Waasi wa ADF waushambulia mji wa Beni | Matukio ya Afrika | DW | 23.12.2018
  1. Inhalt
  2. Navigation
  3. Weitere Inhalte
  4. Metanavigation
  5. Suche
  6. Choose from 30 Languages
Matangazo

Matukio ya Afrika

Waasi wa ADF waushambulia mji wa Beni

Kundi la waasi wa Uganda la ADF limeushambulia mji wa Beni nchini Congo na kusababisha vifo vya watu wanane na kupora mifugo. Watu wengine watatu wamejeruhiwa.

Asubuhi ya tarehe 23.12.18 katika kata ya Boikene, waasi wa Uganda ADF waliwauwa watu zaidi ya watano na kuiba mifugo pamoja na kuwachukuwa watu wengine mateka. Shambulio la Usiku wakuamkia Jumapili ya leo, lilitarajiwa kwani palikuwepo na fununu kuwa ADF wataushambulia mji wa Beni Desemba 23, ili kuvuruga shughuli za uchaguzi katika mji huu.

Kuahirishwa kwa uchaguzi huo kulidhaniwa na wengi kuwa ADF hawataushambulia tena mji huu, lakini kwa bahati mbaya Beni ikashambuliwa milango ya saa mbili usiku.

Shambulio hilo limelaaniwa na mwenyekiti wa mashirika ya kiraia katika mji wa Beni Kizito Bin Hangi, anayeomba majeshi ya serikali pamoja na yale ya Umoja wa Mataifa kuhakikisha wanaimarisha usalama katika eneo hili, ili siku ya uchaguzi ambayo sasa imepangiwa kufanyika Desemba 30, wakaazi wa Beni wasihofie maisha yao, na kutokwenda kupiga kura.

Soldaten der FARDC in der Nähe von Beni Kongo im Einsatz gegen Islamisten aus UgandaJanuar 2014 (Getty Images/AFP/Alain Wandimoyi)

Baadhi ya vikosi vya serikali ya Jamhuri ya Kidemokrasi ya Congo mjini Beni

Hata hivyo kuna habari ambazo hazijathibitishwa kwamba vijana wa kata ya Boikene iliyoshambuliwa na ADF, wataandamana kupinga mauwaji ya wenzao, na endapo maandamano hayo yatafanyika, huenda yakavuruga hali ya utulivu ilioko Beni kwa wakati huu.

Wale walioshuhudia shambulizi hilo wanasema watu wengine watatu walijeruhiwa katka shambulizi la leo asubuhi na walikuwa wanapata matibabu katika hospitali moja mjini Beni. Kundi la ADF ambalo limekuwa likifanya operesheni zake tangu mwaka 1995 limedaiwa kuendelea kufanya mashambulizi na mauaji ya wengi tangu mwaka 2014.

Kando na mashambulizi ya ADF eneo hilo la mpakani pia limekumbwa na mkurupuko wa ugonjwa hatari wa Ebola ambao hadi sasa umesababisha vifo vya watu 347 tangu mwezi wa Agosti hii ikiwa ni kwa mujibu wa utafiti wa hivi karibuni uliofanywa na wizara ya afya siku ya Jumamosi.

Mwandishi: John Kanyunyu DW Beni

Mahriri: Iddi Ssessanga