1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Waasi wa Libya wailaumu NATO kuwaacha mkono

6 Aprili 2011

Waasi wa Libya wanalalamika kukosa usaidizi wa kutosha kutoka Jumuiya ya Kujihami ya NATO, ambayo imechukua rasmi uongozi wa operesheni ya marufuku ya anga dhidi ya vikosi vya Muammar Gaddafi na pia kuwalinda raia.

https://p.dw.com/p/10o8G
Waasi wa Gaddafi mjini Misrata
Waasi wa Gaddafi mjini MisrataPicha: dapd

Yalipoanza mashambulizi ya angani kutoka vikosi vya Majeshi ya Ushirika, yaliyoongozwa na Marekani wiki mbili zilizopita, vikosi vya waasi vilipata fursa ya kusonga mbele kutoka mashariki kuelekea magharibi na hata kujenga matumaini kwamba hivi punde wangeliingia Tripoli kumng'oa Muammar Gaddafi.

Lakini sasa, waasi hao wanaonekana kuvunjika moyo, baada ya mashambulizi hayo kusita kwa siku chache tu, na vikosi vya Gaddafi kuwarudisha nyuma, kutoka mji wa Brega hadi Misrata na sasa wanapigania kuunusuru mji wa Ajdabiya.

Hata hivyo, msemaji wa NATO, Carmen Romero, ameliambia shirika la habari la AFP hivi leo kwamba bado vikosi vyake vinaendelea na jukumu lake la kuwalinda raia.

"Misrata ni kipaumbele chetu cha mwanzo. Tuna idhini ya kuwalinda raia na sisi tutatimiza wajibu wetu." Amesema Romero.

Hapo Jumatatu (04.04.2011) ndege za NATO ziliyashambulia makambi ya kijeshi ya Gaddafi yaliyoko Misrata na kwamba hadi sasa karibu asilimia 30 ya nguvu za kijeshi za utawala huo zimeshaharibiwa.

Waasi wapata mafunzo ya kijeshi

Waziri wa Mambo ya Nje wa serikali ya waasi wa Libya, Ali al-Essawi
Waziri wa Mambo ya Nje wa serikali ya waasi wa Libya, Ali al-EssawiPicha: dapd

Ingawa hakuna taarifa za waziwazi kutoka NATO na washirika wengine wa Kimagharibi, habari zinasema kuwa baadhi ya nchi za Magharibi zimekuwa zikiwapa waasi wa Libya mafunzo mafupi ya kijeshi, katika jitihada za kuwafanya wawe na uwezo wa kukabiliana na vikosi vya Gaddafi.

Mmoja wa walimu wa mafunzo hayo, Sidik, ambaye ni mwanajeshi mstaafu kutoka jeshi la Gaddafi, anasema kuwa mafunzo haya yanawasaidia sana kujenga moyo wa wapiganaji wao.

"´Kwa jina la Mungu, mafunzo haya ni mazuri sana kwao. Hapo kabla wengi wao walikuwa wamekaa kwenye viti hawana la kufanya. Ulipokuja wito wa kujiunga na jeshi, wote wakakimblia huku wakiwa hawana ujuzi wowote. Wengi wao walikuwa hawajui hata kushika silaha, lakini baada ya siku saba watakuwa tayari." Anasema Sidik.

Nchi za Kiarabu zajiunga na operesheni dhidi ya Gaddafi

Kiongozi wa serikali ya waasi wa Libya, Mustafa Abdul Jalil
Kiongozi wa serikali ya waasi wa Libya, Mustafa Abdul JalilPicha: picture alliance/dpa

Wakati huo huo, Jordan imetuma ndege zake za kijeshi kusaidia huduma za kibinaadamu nchini Libya, ikiwa ni sehemu ya kampeni ya kimataifa dhidi ya utawala wa Gaddafi. Waziri wa Mambo ya Nje wa nchi hiyo, Nasser Judeh, amesema kuwa ndege za jeshi la nchi yake zimetua Libya tangu siku mbili zilizopita, katika mji wa Benghazi.

Judeh amekataa kuthibitisha idadi ya ndege hizo, lakini inafahamika kuwa Jordan ilikubali kutoa msaada wa kibinaadamu na kifedha katika operesheni hii ambayo sasa inaongozwa na NATO.

Qatar ilikuwa nchi ya mwanzo ya Kiarabu kutuma ndege zake za kijeshi, kuongeza nguvu kwenye operesheni ya kuzuia ndege kuruka kwenye anga ya Libya.

Alhamisi iliyopita, msemaji wa vikosi vya Ufaransa, nchi ambayo ilionekana kushadidia operesheni hii, alisema kuwa Umoja wa Falme za Kiarabu wa Imarat, ulituma pia ndege zake na sasa ziko kwenye kituo cha kijeshi cha Sardinia tayari kushiriki operesheni za kuwalinda raia dhidi ya mashambulizi ya vikosi vya Gaddafi.

Mwandishi: Mohammed Khelef/Reuters/AFP
Mhariri: Othman Miraji

Ruka sehemu inayofuata Gundua zaidi