1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Waangalizi: Hatutaingilia taratibu za uchaguzi Uganda

11 Januari 2021

Ujumbe wa wangalizi kutoka mataifa wanachama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki pamoja na Jumuiya ya Maendeleo ya Pembe ya Afrika, IGAD unaofatilia uchaguzi mkuu wa Uganda, umefafanua kuwa hautaingilia kuhoji taratibu kadhaa zilizowekwa kwa tume ya uchaguzi ya nchi hiyo. Waangalizi hao wamesema watafuatilia shughuli hiyo na kutoa maoni yao kuhusu mafanikio na changamoto zitakazojitokeza.

https://p.dw.com/p/3nmIi

Huenda wapiga kura nchini Uganda wasitarajie mabadiliko yoyote katika mchakato mzima wa uchaguzi kutoka kwa waangalizi wa Afrika, kabla, wakati na baada ya zoezi hilo.

Hii ni kwa sababu ujumbe huo unalenga tu kuorodhesha mafanikio na changamoto zitakazoikumba shughuli hiyo kwa mujibu wa mwongozo wa Tume ya Uchaguzi ya Uganda pamoja na nadharia ya kujenga utawala wa kidemokrasi barani Afrika.

Kiongozi wa ujumbe wa Afrika Mashariki ni aliyekuwa rais wa Burundi kati ya mwaka 2003 hadi 2005 Domitien Ndayizeye.

Jukumu la ungalizi litakuwa lipi?

Uganda IGAD Wahlbeobachtermission
Kiongozi wa ujumbe wa waangalizi wa Jumuiya ya IGADFegessa Siraj (kulia) akizungumza na waangalizi wengine mjini Kampala.Picha: Lubega Emmanuel/DW

Kulingana na ujumbe huo, jukumu lao ni kuhimiza utawala mwema na wa kisheria katika mazingira wazi yanayotanguliza haki na usawa kwa wote katika zoezi kama hilo linalolengwa kujenga demokrasia.

Kwa msingi huo ndipo watatoa tathmini yao kuhusu uchaguzi utakaofanyika siku ya Alhamisi wiki hii.

Lakini wadau mbalimbali wametoa maoni kuwa ujumbe wa wangalizi usifumbie macho vitendo na matamshi kutoka kwa vyombo vya usalama na wakuu wao kwani ndivyo vinaweza kuchochea ghasia katika uchaguzi.

Wakati zikisalia siku mbili uchaguzi kufanyika, watu wengi wameamua kufunga shughuli zao za kujiingizia kipato na kusafiri kwenda vijijini.

Baadhi wameelezea kuwa wanahofia ghasia kutokea au manyanyaso ya vyombo vya usalama ambavyo askari wake wameweka doria sehemu mbalimbali mji mkuu, Kampala.

Ujumbe wa wangalizi umewahimiza kutohofia chochote ila washiriki katika uchaguzi kwani ndiyo fursa ya pekee ya kudhirisha matarajio yao kwa wale watakaoshinda katika uchaguzi mkuu.