1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Waasi wa ADF wawaachia huru mateka 22

Amina Mjahid
6 Machi 2019

Waasi wa kundi la ADF la nchini Uganda, wanaoendesha harakati zao katika misitu ya wilaya ya Beni katika Jamhuri ya Kidemokrasi ya Congo, wamewaachia huru mateka 22.

https://p.dw.com/p/3EX9b
DR Kongo Alltagsleben in Beni in der nähe von dem Kreisverkehr Nyamwissi
Picha: DW/W. Bashi

Mateka waliochukuliwa kutoka vijiji mbalimbali vya wilaya ya Beni walikuwa wakitumiwa na wapiganaji wa ADF kusafirisha bidhaa walizopora na kulima mashamba yao.

Wakaazi wa mji huo walijawa na furaha, yakuwaona ndugu zao waliotekwa nyara na ADF wakiaachiwa huru wakiwa hai. Kwa kawaida, waasi hao huwa wanawauwa mateka wao baada ya kuwatumia kama wachukuzi, au kuwaorodhesha katika kundi lao na kuwafanya kuwa wapiganaji.

Kuachiwa huru kwa mateka ishirini na mbili sio jambo la kawaida kwani, ni wengi ambao wameshapoteza maisha katika misitu wanamoishi waasi wa Uganda ADF katika wilaya ya Beni, na wengine kusajiliwa katika kundi hilo la uasi.

Demorkatische Republik Kongo - Soldaten der Democratic Republic of Congo nach Kämpfen mit Rebellen
Baadhi ya wanajeshi wa serikali ya Congo wanaopambana na waasi wa ADF Picha: Reuters/G. Tomsaevic

Akizungumza na wanahabari katika mji mdogo wa Eringeti walikowasili mateka wa ADF, baada ya kusindikizwa na wapiganaji wa kundi hilo hadi eneo linaloitwa Mayisafi, mashariki mwa Eringeti, Mjumbe maalumu wa gavana wa mkoa wa Kivu ya kaskazini Eringeri Njiamoja Sabiti aliwahimiza wanajeshi wa Kongo kuwatokomeza waasi hao.

"Taarifa nzuri ni kurudi nyumbani kwa ndugu zetu, marafiki zetu wa Kithevya, Kengele, Apetina na Mamove,waliotekwanyara na ADF. Tunaomba kwa wanajeshi wetu kuchukuwa majukumu yao ilikutokomeza vitendo vya kundi hili la waasi."

Nao baadhi ya mateka wa ADF walioachiwa huru waliiambia DW, kuwa katika misitu wanakojihifadhi ADF, walikuwa wanaishi katika magereza ya ardhini, na kwamba katika magereza hayo, wanaume wanateremshwa ndani kwakutumia kamba, na wanawake wanatumia ngazi ilikuteremka katika gereza.

Waasi wa Uganda ADF, wanashukiwa kuwauwa watu zaidi ya elfu mbili katika mji na wilaya ya Beni, tangu yalipoanza mauwaji hayo katika eneo hili oktoba Mwaka wa 2014.

Majeshi ya serikali pamoja na yale ya Umoja wa mataifa kupitia kikosi maalumu cha kuingilia kati FIB, yamekuwa ya kipambana na waasi hao bila ya kuwatokomeza. Dua ya wakaazi kila uchao nikuona waasi hao wanatokomezwa, jambo litakalowapelekea wengi kurudi katika mashamba yao na kuondokana na maisha ya ukimbizi.

Mwandishi: John Kanyunyu DW Beni

Mhariri: Iddi Ssessanga