Waasi wadai kusonga mbele | Matukio ya Afrika | DW | 12.08.2011
  1. Inhalt
  2. Navigation
  3. Weitere Inhalte
  4. Metanavigation
  5. Suche
  6. Choose from 30 Languages

Matukio ya Afrika

Waasi wadai kusonga mbele

Waasi nchini Libya wanadai wamefanikiwa kuidhibiti sehemu ya mji wa mafuta wa Brega wakati majeshi yao hivi sasa yakiendelea kusonga kuelekea mji mwingine wa Zawiyah, kujaribu kuujongelea mji mkuu wa nchi hiyo Tripoli.

default

Mpiganaji muasi akiwa mstari wa mbele

Kiongozi wa Libya kanali Muammar Gaddafi ameendelea kung'ang'nia madaraka pamoja na kuendelea kwa kampeni ya anga ya Umoja wa Kujihami-NATO, vikwazo vya kiuchumi na vita vya muda mrefu na waasi wakijaribu kuufikisha kikomo utawala wake wa miaka 41.

Waasi wametapakaa sehemu kubwa ya nchi hiyo ya Afrika ya Kaskazini, lakini wanakabiliwa na changamoto kadhaa ikiwemo ya mgawanyiko miongoni mwao na kutokuwa na uzoefu.

Beerdigung FLAG Benghazi Libyen 07.05.2011

Waasi wakishambulia

Msemaji mmoja wa waasi amenukuliwa na Shirika la Habari la Uingereza-Reuters akisema wamefanikiwa kulidhibiti eneo la makazi ya watu la Brega lakini wanajeshi wa Gaddafi bado wanalimiliki eneo la magharibi la mji huo ambalo ndilo lenye hazina ya mafuta.

Msemaji huyo Mossa Mahmoud al-Mograbi alisema" Limekombolewa na lipo katika himaya yetu sasa" alikuwa akizungumzia upande wa mashariki wa mji huo.

Eneo la makazi ambalo mapigano hayo yalikuwa yakifanyika, lipo umbali wa kilometa 15 mashariki mwa eneo la mafuta na bandari. Lakini haikuwa rais kwa mwandishi wa reuters kuthibitisha taarifa hizo na waasi wamekuwa wakirudiarudia kauli ya kwamba wanadhibiti baadhi ya miji.

Katika eneo la milimani waasi wanasema wamefika kijiji cha Bir Shuaib kiasi cha kilometa 25 kutoka Zawiyah. Eneo hilo walilikaribia mara mbili tofauti kabla ya kukabiliana na upinzani kutoka majeshi ya Gaddafi.

Kijiographia eneo hilo lipo umbali wa kilometa 50 kutoka Tripoli, katika barabara kuu ya kuelekea nchi jirani ya Tunisia. Mpiganaji muasi alisema tayari wamekipita kijiji cha Nasr na kwamba hivi sasa wapo umbali wa kilometa 25 kutoka Zawiyah.

Hata hivyo waasi wamewazuia waandishi wa habari wasifike eneo la mapigano kwenda kujionea wenyewe.

Kwa ujumla waasi katika maeneo ya milima ya magharibi, hawafanikishi mapigano hayo kwa umoja, kila mji una kikosi chake. ingawa wakati mwingine wanaungakana katika kufanikisha operesheni kubwa.

Katika hatua nyingine Rais Dmitry Medvedev amesaini makubaliano ya kuongeza makali ya vikwazo dhidi ya Libya ikiwa ni miezi mitano baada ya kupitishwa na Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa. Vikwazo hivyo vipo katika azimio namba 1973 la umoja huo.

Mwandishi: Sudi Mnette/RTR/AFP
Mhariri:Josephat Charo

DW inapendekeza