna Waukraine zaidi wanaokufa mikononi mwa waasi na majambazi. Amesema vitendo vya kihalifu vinavyofanywa na maadui wa wananchi wa Ukraine vitaadhibiwa.

Hapo jana Kaimu rais wa Ukraine Alexander Turchynov aliliarifu bunge kwamba alipata taarifa kwamba magaidi wakitumia kombora la kisasa la kudungulia ndege wameiangusha helikopta karibu na mji wa Slavyansk na kusababisha kifo cha Generali Volodymyr na wanajeshi sita wa kikosi cha Ulinzi wa Taifa kinachoundwa na wapiganaji wa kujitolea na wanajeshi wa wizara ya mambo ya ndani.

Kaimu Rais wa Ukraine Alexander Turchynov.

Kaimu Rais wa Ukraine Alexander Turchynov.

Turchynov amesema "Nina imani kwamba jeshi letu la ulinzi na taasisi zetu za usalama zitakamilisha kazi ya kuwatokomeza magaidi.Wahalifu wote wanaogharamiwa na shirikisho la Urusi wataangamizwa au kufikishwa mahakamani.”

Baadhi ya sehemu zakombolewa

Hayo yalikuwa ni maafa makubwa kwa upande wa vikosi vya serikali ya Ukraine tokea ilipopoteza wanajeshi 18 wakati wa mapigano makali katika jimbo hilo hilo la Donetsk hapo Mei 22.

Waziri wa Ulinzi wa Ukraine Mykhailo Koval amesema leo hii kwamba vikosi vyake vimekombowa baadhi ya sehemu zenye uasi mashariki mwa nchi hiyo kutoka kwa waasi ambao wamekuwa wakiendesha mapambano yenye maafa tokea mwezi wa Aprili.

Waziri huyo amewaambia waandishi wa habari kwamba vikosi vyao vya ulinzi vimekamilisha suhughuli yao na kuzikombowa kabisa sehemu za kusini na magharibi za Donetsk na kaskazini mwa Luhansk kutoka kwa waasi

Urusi yapenyeza wapiganaji Ukraine

Waasi wakiwa na silaha nzito katika mji wa Donetsk.

Waasi wakiwa na silaha nzito katika mji wa Donetsk.

Mojawapo ya viongozi wa waasi hapo jana alitowa taarifa za kushangaza kwa kukiri kwamba waasi 33 kati ya zaidi ya 40 waliouwawa wakati wa shambulio kwenye uwanja wa ndege wa Donetsk wiki hii walikuwa ni raia wa Urusi kutoka maeneo ya Waislamu kama vile Chechnya

Kufichuka kwa taarifa hizo kunapingana na kauli ya Rais Vladimir Putin wa Urusi ya kukataa kuhusika kwa Urusi na harakati za waasi na hiyo kuunga mkono madai ya serikali ya Ukraine kwamba waasi hao hawawakilishi matakwa halisi ya wafanyakazi wa migodi na viwanda vya chuma waliolifanya eneo la mashariki la nchi hiyo kuwa engini ya uchumi wa Ukraine.

Waziri wa mambo ya nje wa Marekani John Kerry amesema hapo jana kuna ushahidi kwamba Warusi wamekuwa wakiwavusha na kuwaingiza Ukraine watu waliopatiwa mafunzo Urusi kutoka Chechnya ambapo wanakwenda kukoroga mambo kwa kujihusisha katika mapigano.

Taariza za hivi punde zinasema kwamba waangalizi wa kiraia kutoka Shirika la Usalama na Ushirikiano barani Ulaya OSCE waliokuwa wakishikiliwa mateka na wanamgambo wanaoiunga mkono Urusi mashariki mwa Ukraine wameachiliwa huru.

Hata hivyo habari hizo hazikuweza kuthibitishwa mara moja na shirika la OSCE.

Mwandishi : Mohamed Dahman/AFP/dpa

Mhariri: Yusuf Saumu

Matangazo

Unaweza kusikiliza matangazo yetu hapa

Kusikiliza matangazo ya Idhaa ya Kiswahili ya DW, tafadhali bonyeza alama ya spika ya masikioni hapo chini, na kuwasiliana nasi, tafadhali tuandikie moja kwa moja kupitia: kiswahili@dw.com