1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Waasi wa Kiislamu Nigeria wavamia vituo vya polisi

Kabogo Grace Patricia27 Julai 2009

Uvamizi huo uliotokea mapema leo asubuhi katika vituo vya polisi kwenye majimbo ya Yobe na Borno, umesababisha kifo cha mtu mmoja.

https://p.dw.com/p/Iy2t
Watu wakiangalia gari lililoungua moto katika kituo cha polisi cha Okoro Obio, Port Harcourt, Nigeria, 2007, baada ya mtu mwenye silaha kuvamia kituo hicho na kusababisha vifo vya watu saba.Picha: AP

Waasi wa Kiislamu wamevamia vituo vya polisi nchini Nigeria katika majimbo mawili ya kaskazini-mashariki mwa nchi hiyo na kumuua askari mmoja wa kikosi cha zimamoto, ikiwa ni siku moja baada ya watu zaidi ya 50 kuuawa katika gahsia kwenye jimbo la Bauchi.

Askari huyo wa zima moto ameuawa mapema leo asubuhi baada ya wapiganaji hao wanaotaka kuanzishwa kwa sheria ya Kiislamu ya Sharia, kuchoma moto kituo cha polisi cha Potiskum kilichopo kwenye jimbo la Yobe. katika shambulio hilo, askari polisi wanne wamejeruhiwa. Katika jimbo jirani la Borno, waasi wanaosadikiwa kuwa wafuasi wa kundi dogo la Kiislamu la Boko Haram, wameshambulia kituo cha polisi katika mji mkuu wa jimbo la Maiduguri, ingawa bado haijafahamika kama kuna majeruhi wowote. Ghasia hizo hazihusiani na mzozo uliopo katika eneo la mafuta la Niger Delta.

Kundi la Boko Haram, ambalo wakati mwingine linaitwa Wataliban wa Nigeria, linalotaka kuanzishwa kwa Sheria ya Kiislamu katika nchi hiyo, lilianza kufanya mashambulio yake kaskazini-mashariki mwa mji wa Bauchi mapema jana Jumapili ikiwa ni katika kulipiza kisasi kufuatia kukamatwa kwa viongozi wao. Zaidi ya watu 50 waliuawa katika mashambulio hayo na kusababisha ganava wa jimbo la Bauchi kutangaza amri ya kutotembea usiku. Aidha, Polisi walifanikiwa kuwakamata zaidi wa watu 100 kufuatia tukio hilo. Hata hivyo, kundi hilo la Boko Haram halina uhusiano na kundi jingine la waasi nchini Nigeria la Movement for the Emancipation of the Niger Delta (MEND).

Bauchi, Yobe na Borno ni miongoni mwa majimbo 12 ya Nigeria kati ya 36 yaliyoanza kufuata Sheria ya Kiislamu tangu mwaka 2000, hatua iliyosababisha mfarakano mkubwa baina ya Wakristo wachache na Waislamu, hivyo kusababisha mapigano ya kidini yaliyopoteza maisha ya maelfu ya watu.

Zaidi ya makabila 200 yanaishi kwa amani katika nchi hiyo ya Afrika Magharibi, ingawa vita vya wenyewe kwa wenyewe vya mwaka 1967 na 1970 vimesababisha vifo vya watu milioni moja na tangu wakati huo kumekuwa na mifarakano ya kidini. Ghasia za mwezi Februari, mwaka huu katika jimbo la Bauchi zilisababisha vifo vya watu 11 na wengine kadhaa kujeruhiwa, ambapo pia makanisa na misikiti kadhaa ilichomwa moto. Aidha, mwezi Novemba, mwaka uliopita, mamia ya watu waliuawa katika mapigano ya siku mbili katika mji wa Jos baada ya kutokea malalamiko katika matokeo ya uchaguzi.

Mwandishi: Grace Patricia Kabogo (RTRE/DPAE)

Mhariri: M.Abdul-Rahman