Waasi wadungua helikopta Syria | Matukio ya Kisiasa | DW | 20.09.2012
  1. Inhalt
  2. Navigation
  3. Weitere Inhalte
  4. Metanavigation
  5. Suche
  6. Choose from 30 Languages
Matangazo

Matukio ya Kisiasa

Waasi wadungua helikopta Syria

Wapiganaji waasi wameidungua helikopta katika mji wa mapambano karibu na Damascus leo hii wakati upinzani nchini Syria ukitangaza sehemu za mji mkuu huo kuwa eneo la maafa huku matumaini ya amani yakizidi kufifia.

Mapigano Syria.

Mapigano Syria.

Mirupuko kadhaa iliutikisa mji wa Douma ulioko kaskazini mashariki ya Damascus muda mfupi kabla ya waasi kuiangusha helikopta.Kwa mujibu wa Shirika la Haki za Binaadamu nchini Syria lenye makao yake mjini London helikopta hiyo imeanguka katika eneo la Tall al-Kurdi karibu na Douma na kwamba imedunguliwa na waasi kufuatia miripuko katika mji huo.

Televisheni ya taifa nchini Syria na shirika la habari la serikali SANA vimesema tu helikopta moja imeanguka.

Taarifa hizi zinakuja wakati Baraza la Taifa la Syria likisema kwamba Damascus kusini ni eneo la maafa wakati jeshi likishambulia kwa mizinga eneo la Al-Hajar Al- Aswad na kambi ya wakimbizi wa Kipalestina ya Yarmuk.

Baraza hilo ambalo ni kundi kuu la upinzani nchini Syria limesema kwamba helikopta za kivita zimekuwa zikishambulia nyumba za raia huko Al-Hajar Al- Aswad, Damascus ya kusini kwa kutumia maroketi yaliopachikwa mabomu.

Rais Bashar al-Assad wa Syria akimkaribisha mjini Damascus Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran Ali Akbar Salehi(September 19, 2012)

Rais Bashar al-Assad wa Syria akimkaribisha mjini Damascus Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran Ali Akbar Salehi(September 19, 2012)

Baraza hilo limeongeza kusema kwamba watu wengi wameuwawa au kujeruhiwa lakini inakuwa vigumu kwa wanaharakati kuorodhesha majina ya wahanga kutokana na mashambulizi hayo.Imeripotiwa kwamba hapo jana watu 12 wameuwawa katika wilaya mbili za kusini.

Shirika la Haki za Binaadamu la Syria limesema kwamba watu wengi pia wameuwawa na kujeruhiwa katika mji mkuu wa kibiashara nchini Syria wa Aleppo ulioko kaskazini mwa nchi hiyo kutokana na mashambulizi makubwa ya mizinga ya jeshi la serikali ingawa haina habari juu ya idadi halisi ya watu waliopoteza maisha yao.

Shirika hilo linasema watu 125 wameuwawa nchini kote Syria hapo jana wakiwemo raia 80,waasi 17 na wanajeshi 28 .

Kwa upande mwengine mjumbe mpya wa Umoja wa Mataifa kwa masuala ya watoto walioko kwenye mizozo Leila Zerrougui amesema Umoja wa Mataifa unayachunguza makundi ya waasi na vikosi vya serikali kwa mashambulizi ambayo yameuwa watoto.

Hapo jana Shirika la Kimataifa la Kutetea Haki za Binaadamu Amnesty Internatiaonal limesema kwamba mashambulizi ya vikosi vya serikali yamekuwa yakiuwa ovyo raia.

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Ban Ki-moon akiwa na mjumbe wa Umoja wa Mataifa na Umoja wa Nchi za Kiarabu kwa suala la Syria Lakhdar Brahimi.

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Ban Ki-moon akiwa na mjumbe wa Umoja wa Mataifa na Umoja wa Nchi za Kiarabu kwa suala la Syria Lakhdar Brahimi.

Wakati huo huo Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Ban Ki- moon ameonya kwamba inaonekana serikali ya Syria na waasi wameazimia kupambana hadi mwisho na kuona kwamba mzozo wao huo wa uasi wa miezi 18 dhidi ya utawala wa Rais Bashar al Assad unatatuliwa kijeshi.

Akizungumza na waandishi wa habari Ban amesema hadhani hatua za kijeshi zitaweza kuutatua mzozo huo na ametowa wito wa kufanyika mazungumzo ya kisiasa yenye kuwakilisha matakwa ya dhati ya wananchi wa Syria.

Ban amesema suala la mzozo huo litakuwa juu katika agenda wakati wa Mkutano wa wiki ijayo wa Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa wa viongozi wa dunia juu ya kwamba hakuna mkutano rasmi juu ya Syria na kwamba huenda Umoja wa Mataifa ukapendekeza mkakati mpya wa amani kwa Syria.

Mwandishi: Mohamed Dahman/AFP

Mhariri:Mohammed Abdul-Rahman

Matangazo

Unaweza kusikiliza matangazo yetu hapa

Kusikiliza matangazo ya Idhaa ya Kiswahili ya DW, tafadhali bonyeza alama ya spika ya masikioni hapo chini, na kuwasiliana nasi, tafadhali tuandikie moja kwa moja kupitia: kiswahili@dw.com