1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Waasi Syria wateka mji muhimu

30 Machi 2013

Waasi nchini Syria wameteka mji muhimu uliyoko katika barabara kuu inayounganisha mji wa Damascus na maeneo ya kusini mwa nchi hiyo, katika mafanikio yao ya hivi karibuni mkoani Daraa, katika mpaka na Jordan.

https://p.dw.com/p/1875M
Wapiganaji wa Jeshi Huru la Syria wakipambana na wanajeshi wa serikali.
Wapiganaji wa Jeshi Huru la Syria wakipambana na wanajeshi wa serikali.Picha: picture-alliance/AP

Wakitumia uingiaji wa silaha kama mtaji, waasi hao wanaanzisha vita vya kimkakati kuchukua eneo la kusini mwa Syria, na wanatafuta udhibiti wa njia kuu kutoka mpaka wa Jordan kuelekea mji wa Damascus, katika kujiandaa na mapambano ya mwisho dhidi ya mji wa huo, ambao ndiyo makao makuu ya serikali ya rais Bashar al-Assad. Ijumaa waasi walisherehekea ushindi wao wa hivi karibuni, kwa kuchukua udhibiti kamili wa mji wa Dael, baada ya wanajeshi watiifu kwa utawala wa Assad kuondoka wote kutoka mji huo.

Wanajeshi wa jeshi la Syria katika mapambano.
Wanajeshi wa jeshi la Syria katika mapambano.Picha: AFP/Getty Images

"Mungu ni mkubwa! Tunakuja Bashar!" walisema wapiganaji usiku wa Alhamis, baada ya kuteka kizuizi cha mwisho cha kijeshi katika mji huo ambako wanajeshi wa Assad walikuwa wamezingirwa, kwa mujibu wa mkanda wa video uliyowekwa kwenye mtandao. Dael ni moja ya miji mikubwa zaidi katika mkoa wa kusini wa Daraa, ambako uasi dhidi ya rais Assad ulianzia Machi 2011, baada ya vikosi vya usalama kuwakamata wanafunzi waliokuwa wanachora kwenye ukuta michoro ya kuipinga serikali.

Wanaharakati wanasema ni katika mji wa Dael, ambako sanamu ya kwanza ya babake Assad na mtangulizi wake, marehemu Hafez Assad, iliangushwa baada ya maandamano kuripuka. Utawala ulijibu kwa kutumia ukandamizaji uiliyokithiri wa kijeshi katika eneo hilo, na ulifanikiwa kuzima uasi huko wakati vikosi vya serikali vilipogeuzia usikivu wake kulinda mikoa ya mashariki na kaskazini dhidi ya waasi waliokuwa wanasonga mbele, wakati maandamano yakigeuka kuwa vita vya wenyewe kwa wenyewe, ambako watu wapatao 70,000 wameuawa.

Lakini katika miji ya kilimo yenye vumbi na katika vijiji mkoani humo, waasi wamezidisha mashambulizi, na kupanua uwepo wao na kuwa na hisia mpya za malengo. Miongoni mwa waasi hao pia wamo wapiganaji wenye msimamo mkali wa dini. Mkoa huo muhimu, maarufu kama viwanja vya Houran, ambao unaanzia katika viunga vya mji mkuu kusini kuelekea Jordan, unatizamwa kama nji muhimu kuelekea katika zawadi ya mwisho, ambayo ni mji wa Damascus.

Rais Bashar al-Assad.
Rais Bashar al-Assad.Picha: Reuters

Upatikanaji wa hivi karibuni wa silaha unaonekana kufanya lengo hilo kutimizika zaidi kuliko ilivyokuwa huko nyuma. Ingawa waasi wanadhibiti maeneo makubwa kaskazini mwa Syria karibu na mpaka wa nchi hiyo na Uturuki, mpaka wa Jordan uko umbali wa kilomita 100 tu kutoka Damascus, au theluthi moja ya umbali kwenda Uturuki huko kaskazini, ambako wapiganaji wanadhibiti maeneo makubwa.

Njia kuelekea Damascus

Waasi wameweka kambi katika viunga kadhaa vya mji wa Damascus lakini wamefanikiwa kuingia katika maeneo machache kusini na kaskazini mwa mji huo mkuu. Wapiganaji wanasema wanajaribu kutengeneza nji kutokea Jordan kwenda Damascus. katika wiki za hivi karibuni, wamepata mafanikio muhimu katika mikoa ya kusini ya Daraa na Quneitra inayopakana na Jordan na Israel, wakiteka miji na vijiji karibu na eneo la kusitisha mapigano kati ya Israel na Syria, na katika milima ya Golani na kwenye barabara kuu inayoiunganisha Damascus na Jordan.

Pia wameteka vituo kadhaa vya ukaguzi wa kijeshi, wakisafisha eneo lenye umbali wa kilomita 25 katika mpaka wa Syria na Jordan. Wiki iliyopita waasi waliteka kituo muhimu cha kijeshi karibu na kijiji cha Saida. Ni vigumu kujua ukubwa wa eneo linalodhibitiwa na waasi kwa sasa. Wanaharakati wanasema kuwa katika miji mingi na vijiji, vikosi vya serikali vinaendeleza uwepo wa kiishara kupitia vituo vidogo vya kijeshi na vya ukaguzi, ambavyo vinashambuliwa mara kwa mara. Mapigano yanatokea kila siku katika maeneo kama vile Tafas, Sheikh Maskin na Izraa yaliyoko katika barabara hiyo.

Siku ya Ijumaa vikosi vya serikali viliondoka katika kituo cha mwisho cha ukaguzi mjini Dael, baada ya mashambulizi ya waasi yaliyodumu masaa 24. Mji wa Dael una wakaazi 40,000 na hivyo kuwa moja ya miji mikubwa zaidi katika mkoa, na una mashamba madogo madogo mengi ya kifamilia na uko umbali wa chini ya kilomita 15 kutoka mpaka wa Jordan katika mkoa wa Daraa. Mwanaharakati aliezungumza kwa masharti ya kutoandikwa jina lake kwa kuhofia kuchukuliwa hatua na serikali, alisema uwepo wa vikosi vya serikali katika mkoa huo unapungua kila siku.

Kiongozi wa Muungano wa upinzani, Ahmed Moaz al-Khatib.
Kiongozi wa Muungano wa upinzani, Ahmed Moaz al-Khatib.Picha: Reuters

Makundi yanayopigana mkoani Daraa

Brigedi za Ababil Houran na Al-Omari ni miongoni mwa makundi maarufu yanayoshiriki mapigano, pamoja na brigedi ya Mashahidi wa Yarmouk, ambayo ni kundi la wapiganaji wa Kiislamu liliwateka wafilipino 21, ambao ni wanajeshi wa kulinda amani wa Umoja wa Mataifa katika milima ya Golan. Video zilizowekwa kwenye mtandao ziliwaonyesha waasi katika mitaa ya Dael na miili ya wanajeshi wa serikali ikiwa chini. Ilionyesha pia wanawake wakishagilia na wapiganaji wakipiga kelele za "tunakuja Bashar."

Mfululizo wa mafanikio ya waasi unakwenda sambamba na kile maafisa wa kanda na wataalamu wa kijeshi wanachosema ni uingizaji wa shehena za silaha kwa upande wa waasi na serikali za mataifa ya kiarabu, kwa kushirikiana na Marekani, kwa matumaini ya kujianda na mapambano ya mwisho ya mji wa Damascus. Maafisa na wataalamu wa kijeshi wa mataifa ya magharibi waliiambia AFP, kuwa Jordan ilifungua njia ya kupitisha silaha mwishoni mwa mwaka uliyopita.

Wachambuzi wawili wa kijeshi wanaofuatilia usafirishaji huo kw akaribu, walisema silaha hizo zinahusisha bunduki na maroketi yenye nguvu zaidi ya kushambulia vifaru kutoka Croatia, ambazo waasi hawakuwa nazo hapo kabla. Elliot Higgins, mwingireza na Nic Jenzen-Jones kutoka Australia walisema zinahusisha silaha ndogo zinazorusha miripuko mikubwa aina ya M60, maroketi ya Osa aina ya M79, na silaha za kuripuwa gruneti aina ya RBG-6, ambazo zote ni silaha zenye nguvu za kushambulia vifaru.

Mwanaharakati wa Syria Maher Jamous anaetokea Dael lakini anaishi katika Falme za Kiarabu, alisema licha mafaniko wanayoendelea kupata waasi, utawala wa Syria bado una uwepo imara katika mkoa huo unaoelekea mji mkuu. Utawala huo ulipeleka wanajeshi wenye mafunzo ya hali ya juu katika mkoa huo, ambao wakati moja ulichukuliwa kama moja ya mikoa tiifu zaidi kwa utawala huo. Makamu wa rais Farouk al-Sharaa, naibu waziri wa mambo ya kigeni Faysal Mekdad, waziri wa mawasiliano Omran al-Zoubi na maafisa wengine wa ngazi ya juu wanatoka mkoani Daraa.

Wakimbizi wa Syria wakivuka mpaka kuingi nchini Jordan.
Wakimbizi wa Syria wakivuka mpaka kuingi nchini Jordan.Picha: AFP/Getty Images

Kanali Ahmad Fahd al-Naameh, kamanda wa baraza la kijeshi la vikosi vya kusini alisema mkakati wao ni kuidhibiti Daraa na Damascus, kwa sababu utawala utashindwa tu na kuangushwa mjini Damsacus. Katika mazungumzo na kituo cha televisheni cha Al-Arabiya, alikanusha kupokea silaha kupitia Jordan, na kusema kuwa silaha nyingi wanazotumia waliziteka baada ya kuteka vituo vya kijeshi, au zilinunuliwa na fedha za matajiri wa Syria.

Mapigano yaendelea kwengine

Katika mapigano mengine, shirika la uangalizi wa haki za binaadamu nchini Syria, lilisema kuwa mapigano makali yametokea kati ya vikosi vya serikali na wapiganaji wanaojaribu kuvamia upya kituo muhimu cha kijeshi katika mji wa kaskazini wa Raqqa, ambacho kilitekwa na waasi mwezi huu. Kituo hicho ndiyo ngome muhimu ya mwisho kwa utawala wa Assad katika mkoa huo wa kaskazini unaopakana na Uturuki.

Shirika hilo la uangalizi wa haki za binaadamu lilisema vikosi vya serikali vilishambulia viunga vya mji wa Damscus vya Adra, wakati televisheni ya Al-Akhbariyya ilisema majeshi ya serikali yaliuwa "magaidi" wengi katika eneo hilo lililoko karibu na gereza kuu la Syria. Kituo cha habari cha Aleppo na shirikala uangalizi wa haki za binaadamu pia viliripoti mapigano na mashambulizi ya helikopta karibu na uwanja wa ndege wa kimataifa wa Aleppo. Watu wasiopungua 15 waliuawa na wengine wengi kujeruhiwa, baada ya kombora kutua katika mji wa Hretan, mkoani Aleppo, kwa mujibu wa kamati ya wanaharakati ya uratibu katika eneo hilo, ambayo hata hivyo haikuweza kuthibitishwa.

Mwandishi: Iddi Ismail Ssessanga/ape,afpe
Mhariri: Amina Abubakar