Waangalizi wa UN chupuchupu Syria | Matukio ya Kisiasa | DW | 09.05.2012
  1. Inhalt
  2. Navigation
  3. Weitere Inhalte
  4. Metanavigation
  5. Suche
  6. Choose from 30 Languages
Matangazo

Matukio ya Kisiasa

Waangalizi wa UN chupuchupu Syria

Kiongozi wa timu ya waangalizi wa Umoja wa Mataifa nchini Syria aliponea chupuchupu kuuawa baada ya bomu kulipuka karibu kabisaa na msafara wake katika mkoa wa Daraa siku ya Jumatano.

Wanajeshi wa Syria wakilizunguka gari lililoharibiwa na mlipuko wa bomu mjini Daraa Mei 9.

Wanajeshi wa Syria wakilizunguka gari lililoharibiwa na mlipuko wa bomu mjini Daraa Mei 9.

Kwa mujibu wa msemaji wa timu hii ya wangalizi Neeraj Singh, askari sita wa jeshi la serikali ya Syria waliyokuwa wakisindikiza masafara huu walijeruhiwa katika mlipuko huo.

Singh ambaye alikuwa katika msafara huo, ameliambia shirika la habari la Ujerumani dpa kuwa mlipuko huo umetokea muda mfupi tu baada ya msafara wa Meja Jenerali Robert Mood kupita katika kizuizi cha kijeshi katika viunga vya Daraa.

Singh alimnukuu Mood akisema kuwa mlipuko huu ni mfano halisi wa kiwango cha vurugu ambazo amesema laazima zikomeshwe nchini Syria.

Haikuweza kubainika mara moja nani alikuwa nyuma ya mlipuko huu na Meja Jenerali Mood alisema hajui kama ulikuwa unalenga waagalizi au wanajeshi wa serikali lakini akasisitiza kuwa ni muhimu kuzingatia ukweli kuwa hiyo ndiyo hali wanayokabiliana nayo raia wa Syria kila siku.

Waasi wakanusha kuhusika
Jeshi la waasi la Free Syria limekanusha kuhusika na mlipuko huo lakini kiongozi wake Kanali Riad al-Assad alinukuliwa na gazeti la Asharq al-Awsat la Lebanon lakisema wataanza tena mashambulizi kwa kuwa serikali ya rais Assad imeshindwa kuheshimu makubaliano ya kusitisha mapigano.

Kiongozi wa timu ya Waangalizi Meja Jenerali Robert Mood.

Kiongozi wa timu ya Waangalizi Meja Jenerali Robert Mood.

Katika mahojiano na gazeti hilo yaliyochapishwa siku ya Jumatano, al-Assad alisema raia wa Syria wanawataka wawalinde lakini wachambuzi wanasema matamshi haya yanaweza kurudisha nyuma jitihada za Mjumbe wa Umoja wa Mataifa Koffi Annan kurejesha amani nchini humo.

Annan aonyesha mashaka
Tayari Annani ameonyesha wasiwasi juu ya mustakabali wa mpango wake aliposema jana kuwa:"Kuna wasiwasi mkubwa kwamba nchi hii inaweza kutumbukia katika vita vya wenyewe kwa wenywe na matokeo yake ukiyatafakkari yanatisha. Hatuwezi kuruhusu hilo kutokea. Kumekuwepo na kupungua kwa shughuli za kijeshi lakini kuna ukiukwaji mkubwa wa makubaliano ya kusitisha vurugu na viwango vya vurugu na unyanyasaji havikubaliki."

Wakati huo huo wanaharakati wa upinzani wameripoti kuwa mtu mmoja ameuawa na wengine watatu kujeruhiwa katika mapigano kati ya wanajeshi wa serikali na waasi katika mkoa wa kaskazini wa Idlib.

Katika mkoa wa Homs, taarifa zinasema kumekuwepo mfululizo wa mashambulizi katika eneo la Al-Rastan ambalo lilishuhudia mapigano makali kati ya vikosi vya serikali na waasi hapo jana.

Mjumbe maalum wa Umoja wa Mataifa Kofi Annan.

Mjumbe maalum wa Umoja wa Mataifa Kofi Annan.

Imekuwa vigumu kuthibitisha taarifa zinazotoka ndani ya Syria kwa kuwa serikali ya nchi hiyo ilipiga marufuku vyombo vya habari vya kimataifa kuingia katika maeneo mengi nchini humo tangu kuanza kwa harakati za kumung'oa rais Bashar al-Assad.

Shirika la habari la Lebanon limeripoti kuwa mwanamke mmoja raia wa nchi hiyo ameuawa katika shambulio la risasi kutoka upande wa Syria, haya yakiwa ni mauaji ya pili ya aina hii ndani ya mwezi mmoja. Serikali ya Syria ilisema huko nyuma kuwa majeshi yake yanawashambulia waasi wanaokimbilia nchini Lebanon.

Mwandishi: Iddi Ismail Ssessanga\DPAE\APE
Mhariri: Saum Yusuf

Matangazo

Unaweza kusikiliza matangazo yetu hapa

Kusikiliza matangazo ya Idhaa ya Kiswahili ya DW, tafadhali bonyeza alama ya spika ya masikioni hapo chini, na kuwasiliana nasi, tafadhali tuandikie moja kwa moja kupitia: kiswahili@dw.com