Waasi wa zamani Sierra Leone hatiani. | Wafanyakazi wa Idhaa ya Kiswahili | DW | 26.02.2009
 1. Inhalt
 2. Navigation
 3. Weitere Inhalte
 4. Metanavigation
 5. Suche
 6. Choose from 30 Languages

Timu Yetu

Waasi wa zamani Sierra Leone hatiani.

Watu watatu wamepatikana na hatia ya kutenda uhalifu wa kivita na uhalifu dhidi ya ubinadamu nchini Sierra Leone.

default

Waasi wa zamani wa Sierra Leone Augustine Gbao kushoto na Issa Hassan Sesay wakiwa mahakamani.

Watu hao waliokuwa waasi wametiwa hatiani kwenye mahakama inayopambana na uhalifu wa kivita inayoungwa mkono na Umoja wa Mataifa.


Mahakama hiyo imethibitisha kwamba watu hao walitenda uhalifu huo wakati wa vita vya wenyewe kwa wenyewe nchini Sierra Leone vilivyochukuwa muda wa miaka 10.

Wahalifu hao Issa Sesay, Morris Kallon na Augustine Gbao wa kundi la waasi lililokuwa linaitwa Revolutinary United Front walipatikana na hatia ya kuamrisha mauaji , vitendo vya ubakaji na kuwakatakata watu viungo vya mwili wakati wa vita vya nchini Sierra Leone vilivyomalizika mnamo mwaka 2001.

Juu ya hukumu iliyotolewa Mwendesha mashtaka wa mahakama inayoungwa mkono na Umoja wa Mataifa, Stephen Rapp amesema.

´´Uamuzi wa mahakimu umetilia maanani mateso yaliyowakabili watu wengi,waliokatwa katwa viungo vya miili yao ,waliogeuzwa watumwa,waliobakwa , waliouliwa na waliopoteza makao yao na kuwa maskini."

Washtakiwa hao watatu walikabiliwa na mashtaka 18.Wawili kati yao Sesay na Kallon walipatikana na hatia katika mashtaka 16 kati ya hayo 18. na mwengine Gbao alipatikana na hatia katika mashtaka 14.

Hakimu alimsomea Issa Sesay uamuzi wa mahakama kwa kusema.

´´Umepatikana na hatia ya kuua kwa kudhamiria na kwa kushiriki pamoja wengine katika matendo ya kihalifu.

Ulitenda uhalifu huo katika mazingira ya mgogoro wa kivita."

Mshtakiwa mwengine Gbao alipatikana na hatia katika mashtaka 14 ikiwa pamoja na ya mauaji,ubakaji,ukatili,kuwatumiwa watoto kama askari na kuwashambulia askari wa Umoja wa Mataifa wakati wa vita.

Hadi vita vilipomalizika nchini Sierra Leone watu laki moja na alfu 20 walikuwa wameuliwa na maalfu wengine walikatwa katwa sehemu za miili yao kama, pua masikio ,miguu na mikono.

Adhabu za watu zitatolewa mbalimbali katika wiki zijazo.

Hatahivyo mahakama ya Sierra Leone inayoungwa na Umoja wa Mataifa haina adhabu ya kifo na wala haina adhabu ya juu kabisa. Adhabu ya juu kabisa iliyowahi kutolewa na mahakama hiyo hadi sasa ni kifungo cha miaka 50.

Hukumu iliyotolewa kwa wahalifu hao watatu imeshangiliwa na watu wengi waliokuwa wahanga wa uhalifu wa kivita.

Mtu mmojaamesema, kuwa ingawa hajui ni adhabu gani watapewa wahalifu hao, ameridhika kwamba kwanza wamepatikana na hatia.

Mashirika ya kutetea haki za binadamu pia yameunga mkono uamuzi wa mahakama.

Shirika la kutetea haki za binadamu Amnesty International limesema kuwa hukumu zilizotolewa ni ujumbe kwa wote wanaotenda uhalifu kwamba hawataweza kuendelea kutenda uhalifu huo bila ya kuadhibiwa.

Vita vya wenyewe kwa wenyewe nchini Sierra Leone vilikuwa vya kupigania udhibiti wa migodi ya almasi. Washtakiwa walishirikiana na aliekuwa rais wa Liberia Charles Taylor katika njama hizo za kihalifu.

 • Tarehe 26.02.2009
 • Mwandishi Abdul Mtullya
 • Chapisha Chapisha ukurasa huu
 • Kiungo https://p.dw.com/p/H1YX
 • Tarehe 26.02.2009
 • Mwandishi Abdul Mtullya
 • Chapisha Chapisha ukurasa huu
 • Kiungo https://p.dw.com/p/H1YX
Matangazo

Sikiliza Matangazo Yetu

Unaweza kusikiliza matangazo yetu hapa

Kusikiliza matangazo ya Idhaa ya Kiswahili ya DW, tafadhali bonyeza alama ya spika ya masikioni hapo chini, na kuwasiliana nasi, tafadhali tuandikie moja kwa moja kupitia: kiswahili@dw.com